Kifo cha Magufuli: 'Mimi ndiye Rais' - Je, rais Samia Hassan Suluhu anatuma ujumbe gani kwa Watanzania?

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania
Samia Suluhu Hassan

Chanzo cha picha, Mkurugenzi wa mawasiliano afisi ya rais Tanzania

Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameanza kutoa majibu ya maswali magumu ambayo yanawatawala wananchi wake tangu alipoapishwa kushika wadhifu huo kuchukua nafasi ya Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 Machi mwaka huu wa 2021 katika Hospitali ya Mzena Dar es salaam na kuacha simanzi kubwa miongoni wa wananchi wa Taifa hilo la Afrika mashariki.

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa baada ya kutoa hotuba mbili, ya kuapishwa kwake Ikulu jijini Dar es salaam tarehe 19 Machi na ile ya kumuaga Rais Magufuli jijini Dodoma tarehe 22 Machi mwaka huu zimeonesha ujumbe wa uimara wake, matumaini na mwelekeo mpya katika kustawishi Taifa hilo.

Hotuba zote mbili zimebeba ujumbe mzito kwenda kwa wanasiasa wa ndani ya chama tawala CCM na upinzani, viongozi wastaafu wakiwemo marais, uhusiano wa nchi hiyo na jirani zake, uhusiano na viongozi na nchi za kimataifa, msimamo thabiti wa Tanzania, kufuata nyayo za mtangulizi wake katika maendeleo na kusisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi na viongozi wao.

Kabla ya hotuba hizo Watanzania walikuwa wakijiuliza maswali kadhaa yakiwemo rais Samia Suluhu ataanza na nini katika uongozi wake? Ni mambo gani ambayo yatakuwa kipaumbele katika uongozi wake? Uongozi wa rais mpya utakuwa wa namna gani?

Je, ataweza kuendeleza mambo yaliyoanzishwa na mtangulizi wake? Rais mpya ataleta matumaini au wasiwasi kwa Watanzania?

Na zaidi hotuba zake kwa sasa zinatuma ujumbe gani kwa wananchi wake,viongozi na Jumuiya ya Kimataifa?

Diplomasia

Akiwa amepokea pongezi kutoka kwa viongozi wa nchi mbalimbali barani Afrika, pamoja na wengine kutoka bara la Asia, Amerika kusini na kaskazini, rais Samia Suluhu ametuma ujumbe kwao kuwa serikali yake itasimamia kwa umakini suala la uhusiano nao na kuwa chachu ya kujenga jamii bora baina ya mataifa hayo.

"Kwa jirani zetu na marafiki zetu niwahakikishie tutaulipa wema mliotuonesha kwa kuimarisha na kushamirisha uhusiano wetu nanyi," alisema Rais Suluhu katika hotuba yake ya kumuaga Magufuli mkoani Dodoma.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Tanzania

Maelezo ya picha,

Rais Samia Suluhu akilikagua gwaride la kijeshi

Huu ni ujumbe muhimu na wenye kwa mataifa yote yanayoizunguka Tanzania yakiwemo Burundi,Malawi,Msumbiji,Comoro,Rwanda,Uganda, Kenya pamoja na wale waliohudhuria kuagwa Rais Magufuli kutoka nchi za Zimbabwe, Namibia, Afrika kusini, Zambia, Botswana na Angola kuwa rais mpya anatarajia kujenga uhusiano mwema kati yake na majirani zake. Pia ujumbe huo unaleta majibu ya swali la mustakabali wa Kidiplomasia wa Tanzania na Jumuiya ya kimataifa.

Kwamba Rais amethibitisha kuwa yupo tayari kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwaita "Marafiki zetu" ikiwa na maana ya kuwakaribisha katika mashauriano ya Kidiplomasia na kuwahakikishia ushirikiano madhubuti.

Katika kipindi cha Rais Magufuli ilishuhudiwa uhusiano kati ya Tanzania na Kenya ukiingia dosari mara kwa mara kutokana na nchi hizo 'kutopikika' chungu kimoja. Matukio kadhaa yaliyotokea kati ya Tanzania na Kenya yanathibitisha hali ilivyokuwa, mfano serikali ya Kenya kuzuia na kutangaza mahindi kutoka Tanzania yana sumu.

Pia serikali ya Tanzania kuchoma moto vifaranga kutoka Kenya pamoja na kuzuia malori ya mahindi yaliyotoka nchini Zambia. Rais Samia ametoa ujumbe kwao kuimarisha ushirikiano mwema na majirani ikiwa na maana kuondoa 'wingu jeusi' la uhusiano baina ya nchi yake na Kenya.

