Coronavirus: Raia wanne wa kigeni walioingia na mafua Uganda watengwa

Ukaguzi wa kimatibabu

Chanzo cha picha, EPA

Raia wanne wa kigeni waliowasili nchini Uganda na dalili za virusi vya corona wametengwa katika hospitali ya Entebbe, Waziri wa afya amethibitisha.

Bila ya kutaja uraia wao, afisa mahusiano wa waziri wa afya bwana Emmanuel Ainebyoona alisema kuwa raia hao wamechukuliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe.

"Sampuli ya vipimo vyao vimepelekwa katika kituo cha utafiti wa virusi nchini humo (UVRI). Na tutaitaarifu umma " gazeti la Daily Monitor limemnukuu.

Wizara ya afya imewataka wananchi kuwa watulivu na kufuata hatua za kujikinga na ugonjwa wa corona kwa sababu hakuna udhibitisho wa kuwa virusi hivyo vimeingia nchini humo.

Aidha mwandishi wa BBC nchini Uganda amesema kuwa waziri wa afya nchini humo, ametoa agizo kwa wageni wanaotoka katika nchi zilizoathirika na virusi vya corona watengwe kwa muda wa siku 14.

Zaidi ya visa 85,000 vya ugonjwa wa coronavirus vimethibitishwa katika nchi 57 kote duniani huku vifo 3,000 vikithibitishwa, kulingana na Shirika la Afya Duniani.