''Trump alivunja sheria kwa kuzuia msaada wa Ukraine ambao tayari ulikuwa umepitishwa na bunge'', lasema shirika

Rais Donald Trump
Image caption Ikulu ya Whitehouse imedaiwa kuvunja sheria kwa kuzuia msaa ambao tayari ulikuwa umepitishwa na bunge la Congress

Ikulu ya White house ilivunja sheria kwa kuzuia ufadhili ambao tayari ulikuwa umeidhinishwa na bunge la Congress , limesema shirika moja nchini humo.

Uamuzi huo wa afisi hiyo inayohusika na jukumu la kuiwajibisha serikali GAO ni pigo kubwa kwa rais Donald Trump huku akikabiliwa na kesi katika bunge la seneti.

Anatuhumiwa kuzuia ufadhili ili kuishinikiza Ukraine kumchunguza mpinzani wake wa kisiasa.

Kwa nini ilikuwa makosa kuuzuia msaada huo?

''Sheria haimruhusu rais kuweka mbele malengo yake ya kibinafsi badala ya yale ambayo yaliidhinishwa na bunge la Congress na kufanywa kuwa sheria'', ulisema uamuzi huo wa Gao.

''Afisi ya Ikulu ya Whitehouse inayosimamia bajeti , OMB ilizuia fedha kwa sababu ya sera, swala ambalo haliruhusiwi chini ya sheria ya udhibiti'' , lilisema shirika hilo.

Ikulu ya Whitehouse imesema kwamba inapinga maono yaliotolewa na Gao , ikilishutumu shirika hilo kwa kujiingiza katika utata wa vyombo vya habari .

Hatahivyo wanachama wa Democrats waliupongeza uamuzi huo.

Haki miliki ya picha Getty Images

Katika mahaojiano na vyombo vya habari mapema siku ya Alhamisi , Spika wa bunge la Congress Nancy Pelosi alisema kwamba ikulu ya Whitehouse ilivunja sheria.

Hapo awali mshirika wa karibu wa wakili wa Rais wa Marekani Rudy Giuliani alidai kuwa Donald Trump "alijua kila kitu kinachoendelea" kuhusu kushinikizwa kwa Ukraine kuwachunguza Makamu wa Rais mstaafu Joe Biden pamoja na mtoto wake.

Lev Parnas amekiambia kituo cha runinga cha MSNBC kuwa Guilani alikuwa hachunguzi tuhuma za rushwa bali namna ya kumchafua Biden ambaye anaonekana kuwa kinara wa tiketi ya kiti cha Urais kupitia chama cha Democrats.

Rais Trump anakanusha vikali madai hayo.

Wakati hayo yakijiri, Baraza la Wawakilishi nchini Marekani limepiga kura kuidhinisha kutumwa kwa mashtaka dhidi ya Rais Donald Trump kwenda katika Baraza la Seneti ikiwa ni hatua ambayo inaashiria kuanza kwa kesi inayoweza kumuondoa madarakani.

Bw Parnas ambaye anakabiliwa na kesi ya jinai amedai kuwa rais Trump anadanganya na anajua wazi masharti waliyopwapa Ukraine kuwa kama usingefanyika uchunguzi dhidi ya Biden na mwanawe Hunter ambaye alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya gesi Ukraine, basi msaada wa kijeshi kwa nchi hiyo kutoka Marekani ungesitishwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Lev Parnas adai kuwa Trump anajua fika kila kitu kilichofanyika.

"Nisingeweza kufanya chochote bila idhini ya Rudy Giuliani ama raisi (Trump). Kwa nini wandani wa rais (wa Ukraine) Zelensky kama waziri (wa mambo ya nje, Arsen) Avakov ama watu kama rais (mstaafu, Petro) Poroshenko wakutane na mimi?

"Mimi ni nani? Waliambiwa wakutane nami. Na hiyo ndiyo siri wanayojaribu kuificha. Nilikuwa kibaruani nikifanya kazi yao," ameeleza Parnas.

Kesi dhidi ya Trump kutua Seneti

Kesi hiyo imepelekwa Seneti katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja tangu wabunge wa Baraza la Wawakilishi kumkuta na hatia Rais Trump ya matumizi mabaya ya madaraka na kuzuia juhudi za Bunge kuchunguza vitendo vyake.

Wabunge wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha azimia hilo kwa kura 228 dhidi ya 193. Huku Spika Nancy Pelosi akisaini uamuzi huo sambamba na timu ya Wabunge wa Democratic ambao wataendesha mashtaka ya kesi hiyo inayomkabili Rais Trump.

Mameneja wameteuliwa leo na spika kwa ajili ya kuendesha mashtaka kutokana na kupeleka ambacho kimepitishwa. masetena kama wazee wa baraza na baadaye kupiga kura.

Haki miliki ya picha BBC Sport
Image caption Wawakilishi wa Democrats wakipeleka hati ya mshtaka dhidi ya Trump katika bunge la Seneti

Baraza hilo la Wawakilishi ambalo linadhibitiwa na chama cha upinzani cha Democrats, kutaka Rais Trump kuondolewa madarakani.

Hata hivyo Baraza la Seneti ambalo linadhibitiwa na chama tawala kinachoongozwa na Rais Trump, kitaamua aidha kumtia hatiani na kumuondoa madarakani. Jambo ambalo halitarajiwi.

Katika mkutano na wanahabari kabla ya kutia saini hati, Bibi Pelosi alisema: ''Leo tutaweka historia tutakapo peleka hati za mashtaka dhidi ya rais wa Marekani kwa vitendo vyake vya matumizi mabaya ya madaraka na kuzuia majukumu ya bunge kushughulikia suala hilo''.

Hati hizo kisha zikapelekwa kwenye baraza la seneti, ambapo kiongozi wake ni Mitch McConnell kutoka chama cha Republican amesema zitawasilishwa siku ya Alhamisi mchana, zoezi litakalofuatiwa na kusikilizwa kesi siku ya Jumanne juma lijalo.

Iwapo Seneti itamlinda Trump (uwezekano ni mkubwa), sasa ni nini maana ya mchakato wote huu?

Image caption Donald Trump amekuwa rais wa tatu katika historia ya Marekani kupigiwa kura ya matumizi mabaya ya madaraka

Kama uliwasikiliza Democrats, sababu iliyowafanya wapitie yote haya hata kama mtazamo ni kwamba uwezekano wa Seneti (ambayo inatawaliwa na chama cha Trump, Republican) wa kumpata na hatia ni mdogo sana au haupo ni kwa sababu wanahisi wanawajibu wa kumuwajibisha rais kwa matendo yake.

Wanamtazama rais kama mtu aliyetumia vibaya mamlaka aliyonayo kuishinikiza Ukraine kuanzisha uchungzi dhidi ya hasimu wake wa kisiasa, na kama hawatachukua hatua ,hata kama haitawezesha kuondolewa kwake madarakani , rais atalazimika kuchukua hatua zaidi ambazo zinaweza kuwa na athari kwa Democrat katika uchaguzi wa mwaka huu.

Halafu kuna ukweli halisi wa kisiasa kwamba makao makuu ya Democrat yamekua yakijiandaa kwa uchunguzi huu kwa miezi kadhaa.

Kama maafisa wakuu wa Democrat wasingelichukua hatua, wangekuwa katika hatari ya kuwakosa wafuasi wao au kukabiliwa na changamoto katika uchaguzi wa majimbo au kupoteza ufuasi katika uchaguzi mkuu kwa sababu wafuasi wao wasingehisi kuwa na msukumo wa kutosha wa kurejea katika uchaguzi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii