Kifo cha Rais Magufuli: Haiba, itikadi na usiri wa familia yake

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania
Magu

Wakati wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walipofanya Uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995 jina la John Pombe Joseph Magufuli lilikuwa miongoni mwa wagombea wa kiti cha Ubunge kupitia chama tawala CCM.

Kihistoria Magufuli amejiandikia rekodi binafsi ya kuwa mwanasiasa aliyeshiriki uchaguzi wa kwanza wa siasa za vyama vingi mwaka 1995 ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kurejeshwa mfumo huo mwaka 1992.

Ni uchaguzi uliong'arisha nyota yake ambapo alianza kupanda ngazi baada ya kuteuliwa na Hayati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa katika Baraza la Mawaziri kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Miaka 20 baadae, jina la John Pombe Joseph Magufuli, lilipaa katika anga za siasa na sasa alilazimika kuzunguka karibu nchi nzima kuomba kura za wananchi kuliko ilivyokuwa awali alipokuwa anagombea ubunge jimboni kwao Chato mkoani Geita, kwani safari hiyo alikuwa mgombea wa urais na alishinda kiti hicho.

Akiungwa mkono na mkewe Janeth Magufuli, maisha yao yalimulikwa zaidi na maelfu ya wananchi ndani na nje ya nchi.

Mama Janeth akiwa bega kwa bega kwenye shughuli za kisiasa ameshuhudia utawala wa mumewe akiwa rais kwa miaka mitano na siku 114.

Hapo ndipo akiwa baba wa familia na kiongozi haiba yake ilipanda thamani na kuvutia wengi kuliko chama alichotumia kuombea kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ule mvuto wake aliokuwa nao kupitia wizara mbalimbali alizokabidhiwa kuongoza bado haiba na familia yake vilibaki kuwa mambo yaliyofuatiliwa, huku watu wakitaka kujua Janeth Magufuli ni mwanamke wa namna gani?

  • Watoto wake wanafanya nini?
  • Je watoto wake wanajishughulisha na siasa kufuata nyendo za baba yao?
  • Je, Magufuli anafuata mrengo wa kulia au kushoto na mitazamo yake ikoje katika ulimwengu wa leo?

Usiri wa familia ya Magufuli

John Magufuli hadi anafariki dunia jambo moja ambalo linaweza kutafsiriwa kuwa ni utambulisho wa familia yake ni usiri na ambalo watanzania wengi watakuwa na wakati mgumu kubashiri mwelekeo wao nchini.

Watoto wa Magufuli ni Suzzan John Magufuli, Edna John Magufuli, Joseph John Magufuli, Jesca John Magufuli, Ruth John Magufuli, Jurgen John Magufuli,Jeremiah John Magufuli pamoja na marehemu Juliana John Magufuli.

Mwaka 2006 hadi 2007 nilipata kusoma na Edna John Magufuli katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal College of Tanzania jijini Dar es salaam nchini Tanzania.

Awali binti huyo hakujulikana kwa haraka kama ni mtoto wa mwanasiasa mkubwa nchini kutokana na mienendo na hulka zake.

Hata hivyo ilishindikana kujificha moja kwa moja baada ya kutokea mabadiliko yaliyomuondoa kutumia usafiri wa umma na wanafunzi wenzake, badala yake akawa na dereva maalumu wa kumleta chuoni na kumrejesha kwao.

Mabadiliko hayo yalitokana na kubainika kuwa mtoto wa mwanasiasa mkubwa nchini.

Alikuwa mwanamke asiyependa mzaha,mtiifu wa dini, mwenye msimamo mkali na aliyekuwa tayari kumkabili yeyote aliyejaribu kuvunja heshima yake ama utani ambao hakupenda.

Aliweza kufoka na kukaripia kwa lugha kali, mambo ambayo tumeyaona kwa baba yake katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano.

Aidha, ameonekana pia kuwakilisha hulka ya familia ya Magufuli kutojikweza na kujitapa kwa muda wote aliokuwapo masomoni.

