Pierre Nkurunziza:Nchi za Afrika mashariki zamuomboleza Nkurunzinza

nKURUINZINZA

Tanzania, Kenya na Rwanda ambazo ni nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameungana kumuomboleza rais wa Burundi Piere Nkurunziza aliyefariki ghafla Jumatatu wiki hii.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo zinazoanza Jumamosi Juni 13. mpaka 15 Juni 2020 na bendera zote kuwa nusu mlingoti.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari rais Magufuli amesema kuwa Tanzania inatoa heshima hiyo kwa hayati Nkurunzinza kwa kutambua kuwa alikuwa rais wa nchi jirani ambaye amekuwa na mahusiano mazuri na ushirikiano mzuri wa kindugu, kirafiki na kihistoria na Tanzania.

Chanzo cha picha, IKULU

Maelezo ya picha,

Rais Nkurunziza akiwa na mwenyeji wake Rais John Magufuli baada ya kufika Ngara, kaskazini magharibi mwa Tanzania, Julai 2017

"Burundi ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki na rais Nkurunzinza alipenda sana jumuiya hii, pia alipenda Tanzania na alishirikiana nasi kila alipohitajika, hivyo nimeona watanzania tuungane na ndugu zetu kuomboleza na kumkumbuka rais Nkurunzinza ambaye aliona Tanzania kama nyumbani" alisema rais Magufuli.

Nchini Kenya Rais Uhuru Kenyatta, ametoa maelekezo bendera ya chi hiyo na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kupeperushwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Jumamosi kwa heshima ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.

"Bendera zitapeperushwa nusu mlingoti katika majengo yote ya umma nchini na katika balozi zote za Kenya nje ughaibuni," taarifa iliyotolewa na Ikulu ya rais ilisema.Rais Kenyatta pia ametuma rambirambi zake kwa familia ya Nkurunziza, aliyefariki Jumatatu akiwa na umbra wa miaka 55, kutokana na mshtuko wa moyo.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais Paul Kagame na aliku

Wakati kwa upande wake Rwanda, Rais Paul Kagame ametangaza kuwa bendera za taifa la Rwanda pamoja na bendera za Afrika Mashariki zipapepeka nusu mlingoti kuanzia Jumamosi Juni, 13 mpaka siku ambayo hayati Pierre Nkurunzinza atakapozikwa.

Marais wote wametuma salamu za rambirambi kwa warundi na familia ya marehemu.

Nkurunziza ni nani?

Pierre Nkurunziza amekuwa mwanasiasa wa Burundi na kuwa madarakani tangu mwaka 2005.

Bwana Nkurunziza, kijana wa aliyekuwa mbunge, alinusurika mauaji 1993 ya wanafunzi wa Kihutu katika chuo kiuu cha Burundi ambapo alikuwa mhadhiri na kujiunga na waasi wa FDD kundi ambalo baadae lilibadilika na kuwa chama tawala cha CNDD-FDD ambacho alikuja akawa kiongozi.

Alikuwa mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, hadi alipochaguliwa kama rais wa Burundi.

Maelezo ya video,

Safari ya kisiasa ya Pierre Nkurunziza nchini Burundi

Baada ya makubaliano ya Amani ya Arusha kati ya serikali na waasi, Nkurunziza alitajwa kuwa waziri wa mambo ya ndani kabla ya bunge kumchagua kama rais Agosti 2005.

2015, Nkurunziza alichaguliwa katika uchaguzi uliokuwa na utata na chama chake kwa muhula wa tatu madarakani.

Wafuasi wake na wanaompinga Nkurunziza walikosa kukubaliana katika suala la ikiwa ilikuwa halali kwake kugombea tena na maandamano yakafuata.