Olduvai Gorge: Zana zilizotumiwa na binadamu miaka milioni mbili iliyopita zagunduliwa Tanzania

  • Yusuph Mazimu
  • BBC Swahili
fuvu
Maelezo ya picha,

Ugunduzi huo umefanyika katika bonde la Oltupai maarufu kama Olduvai Gorge, kwenye Kreta ya Ngorongoro.

Wanaakiolojia wamegundua zana za mawe zilizotumika miaka milioni mbili iliyopita na binadamu wa kale zaidi katika eneo la Bonde la Olduvai, Kaskazini mwa Tanzania.

Ugunduzi huo unatoa mwanga mpya juu ya namna binadamu wanaoaminika kuwa ni wa kale zaidi walivyoishi na kuyamudu mazingira yao. Ugunduzi huo pia unatoa jibu la kwamba, binadamu wa kale aliishi miaka milioni mbili iliyopita na sio milioni 1.8 kama ilivyogundulika na watafiti wa awali.

Ugunduzi huo ni matokeo ya utafiti uliochukua miaka mitatu na ulihusisha watafiti kutoka ndani na nje ya Tanzania.

''Tulianza utafiti mwaka 2017, ikatuvutia tukarudi mwaka 2018, tukitoka Olduvai tunarudi maabara, maabara tunakutana na changamoto, tukaendelea kutafiti, kwa sababu tulitaka tufanye kisayansi kabisa, tuliendelea hivyo ili tusiache mashaka hata kidogo kuhusu miaka laki mbili iliyoongezeka,'' alisema Dkt. Pastory Bushozi, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye alikuwa mmoja wa watafiti washiriki.

Watafiti hao wamegundua zana za mawe za kale zipatazo 526 ambazo kwa muonekano wake zinaonesha uwepo wa zama mbalimbali za kuishi kwa mwanadamu.

"Katika kipindi hicho hicho tumegudua pia masalia ya wanyama tofauti wapatao 1,136 wakiwemo mamba, viboko na ndege na mabaki hayo yanaonesha kulikuwa na mazingira fulani ya uwepo wa mwanadamu," alisema Dk. Bushozi.

Nini kimesukuma utafiti huo kufanyika?

Watafiti hao wanasema waligundua uwepo wa viashiria vipya vya maisha ya mwanadamu katika eneo la Olduvai Gorge ambalo linaaminika kisayansi kwamba mwanadamu wa kale zaidi aliishi hapo.

Chanzo cha picha, Pastory Bushozi

Maelezo ya picha,

Imewachukua watafiti miaka mitatu kufikia ugunduzi wa mabaki hayo ya zana za miaka milioni mbili.

Aawali walienda kaskazini mashariki mwa Olduvai, chini ya miamba ambayo masalia ya mwanadamu wa zamani yalipatikana, waligundua uwepo wa udongo ambao uliashiria jambo jipya.

''Tulitaka kujua huko chini ya miamba kuna nini? Tulibaini kwamba, kulikuwa na milipuko ya volkano ambayo ilifunika eneo hilo kwa hiyo kabla ya hapo kulikua na maisha," alisema Bushozi.

Baada ya kutafiti zaidi, watafiti hao wakagundua kuwa katika kipindi cha miaka laki mbili cha baina ya binadamu aliyeishi miaka milioni 1.8 iliyopita (ambaye anatambulika rasmi kisayansi kama binadamu wa kale zaidi) na mabaki waliyogundua hivi punde (ya miaka milioni mbili iliyopita) kulitokea na milipuko minne ama mitano ya volkano.

Kubadilika kwa mazingira katika eneo hilo kukawafanya wanadamu wa wakati huo kutengeneza zana mbalimbali ambazo ndizo zimeonekana sasa kwenye utafiti huu mpya.

Zipo zana za mawe ambazo, zinaonyesha uwepo wa zama tofauti za mwanadamu wa kale, lakini kwa muundo wake zinaonyesha kuwa zilikuwepo kabla ya miaka milioni mbili iliyopita.

Bushozi alisema kugundua kwa masalia hayo na zana za mawe ya kale, kumewafanya watafiti hao kubaini kwamba katika eneo hilo binadamu wa kale alikuwepo kwa zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita, ikiwa ni miaka laki mbili zaidi ya ile inayotambulika sasa na wanasayansi.