Miaka michache baadaye naye alikwenda kusoma Shahada ya kwanza ya Mawasiliano ya Umma Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira jijini Dar es salaam, wakati ambao mwandishi wa makala haya akiwa Mwanafuzni wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam akisomea Sayansi ya Jamii na Ualimu. Kama ilivyokuwa awali, pia nilikutana naye kwenye harakati za kufanya mafunzo kwa vitendo katikati ya Jiji la Dar es salaam miaka kadhaa iliyopita.

Aidha, usiri unadhihirishwa zaidi pale Magufuli alipoeleza tukio la watoto wake watatu kufunga ndoa pasipo umma kufahamu, huku mwenyewe akijigamba kuwa hapakuwa na ulazima wa kuweka hadharani jambo hilo la kifamilia. Ndoa mojawapo ni ya Edna ambapo wanafunzi wenzake wa zamani tuliarifiwa juu ya harusi yake.

Mwingine Ruth John Magufuli ambaye ni miongoni mwa viongozi katika Mkoa wa Morogoro akiwa katika nafasi ya Katibu tawala. Jesca Magufuli alisoma shahada ya uzamili ya Utawala wa umma katika Chuo Kikuu Dodoma kilichopo jijini Dodoma katikati mwa Tanzania. Lakini haijafahamika undani wa maisha ya watoto wengine.

Je watoto wa Magufuli ni wanasiasa?

Familia ya Magufuli haina ukubwa katika siasa kama alivyokuwa baba yao.

Hawajulikani, hawatabiriki wala hawaonekani kwenye anga za kisiasa kuchukua mkondo au kuwa maarufu kama walivyokuwa watoto wa wanasiasa wengine January Makamba, Ridhiwani Kikwete, Halima Bulembo na Miraji Kikwete kwa kuwataja wachache.

Kiongozi mmoja mstaafu katika serikali ya awamu ya nne amemwambia mwandishi wa makala haya, "Magufuli familia yake ina usiri sana, ana watoto wakubwa ila sio wanasiasa. Ni kama hawapo kwa sasa labda miaka ijayo. Uchaguzi uliopita alikuja yule mtoto wa dada yake Furaha Dominic Jacob alitia nia ya ubunge CCM pale Kawe, japo alishinda ila hakupita mwenyekiti alimkata. Sasa yule ni mtoto wa dada yake, ila wa kwake hawapo kisiasa, wana mambo yao mengine tofauti."

Edna Magufuli kitaaluma ni mwandishi wa habari na hakuwahi kuonesha dalili za kuvutiwa na kuwa atakuja kuwa mahiri katika siasa, na alifunga ndoa miaka michache iliyopita wakati baba yake akiwa Rais wa Tanzania.

"Hao ni watu wazima, wapo na wanaendesha maisha yao nje ya siasa, lakini hawajulikani hadharani kama watoto wa vigogo wengine, na ni vyema kuwa wasiri, wamelelewa hivyo," mmoja wa wanahabari na mhariri mwandamizi wa masuala ya siasa amemwambia mwandishi wa makala haya.

Magufuli aliamini katika itikadi gani?

Alikuwa mserikali, yaani mwanasiasa aliyeamini matendo ya serikali zaidi kuliko nje ya serikali. Mserikali ni mtu anayeamini kuwa uendeshaji wa mifumo ya uchumi na huduma nyinginezo hutakiwa kutolewa na serikali huku sekta binafsi ikipigwa kumbo na kuonekana kama vile haina msaada kwa taifa.

Kwa vile alikuwa mtoto wa mkulima aliyejua umasikini ni nini na ukoje, ndiyo msingi wa itikadi yake ya ujamaa.

Magufuli amekulia katika mfumo wa itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea chini ya rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere(1961-1984) na kupata elimu na kupevuka katika utawala wa Ali Hassan Mwinyi ambaye alianza kuruhusu sekta binafsi kupitia Azimio la Zanzibar ambalo kihistoria linatajwa kufuta Azimio la Arusha lililoanzishwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1967.

Kimsingi alikuwa mjamaa kivitendo na maneno ambaye alionekana kuamini serikali inaweza kutoa huduma pasi na mchango wa sekta binafsi.