Nyayo za Magufuli

Miongoni mwa wasiwasi uliotawala ni mwelekeo wa kiongozi huyo mpya katika kutekeleza majukumu,ahadi na mipango iliyokuwa ikisimamiwa na mtangulizi wake. Hata hivyo kiongozi huyo ametuma ujumbe wa kuwaondoa wasiwasi raia wake.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais

Maelezo ya picha,

Rais Samia Suluhu Hassan na mtangulizi wake John Pombe Magufuli

Rais huyo katika hotuba yake ya Dodoma alisema, "Magufuli amemaliza kazi iliyomleta duniani kazi hiyo ilikuwa ni kutuonesha namna kazi zinavyofanywa, namna ya kutekeleza na kuchukua maamuzi magumu kwa masilahi ya Taifa. Nasi hatuna budi kufuata njia hii aliyotuachia,"

Serikali ya Tanzania imekuwa kwenye mikakati ya kuboresha huduma za jamii, ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali,miradi ya maendeleo pamoja na sera zake za kiuchumi, mambo ambayo rais mpya amesisitiza kufuata nyayo za mtangulizi wake kwa masilahi ya taifa hilo.

Ulinzi na Usalama, Umoja na mshikamano

"Nitumie fursa kwa mara nyingine nisisitize kuwa hakuna jambo ambalo litakaloharibika. Nchi yetu iko katika mikono salama mimi na mwenzangu Dk Hussein Mwinyi (Rais wa Zanzibar) tutaendeleza alipoishia na tutafika pale alipopatamani,"

Matamshi hayo ya Rais Samia yanafanana na yale aliyoyasema rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete alipohojiwa na vyombo vya habari hivi karibuni kuelezea kifo cha Rais Magufuli, ambapo alisema Tanzania ipo kwenye mikono salama na Rais mpya anafahamu malengo na mipango ya miaka mitano na maelekezo ya nini kinachopaswa kufanyika kuikamilisha.

Naye Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu ameonesha kukubaliana na hoja za Rais mpya ambapo amemwambia mwandishi wa makala haya, "Rais Samia Suluhu alikuwa anatoa uhakika kwa wale wenye wasiwasi kuwa yale mazuri yaliyofanyika enzi za Rais Magufuli hayataendelezwa.

Lakini ukichambua hotuba ya Dodoma sambamba na ile ya siku ya kuapishwa Ikulu, ni dhahiri kuwa kuna masuala ya enzi ya Rais Magufuli yatabadilishwa. Hiyo ndiyo tafsiri yangu ya wito wa Mama Samia kuwa tusahau yaliyopita,"

"Mimi ndiye Rais"

Kiongozi huyo ameonesha kuwa na msimamo thabiti baada ya kutoa matamshi yanayotoa ujumbe kuwa hatakuwa tayari kuyumbishwa na kuvumilia mtu yeyote itakayomkwamisha au namna yoyote ile ya kujaribu kuvuruga urais wake.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

"Rais Samia Suluhu alikuwa anatoa uhakika kwa wale wenye wasiwasi kuwa yale mazuri yaliyofanyika enzi za Rais Magufuli hayataendelezwa

Msimamo thabiti wa kiongozi huyo unapatikana katika hotuba ya kumuaga Rais Magufuli jijini Dodoma ambapo alisema, "Wale ambao wana mashaka mwanamke huyo ataweza kuwa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania,nataka niwaambie aliyesimama hapa ni Rais. Nataka nirudie kwamba aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"

Msimamo huo unakumbusha ule wa mtangulizi wake ambaye amewahi kutoa matamshi thabiti akiwa katika moja ya mikutano yake ya hadhara mkoani Singida mwaka 2017 ambapo alisema yeye ndiye rais wa Tanzania, hayumbishwi wala kutishwa kwa jambo lolote.

Aidha Magufuli amewahi kutoa kauli kuwa hakwenda Ikulu kutafuta wachumba bali kufanya kazi na 'yeye ndiye rais' anayesimamia ustawi wa nchi. Mfanano wa kauli mbili hizo za Samia Suluhu na John Magufuli zinaonesha ni viongozi wenye misimamo na wametuma ujumbe kwa wasaidizi wao, washindani wa kisiasa pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa wanaongozwa na watu wenye uelewa na kutambua madhumuni ya Taifa na matamanio ya wananchi. Hivyo ili kutimiza majukumu yake lazima atoe ujumbe kuwa ni mwenye msimamo usiotetereka.

Busara za Wazee

Rais Samia Suluhu kama walivyo viongozi wengine amedhihirisha hekima zake baada ya kuwaambia viongozi wastaafu kuwa anahitaji mchango wao katika uongozi wake.

Samia alisema, "Niwaombe wazee wangu wa pande zote za Muungano, lakini pia viongozi wengine wastaafu kwamba mimi ni kijana wenu pia kama alivyokuwa Rais Magufuli. Pia nami nipo tayari kushirikiana nanyi bega kwa bega katika kujenga Tanzania aliyotamani mpendwa wetu na tunayoitamani sisi wote,"

Rais huyu anawasilisha ujumbe kuwa uongozi wake unahusisha pia busara za watangulizi wake,viongozi wastaafu wa chama na serikali kutoka pande zote za Tanzania. Ni hatua kubwa kiuongozi.