Watafiti hao wanasema haikuwa kazi rahisi kutekeleza utafiti huo, kwa sababu ulileta maswali mengi kutokana na tafiti zingine za kisayansi za awali.

Utafiti huu mpya una maana gani kwa Tanzania?

Bonde la Oltupai (maarufu kwa Kiingereza kama Olduvai Gorge) ni eneo la kiakiolojia ni kati ya maeneo ya kale muhimu zaidi duniani.

Bonde hilo lipo katika hifadhi ya Ngorongoro na karibu na ile ya Serengeti, ni mahali ambapo zamadamu, viumbe wa kale waliokaribiana na mwili wa binadamu, waliishi tangu miaka milioni 2 hivi iliyopita, kwa mujibu wa utafiti wa sasa.

Chanzo cha picha, Pastory Bushozi

Maelezo ya picha,

Ugunduzi huo umewaachia maswali watafiti ambayo yanahitaji utafiti zaidi ili kuyajibu.

Eneo hili ni kivutio kikubwa cha cha watalii wengi wanaokuja nchini Tanzania, na mabaki ya mifupa ya wanyama kama tembo, kongoo wenye pembe kubwa na mbuni, mabaki ya fuvu la kichwa la Paranthropus boisei (pamoja na mumewe aliyeitwa kwanza Zinjanthropus) ambalo lipo katika makumbusho ya Dar es Salaam, yaliyogundulika tarehe 17 Julai 1959 na mwanaakiolojia Mary Leakey, ni baadhi ya vitu vinavyovutiwa watalii wengi.

Kwa mujibu wa watafiti hao, ugunduzi huo ni muhimu katika kuchochea utalii wa kiakiolojia nchini Tanzania.

Chimbuko la utafiti wa mwanadamu wa kale katika Bonde la Olduvai

Miongo sita iliyopita, ugunduzi mkubwa ulifanyika katika eneo hilo la bonde la Oltupai maarufu kama Olduvai Gorge, kwenye Kreta ya Ngorongoro.

Wanaakiolojia Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la mtu anayeaminika kuwa ni wa kale zaidi waliyompa jina la Zinjanthropus.

Ugunduzi huo uliofanyika saa nne asubuhi Julai 22, 1959 kipindi hicho kwenye eneo la Tanganyika ulikuwa wa vipande zaidi ya 100 ukasaidia katika kutambua asili ya watu wa awali duniani.

Kabla ya ugunduzi huo, wanasayansi na wanahistoria walikuwa wakiamini kuwa binadamu wa kale walitokea Uchina baada ya ugunduzi wa mafuvu ya kale baina ya 1923 na 1927 nchini humo ya Homo eractus, ama maarufu kama Peking Man.

Mafuvu hayo ya Uchina yalikuwa na umri wa takribani miaka 750,000.

Mafuvu ya Olduvai eneo ambalo kwa sasa lipo Tanzania wakati wa ugunduzi wake lilikuwa na umri wa takribani miaka milioni 1.8, na hakuna mabaki ya mtu wa kale zaidi ambayo mpaka sasa yamegunduliwa sehemu nyengine yeyote.

Toka wakati huo wanasayansi na wanahistoria wanaamini kuwa asili ya mwanadamu ni bara la Afrika na eneo la Olduvai kwa yakini.

Lakini utafiti huu mpya unaleta majibu ya kwamba, binadamu wa kale, aliishi miaka milioni 2 iliyopita, ikiaminika kwamba, alitokea pia kwenye eneo la Olduvai.

Nini kinafuata baada ya Utafiti huu mpya?

Pamoja na hatua hii mpya ya kubainika kwamba binadamu alikuwepo katika kipindi cha zaidi miaka milioni 2 iliyopita, na sio milioni 1.8 iliyogundulika awali na watafiti wengine, bado watafiti hawa wanabaki na maswali kadhaa.

Katika eneo la Olduvai waligundulika aina mbili za zamadamu wa kale walioishi hapo, Ancenstors (mababu zetu) na Zinjis, lakini nani kati ya hao aliyetengeneza zana zilizogundulika sasa? Hili ndilo swali kubwa linalowaumiza kichwa sasa watafiti.

Kwa mujibu wa Dkt Bushozi, mmoja wa watafiti hao, anasema swali linawafanya waone haja ya kuendelea kutafiti zaidi na zaidi, ili kupata majibu.