Virusi vya Corona: Ubalozi wa Marekani Tanzania waendelea kutoa tahadhari juu ya maambukizi

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari mpya ya afya

Chanzo cha picha, AFP

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari mpya ya afya na kusisitiza kuwa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona bado ipo juu jijini Dar es Salaam.

Tahadhari hiyo iliyotolewa Jumanne jioni na kuchapishwa kwenye tovuti ya ubalozi na mitandao ya kijamii ya ubalozi huo inaendelea kuonya raia wan chi hiyo waliopo Tanzania na hususani jijini Dar es Salaam kuendelea kuchukua tahadhari.

Hatua hiyo inakuja wiki moja toka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania kumuita na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani Bi Imni Peterson juu ya tahadhari zilizotolewa hapo awali.

Katika taarifa iliyotolewa na serikali baadaye ilieleza kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo Wilbert Ibuge alieleza masikitiko yake juu ya namna Ubalozi huo umekuwa ukitoa tahadhari zake.

Suala kuu ambalo wizara ililalamikia ni juu ya ubalozi kudai kuwa hospitali nyingi jijini Dar es Salaam (bila ya kuzitaja hospitali hizo) zimefurika wagonjwa wa COVID-19 jambo ambalo serikali inasema si kweli.

Juu ya suala hilo la kuelemewa kuwa, katika tahadhari hii mpya, ubalozi umeeleza: "Vituo vya afya Tanzania vinaweza kuelemewa kwa haraka katika janga la kiafya. Kumekuwa na nyakati ambazo wakati wa mlipuko wa COVID-19 ambapo hospitali jijini Dar es Salaam zilifikia ukomo kwa kupokea wagonjwa wengi wa COVID-19."

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dkt Elisha Osati hivi karibuni aliimbai BBC kuwa mfumo wa afya nchini humo haujaelemewa na corona.

Kama ilivyokuwa awali, tahadhari mpya imeeleza kuwa takwimu mpya za ugonjwa wa corona ikiwemo vifo hazijatolewa nchini Tanzania toka Aprili 29.

Chanzo cha picha, AFP

Hata hivyo, serikali ya Tanzania imeendelea kusisitiza kuwa kasi ya ugonjwa wa corona imepungua. Kutokana na hali hiyo Rais John Pombe Magufuli ameruhusu kwa baadhi ya shughuli zilizokuwa zimefungwa awali kama ligi kuu ya kandanda, masomo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kidato cha sita kurejea.

Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu Jumatatu wiki hii alieleza kuwa "kuna wagonjwa wanne tu wa corona ambao bado wamelazwa hospitali kwa Tanzania Bara."

Tahadhari hiyo inaonya raia wa Marekani kuwa kuna uwezo mdogo wa hospitali nchini Tanzania ambao unaweza kusababisha ucheleweshwaji wa huduma na kuhatarisha Maisha yao.

Ubalozi huo katika tahadhari iliyopita ya Mei 25 ilieleza kuwa hakukuwa na mpango wa karibuni wa kuleta ndege ya kuwaondosha raia wake nchini humo.

Katika tahadhari mpya, umeeleza raia wake kuwa kutokana na serikali ya Tanzania kuruhusu ndege za abiria za kimataifa kurejesha safari zake tayari kuna mashirika ya ndege ambayo yameanza huduma toka Juni 1.