Rais Museveni na mkewe Janet wapata chanjo ya Corona

Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mkewe mama Janet Museveni corona

Chanzo cha picha, Museveni/Twitter

Maelezo ya picha,

Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mkewe mama Janet Museveni wakipata chanjo yao ya corona

Hatimaye Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mkewe mama Janet Museveni wamepata chanjo yao ya Covid-19.

Mwanahabari wa Rais Yoweri Museveni Don Wanyama, amefahamisha katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwamba Rais Museveni amepata chanjo hiyo aina AstraZeneca leo jumamosi katika Ikulu ya Nakasero mjini Kampala.

Taarifa hizo pia zimeonekana kwenye akaunti ya Twitter ya Rais Museveni.

Rais Museveni amehamasisha raia wa Uganda ambao wapo kwenye kundi la wanaoweza kupata chanjo, kufanya hivyo katika mpango huo ambao upo kwenye awamu yake ya pili.

Uganda ilizindua chanjo ya Covid-19 tarehe 10 mwezi huu wa Machi, katika Hospitali kuu ya taifa ya Mulago mjini Kampala, baada ya kupokea shehena ya dozi 864 toka kwa mpango wa Covax na dozi laki moja kutoka serikali ya India na kuhitimisha dozi 964,000.

Awamu ya kwanza ilijumuisha wahudumu wa afya, maafisa wa usalama, walimu na wanahabari.

Awali, Rais Museveni katika hotuba yake kwa taifa, alisema kuwa bado anatafakari ni chanjo gani ambayo atachanjwa na hatimaye leo amefanya maamuzi na kupata chanjo hiyo.

Katika hotuba yake wakati huo, Rais Museveni alisema kuwa ''bado hajapata chanjo kwa kuwa yuko makini na ana ulinzi wa kutosha".

Hata hivyo, kuliwahi kutokea taarifa mwezi uliopita kuwa rais na watu wake wa karibu walikuwa wanapokea chanjo nyingine kwa siri kabla ya taifa hilo kupokea chanjo rasmi, taarifa ambazo Waziri huyo Jane Aceng, alikanusha.

Waziri wa Afya alitoa ufafanuzi baada ya gazeti la nchini humo la Daily Monitor na gazeti la Marekani la jarida la Wall Street kuandika habari hizo za uongo.

Pia ikumbukwe kuwa Waziri wa afya wa Uganda Jane Aceng, ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kupata chanjo hiyo na kushauri watu kwenda kuchanjwa kwasababu chanjo haina madhara yoyote.

Hata hivyo, kulitokea tena sintofahamu na Waziri huyo wa Afya wa Uganda Jane Aceng akaweka mtandaoni video inayomuonesha akipewa chanjo ya corona baada ya madai kuibuka kwamba hakuchanjwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Waziri wa Afya wa Uganda Jane Ruth Aceng akipata chanjo ya corona

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walianza kusambaza video inayomuonesha waziri akiinua mkono kana kwamba anadungwa sindano, lakini sindano hiyo haikuonekana kuiingiia mwilini.

Hata hivyo, baadaye ilielezwa kwamba angerudia tena kupokea chanjo hiyo kwasababu baadhi ya waandishi walisema hawakufanikiwa kupiga picha ya chanjo yake asili.

Baadaye, Dkt Aceng aliweka kwenye Twitter video inayoonesha wakati sindano ikiingia kwenye mkono wake.

Na kutoa wito kwa watu "kuacha kueneza taarifa ghushi".