Itikadi hiyo inathibitishwa kwa matamshi yake ya mara kwa mara ya neno 'Mabeberu' akimaanisha nchi za Magharibi, huku akisifia zile za Asia ikiongozwa na China. Pia alichukua hatua kali za kupunguza taasisi za serikali kutumia kumbi za mikutano za sekta binafsi.

Janeth wa tatu na rekodi ya Shule ya Mbuyuni

Mama Janeth Magufuli ana rekodi ya aina yake. Yeye ndiye 'First Lady' wa tatu kuitwa Janeth katika nchi Afrika mashariki akitanguliwa na Janet au Janeth Museveni (Mke wa rais wa Uganda Yoweri Museveni) na Jeaneth au Janeth Kagame (Mke wa rais wa Rwanda Paul Kagame).

Mke huyo wa rais Magufuli alipokea kijiti cha kuwa 'First Lady' kutoka kwa Salma Kikwete.

Kitaaluma ni mwalimu ambaye alifundisha Shule ya Msingi Mbuyuni iliyopo Oysterbay jijini Dar es salaam katika masomo ya Jiografia,Tehama na Historia.

Mama Janeth Magufuli amesoma shule ya msingi Mbuyuni kisha akawa mwalimu shuleni hapo kwa miaka 17.

Tarehe 18 Februari mwaka 2016 aliwaaga wanafunzi wa shule hiyo ili kuanza majukumu ya kuwa mke wa rais.

Shule hiyo ina rekodi ya kipekee nchini Tanzania kwa kuwatoa wake wawili wa marais; mke wa rais mstaafu Jakaya Kikwete na John Magufuli.

Salma Kikwete naye alifundisha katika shule hiyo wakiwa chini ya Mwalimu Mkuu Dorothy Malecela.

Janeth Magufuli ana umri wa miaka 61 na hakuonekana hadharani kwa siku nyingi.

Ni mwanamke mkimya, haiba yake haifanani na watangulizi wake Salma Kikwete, Anna Mkapa wala Sitti Mwinyi. Kwa mbali Mama Janeth amefuata nyayo za Mama Maria Nyerere ambaye hakufanya harakati zozote za siasa wakati mumewe Mwalimu Nyerere akiwa madarakani.

Salma Kikwete amekuwa akijihusisha harakati za maendeleo ya watoto wa kike nchini Tanzania kama ilivyokuwa kwa Mama Anna Mkapa aliyejihusisha na shughuli mbalimbali zilizogusa siasa kwa namna moja au nyingine.

Salma Kikwete aliingia kwenye hekaheka za kisiasa ndani ya CCM akiwa miongoni wa wajumbe mkoani Lindi na baadaye aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mbunge kisha muda wake ulipomalizika aligombea moja kwa moja jimboni na kushinda katika uchaguzi mkuu 2020.

Mama Janeth hana dalili za kuingia kwenye siasa hata kwa kipindi ambacho mumewe alikuwa mbunge,waziri hadi Amiri Jeshi Mkuu.

Aidha, mke wa rais ni cheo kisicho rasmi kinachoshikiliwa na mke wa Rais wa Tanzania, tangu zamani wake wa marais huanza kwa kuitwa mama. Miaka ya karibuni kulikuwa na mijadala mingi kuhusu suala la kuongeza umaarufu wa wake za marais wa Tanzania. Kumekuwa na mapendekezo pia na kupelekwa bungni kwa nia ya kurasimisha Ofisi ya Mke wa Rais.

Magufuli na Nchi za Magharibi

Hadi anafariki dunia Rais Magufuli hakuwahi kufanya ziara yoyote katika nchi za bara la Ulaya, Asia na Amerika ya kusini na kaskazini. Imezoelekea viongozi wa Afrika kutembelea nchi za Marekani, Uingereza, China,India,Ufaransa,Ujerumani na kadhalika, lakini Magufuli hakufanya ziara zozote katika nci hizo.

Haijaelezwa bayana sababu za kutotembelea, lakini utawala wa Magufuli ulionesha kuwa hakuzipenda wala kutamani kuzitembelea na ndiyo maana kila mara alitoa matamshi yenye ukasisi dhidi ya nchi za Magharibi.

Akiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika amezitembelea nchi za Malawi, Zimbabwe, Rwanda, Kenya,Uganda,Afrika kusini.