Siku ya Wanawake Duniani 2020: Msusi asiyekuwa na uwezo wa kuona anavyojikimu kimaisha Uganda

Aisha Bahati
Maelezo ya picha,

Aisha Bahati akiwa kazini

Kama wasemavyo ulemavu sio kutojiweza na pia kuna walio na ulemavu ambao wanaweza kuchangia pakubwa katika kuboresha maisha ya wenzao.

Wakati tunaelekea kuadhimisha siku ya wanawake duniani hebu tumuangazie mwanamke mwenye ulemavu wa macho, bi. Aisha Bahati ambaye ni mfano wa kuigwa na wengi kutokana na kazi yake na mikakati yake ya kusaidia walemavu wengine ambao hawajiwezi.

Mwandishi wa BBC, Issaac Mumena alimtembelea bi .Aisha katika saluni yake inayoitwa Asumi iliyoko jijini Kampala, Uganda.

Bi.Aisha ambaye ni mmiliki na msusi wa saluni hiyo ambaye anasuka mitindo mbalimbali.

Ni miaka minne sasa tangu aanze kazi hiyo na bi.Aisha anasema anafurahia kazi yake kwa kuwa ndio inamsaidia kupata mahitaji yake muhimu.

Huku upande wa wateja nao pia wanamiminika katika saluni hiyo nao wanaridhika na utendaji wake ndio maana wanafika hapo kwa wingi.

"Anasuka vizuri, tunang'ara na kupendeza, watu wegine huwa wananiuliza huwa nasuka wapi maana kuna watu ambao wanaona lakini hawajui kusuka vizuri kama yeye" mteja aliyekuwa anayesukwa.

Bi.Aisha hakuzaliwa akiwa mlemavu, aliugua malaria akiwa na miaka tisa na asnasema alipelekwa hospitali na dawa aliyochomwa sindano ilikuwa imepita muda hivyo ikamdhuru na kuwa kipofu sasa.

Maelezo ya picha,

Aisha Bahati akiwa na mama yake

Aisha ni mlemavu wa macho lakini pamoja na upofu wake kile anachokipata anawapatia walemavu wengine wasio jiweza, sio kazi rahisi kwa mtu kipofu kupata pesa kwa urahisi anafahamisha jinsi anavyoweza kupata pesa na kuwapatia wenzake:

"Nilikuwa 'Miss Tourism Independent Uganda, hivyo nilikuwa kiongozi ya walemavu Uganda, hivyo nilikuwa naweza kwenda kuwaombea msaada wenzangu kama viatu, nguo na mahitaji mengine.Sina pesa mimi kama mimi ingawa huwa ninaongezea ila kikubwa ninajivunia kuwa naweza kuwasaidia wengine pia."

Wiki hii dunia inakwenda kuhadhimisha siku ya wanawake duniani bi.Aisha anatowa wito kwa walemavu wenzake hususani wanawake:

"Watu wanapaswa kukumbuka kuwa ukiwa mlemavu si mwisho wa dunia,wengine hawana macho, hawana miguu lakini hawapaswi kufikiria hivyo "

Sasa ni miaka 20 tangu macho ya Aisha yalipoharibika na kuwa kipofu, lakini bado anamatumani ya siku moja kuona kama alivyofahamishwa na madakitari.

"Daktari amethibitisha kuwa macho yangu yako vizuri lakini ninahitaji milioni 25 za Uganda ili nifanyiwe upasuaji".

Mbali na upofu wake, Aisha ni mfano wa wanawake wajasiriamali ambao mchango wao kwa jamii unastahili kupongezwa wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya wanawake