Kenya Airways, RwandaAir wasitisha safari zake kuelekea China kwa hofu ya corona

Kenya airways

Chanzo cha picha, Getty Images

Shirika la ndege la Kenya limesitisha safari zote za kwenda China baada ya mlipuko wa virusi vya corona.

Virusi hivyo vimesababisha vifo 213 nchini China na maambukizi kwenye mataifa mengine 16.

Visa sita vya maambukizi vimeripotiwa barani Afrika ingawa wagonjwa waliofanyiwa vipimo wamekutwa kuwa hawana maambukizi ya virusi hivyo.

Nchini Kenya, siku ya jumanne, mwanafunzi aliwekwa karantini hospitalini katika mji mkuu Nairobi, baada ya mwanafunzi huyo kutokea katika mji wa Wuhan nchini China, eneo ambalo ndio chimbuko la mlipuko huo.

Kenya Airways imesema kuwa bado iko kwenye mazungumzo na wizara ya afya na wizara ya mambo ya nje kuhusu muda ambao ndege hizo zitaacha safari ya China.

Lakini safari za mji mkuu wa Thailand, Bangkok, zitakuwa zinaendelea.

Chanzo cha picha, TWITTER

Rwanda

RwandaAir nayo pia imesitisha safari zake za kwenda mji wa Guangzhou nchini China kuanzia leo tarehe 31, Januari 2020 mpaka taarifa zaidi zitakapotolewa hapo baadae.

Mabadiliko hayo yametangazwa baada ya shirika la afya duniani (WHO) kutangaza kuwa virusi vya corona ni janga la afya kimataifa.

Abiria ambao watakuwa wameathirika katika mabadilko hayo, watarudishiwa nauli zao, kuruhusiwa tiketi zao kupelekwa kwa tarehe za mbeleni au kubadilishiwa safari.

Chanzo cha picha, Twitter

Safari za Kigali mpaka Mumbai zitakuwa zinaendelea.

Shirika hilo la ndege limeomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.

Shirika la ndege la Morocco-Royal Air Maroc imesema kuwa safari za ndege zake kwenda China zitasitishwa mpaka mwishoni mwa mwezi wa Februari kwa sababu watu wanaoenda ni wachache wakitokea Casablanca mpaka Beijing.

Wakati huohuo Madagascar nayo imesema kuwa ndege zake zimesitisha safari zake kutoka Guangzhou kuanzia siku ya jumamosi ikiwa ni hatua ya kujikinga.

Air Mauritius pia imesitisha safari zake za ndege kutoka Shanghai kuanzia leo siku ya ijumaa lakini ndege zote za kwenda Hong Kong zitaendelea na safari zake.

Ethiopia

Ethiopian airline, ni ndege ambayo hufanya safari nyingi Afrika, yenyewe imetangaza siku ya alhamisi kuwa safari zake zote za kuelekea China zitaendelea.

Ndege hiyo bado inafanya kazi na mamlaka ya Ethiopia na China kuwalinda abiria wake pamoja na wafanyakazi wake na virusi vya corona.

Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Vilevile shirika la ndege la Air Tanzania limesema kwamba litalazimika kuahirisha safari zake kutoka mjini Dar es Salaam kuelekea China , kutokana na wasiwasi kuhusu kuenea kwa virusi vya Corona ambavyo vimewaua watu 133 kulingana na chombo cha habari cha Reuters.

Air Tanzania ilikuwa imepanga kuanzisha safari za kuelekea China mwezi ujao kabla ya uzinduzi wake wa safari za kila siku hadi katika soko hilo muhimu la utalii barani Asia.

''Tayari tumepokea kibali kuanza safari zetu kuelekea China'' , alisema mkurungezi wa shirika hilo la serikali Ladislaus Matindi akizungumza na chombo cha habari cha Reuters.

''Lakini sasa tutalazimika kuchukua tahadhari zilizowekwa …tutaamua lini tutazindua safari zetu za kwanza kuelekea China baada ya kuangazia maswala yote yanayolinda usalama wa abiria''.

Utalii ndio kipato kikuu cha fedha za kigeni nchini Tanzania , ilio maarufu kwa safari zake za mbugani na fukwe zake nzuri za bahari.