Je ni kweli kwamba mitandao ya kijamii huboresha maisha ya watu?

INSTAGRAM

Chanzo cha picha, Reuters

Matumizi ya mitandao ya kijamii ni mojawapo ya shughuli maarufu zaidi duniani. Mwaka 2018, watu bilioni 2.65 walikadiriwa kuwa watumiaji wa mitandao kote duniani

Hata hivyo idadi hiyo inatazamiwa kuongezeka na kufikia bilioni 3.1 mwaka 2021.

Watumiaji nao wamekua wakiongezeka ambapo Januari peke yake mwaka 2019 waliongezeka kwa asilimia 45.

Nchini Tanzania mtandao wa Instagram umekua maarufu sana na wenye watumiaji wengi, kwa matumizi ya burudani na biashara.

Wengi hutumia kama njia ya kupata marafiki ama kuwafuatilia watu wenye ushawishi katika jamii ikiwemo wasanii wa filamu na muziki.

Ingawa wapo watu ambao hupata umaarufu hata bila kuwa wasanii.

Maelezo ya picha,

Aristote Kagombe ni mmoja wa watu waliojipatia umauarufu mkubwa nchini Tanzania kupitia ukurasa wake wa Instagam

Aristote Kagombe ni mmoja wa watu waliojipatia umaarufu mkubwa nchini Tanzania kupitia ukurasa wake wa Instagam wenye wafuasi zaidi ya laki tano.

Yeye hufanya biashara ya saloon, anasema amekua mbunifu kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo wateja wake ambao ni wanawake wanaofika kwenye ofisi yake na kutengeneza nywele baada ya hapo huwapa burudani.

''Unapokua mbunifu kuna baadhi ya vitu lazima uvibuni ili biashara yako iwe nzuri na iweze kuvutia watu ,Na kila mtu aweze kukubali unachokifanya''

Anasema yeye ni mmoja kati ya watu ambao wamenufaika sana na matumizi ya mitandao ya kijamii hasa instagram ambayo ndio yeye hutumia sana na imemfanya kuwa maarufu na amenufaika nao.

Lakini mbali na Aristote, Piere Gumbo ni moja kati ya watu waliopata umaarufu nchini Tanzania ,yeye hujulikana kama Mzee wa Liquid ama Konki Fire Yeye hakua akifahamika hapo awali lakini baada ya video yake kusambaa kwenye mitandao na kumuibua.

Maelezo ya picha,

Mzee wa Liquid ama Konki Fire

Mwenyewe hakuwa na ufahamu wa kutumia mtandao wakati anaanza kujulikana na hata hakua akifahamika kabisa kwenye mitandao.

Piere anasema yeye anafurahi kuona watu wanacheka kwa sababu yake bila ukorofi wa aina yeyote.

''Sikuweza kujua kuna siku nitakua maarufu, ama kupanda ndege, lakini mitandao ya kijamii imekua sambamba pamoja na mimi tusidharu mitandao tuiheshimu na tuipende,''Piere anaeleza.

Nimenufaika na mambo mengi sana, kwanza mfukoni kuwa na laki moja laki mbili (Dola 50 mpaka 100) lilikua suala la shida yani shida kidogo lakini kwa sasa mambo si mchezo ,ndio maendeleo hayo.''

Maelezo ya picha,

Mzee wa Liquid ama Konki Fire apachikwa jina la mtaa

Mitandao mbalimbali ya kijamii hufanya watu kujiingizia fedha kutokana na idadi ya wafuasi walionao .

Kwa mfano mtandao kama Facebook hutoa fursa kwa makampuni ama wafanya biashara kuwafikia watu moja kwa moja na huwawezesha kuona maoni ya wafuasi/wateja wao ,mawazo yao ni yapi na kipi hasa wamekipenda.

Watu hawa maarufu ama wenye wafuasi wengi hukiri mara zote kunufaika pale unapotumia vizuri mtandao.

Mbali na watu maarufu, wananchi wa kawaida nao hufungua kurasa zao na kutumia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twiter, Instagram na kuunda makundi kupitia mitandao.

Na wao wanakiri kunufaika na mitandao hasa katika masuala ya kibiashara

Lakini ukiachilia mbali suala la watu binafsi kuitumia mitandao ya kijamii kwa simu wanazozimiliki wenyewe bado zipo sheria zinazowabana ili wasitumie vibaya mitandao ama kurasa zao.

Mataifa mengi yameweka sheria mbalimbali ili kuweza kudhibiti matumizi mabaya.

Nchini Tanzania iliundwa sheria mpya ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015 ,taifa la Uganda likiweka tozo kwa watumiaji wa Internet huku Kenya nayo ikipitisha sheria kali ya makosa ya kimtandao.