Waridi wa BBC: 'Mume wangu alizoea kunilawiti na kunibaka'

  • Anne Ngugi
  • BBC Swahili
Virginia Wangari, mama wa miaka 46 anayedai kuwa kwenye ndoa ambayo mume wake aliyekuwa na tabia ya kumbaka na kumlawiti

Chanzo cha picha, Virginia Wangari

Maelezo ya picha,

Virginia Wangari, mama wa miaka 46 anayedai kuwa kwenye ndoa ambayo mume wake aliyekuwa na tabia ya kumbaka na kumlawiti

Virginia Wangari anakumbuka jinsi mume wake alivyobadilika kutoka kuwa kipenzi na kuwa kama hayawani baada ya kuishi naye kwa kipindi cha miaka 20.

Katika maisha yao ya ndoa, kabla mambo hayajabadilika, walikuwa wamejaliwa watoto 11. Baadaye alijaliwa malaika wa 12.

Madhehebu ya dini ya Kikristo ambayo mumewe Wangari alikuwa anaongoza yalikuwa yanafuata mafundisho kwamba wanawake hawafai kupanga uzazi.

Kutokana na hilo, alijipata akijifungua mtoto baada ya mwingine kwa kipindi cha miaka 20 waliyoishi pamoja.

'Utabiri kutoka kwa Mungu'

Bi Wangari anasema mambo yalianza kubadilika pale mumewe, alipomweleza kuwa 'Mungu' alikuwa amemtabiria kwamba hafai kuwa mke wake tena.

Alifahamishwa hayo wakati wa maongezi ya kawaida tu wakila chakula cha jioni mbele ya watoto wao.

Mumewe alikatiza mtiririko wa gumzo na aliwaeleza watoto kuwa mama yao 'Virginia' alikuwa amerukwa na akili na kwamba wasimtambue tena kama mama.

"Kuanzia hapo nilianza kulala kwenye chumba tofauti na mume wangu. Nilikuwa na ujauzito wa miezi 7. Nilitengwa na watu wengine na nikawa kama mfungwa ndani ya nyumba yangu," Virginia anakumbuka.

Kuishi kwake kulitegemea watoto wake waliomfichia chakula na maji.

Chanzo cha picha, Virginia Wangari

Wakati wa kujifungua ulipowadia, aliruhusiwa kutoka chumbani lakini ilimbidi ajikokote mwenyewe hadi hospitalini kwa kuwa hakuna aliyekuwa anamshughulikia.

Anakumbuka kuwa alijifungua katika mazingira ya uchungu mwingi kuliko kawaida.

Mtoto wake alitangulia kwa miguu na ikawa safari ndefu mno ya uchungu usio na kifani.

"Baada ya kujifungua hakuna aliyenitembelea hospitalini kuniona, hata mume wangu alinitekeleza kwa muda niliokuwa hospitalini," anasema.

"Baada ya kuona kuwa sina wa kunisaidia, niliporuhusiwa kuondoka hospitalini, nilianza safari ya kuelekea nyumbani, nikiwa nimempakata mwanangu mchanga. Kichwani mlijaa kero na maswali mengi ya ni jambo gani nililolitenda kustahiki kutendewa unyama huo," Virginia anasema.

Alipofika nyumbani hakupata wa kumlaki. Watoto walikuwa wameamrishwa na baba yao kutoshirikiana wala kusema naye.

Kutengwa na kubakwa

Virginia alielekea kwenye chumba alichokuwa ametengewa. Kwa kipindi cha mwezi mmoja mumewe hakufika hata kumpakata mtoto, wala kumjulia hali mkewe.

Baada ya muda, Virginia anadai kuwa mumewe alianza kuingia kwenye chumba alimokuwa analala kwa hasira huku akimtusi na kumchapa.

Wakati huo alikuwa angali anamnyonyesha mtoto ambaye alikuwa na miezi 3.

Mtoto alitenganishwa na mama kwa nguvu, huku akipokezwa bintiye aliyekuwa kifungua mimba kuwa mlezi.

Chanzo cha picha, Virginia Wangari

Maelezo ya picha,

Virginia Wangari akiwa na mtoto wake wa 11

"Baada ya kutenganishwa na mtoto wangu, mume wangu alianza kunibaka, kunilawiti na kunirushai matusi kila mara," anasema.

"Kila usiku alikuwa akiingia chumbani na kunitendea unyama. Kwa sababu ya kumpenda mume wangu na ile hali ya kunyenyekea sikupiga kelele wala kufanya fujo dhidi ya maovu aliyokuwa ananitendea."

Mambo yalizidi kuwa mabaya kila jua lilipochomoza.

Mateso yalizidi na kuendelea kuuvunja moyo wa Virginia.

Kipindi hicho Virginia alishika mimba ya mtoto wa 12, katika pilkapilka za kubakwa.

Pale nyumbani kwake mwanamke aliyekuwa rafiki wa karibu wa Virginia ndiye aliyekuwa anahakikisha kuwa shughuli za nyumbani zinafanywa.

Virginia hakudhania kuwa yule mama mwenye watoto 5 alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake pale pale nyumbani kwake.

Yule mama wote walikuwa wanahudumu kwenye madhehebu moja.

Kufukuzwa nyumbani

Baada ya sita, siku mmoja mumewe Virginia alimwambia afunganye virago vyake kwani alikuwa ameamua kumrejesha nyumbani kwao.

Alitoa sababu kuwa Virginia alikuwa mchawi na alikuwa silo mke wake tena.

Kwa hivyo Virginia alipelekwa kwa nguvu hadi kwa mama yake mzazi. Walipofika Virginia anakumbuka mumewe alivyomchongea na kumlimbikizia lawama.

"Mama alielezwa kuwa amenirejesha nyumbani kwa kuwa nilikuwa na lengo la kuwapa watoto wangu sumu, na kumroga mume wangu. Na kwa hivyo ilikuwa muhimu nisiwe karibu na watoto wangu tena."

Ni kana kwamba mama yake Virginia alimwamini mumewe kwani alianza kuhisi mabadiliko kwenye uhusiano wake na mamake.

Alianza kuwa mkali kwake na kushirikiana na kumuunga mkono mumewe.

Chanzo cha picha, Virginia Wangari

Kuondoka bila chochote

Virginia alifukuzwa kutoka kwenye ndoa yake bila chochote. Alizuiwa kuondoka na watoto wake au hata kutangamana nao. Alilazimika kumwacha mtoto wake kitinda mimba akiwa na umri wa mwaka mmoja.

Kwa mamake hakukuwa kimbilio salama.

"Ilibidi nitoroke nyumbani kwa mamangu. Nilipanga njama. nilitafuta marafiki wengine kunisaidia kuanza maisha upya. Nilianza kuishi katika vitongoji duni," anasema.

"Nakumbuka nilikuwa mjamzito, nilianza kufulia watu nguo kama vibarua ili kukidhi mahitaji ya msingi."

Kuanza maisha upya bila kuwaona watoto wake na pia kufukuzwa kama mbwa kutoka kwa ndoa yake ni mambo ambayo yamekuwa yakimtatiza Bi Wangari.

Hadi wa leo, hajawahi kuonana hata kidogo na watoto sita aliowazaa tokea alipofukuzwa nyumbani.

Cha ajabu ni kuwa, yule rafiki yake wa kike waliokuwa wanahudumu wote kanisani amekuwa sasa ndiye aliyeirithi nafasi yake kama mke.

Virginia anasema kuwa mkondo wa sheria haujampa haki yake kama mama. Amejaribu mara kadhaa kupatanishwa na watoto wake bila mafanikio.