Tanzania na Uganda wasaini mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta

Museveni

Chanzo cha picha, Museveni-Twitter

Uganda na Tanzania wamesaini mikataba mitatu yenye nia ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ya Uganda, wakati wa ziara ya kwanza ya nje ya nchi ya Rais Samia Suluhu.

Serikali hizo zimekubaliana katika masuala ya hisa, usafirishaji na ushuru katika hatua za awali za mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki.

Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi wa jumla ya Kilometa 1,443 kutoka Magharibi mwa Uganda mpaka kwenye bandari ya bahari ya Hindi, Tanga.

Chanzo cha picha, TWITTER-Museveni

Ujenzi huo utagharimu dola za Marekani bilioni 3.55, na unatarajiwa kuwa mradi wenye bomba refu zaidi la mafuta duniani.

Maafikiano ya mwisho ya mradi huo - na wafadhili wa ujenzi huu- utaafikiwa na mataifa haya mawili na makampuni ya mafuta kabla ya ujenzi huo haujaanza.

Mataifa haya mawili yanatarajia kukuza uchumi na kuzalisha ajira zipatazo 10, 000 wakati wa ujenzi wa bomba hilo na uendeshaji wa mradi huo.

Ingawa mradi huo ulikosolewa vikali na wataalamu wa mazingira, ambao wanaofia athari katika ziwa Victoria na mbuga ya wanyama ya Serengeti.

Uganda inakadiriwa kutoa mapipa yake ya kwanza ya wastani wa bilioni 1. 4 ya mafuta yanayofaa kibiashara mnamo 2025.

Chanzo cha picha, Ubalozi wa Uganda-Tanzania

Rais Samia pamoja na mwenyeji wake Rais Museveni, amehudhuria hafla na utiaji saini mkataba kati ya Serikali ya Uganda na Kampuni ya Mafuta Ghafi ya Afrika Mashariki (EACOP) juu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda kwenda Tanga nchini Tanzania.

Rais Samia amealikwa Ikulu ya Entebbe na mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni na kuanza kukaguwa gwaride la heshima liloandaliwa kwa ajili yake.

Baada ya kukaguwa gwaride Museveni na mgeni wake walifanya mkutano wa faragha pamoja na kampuni ya Total baada ya hapo watasaini utekelezaji wa ujenzi wa bomba la mafuta la mradi mkubwa wa dhamani ya dolla bilioni 15.

Hii ni safari ya kwanza kwa rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania tangu kuchukua madaraka baada ya kifo cha Hayati Dkt John Pombe Magufuli.

Mwaka 2020, aliyekuwa rais wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli na Rais Yoweri Museveni walisaini makubaliano ya jenzi wa bomba hilo unaogharimu dola za Marekani bilioni 3.5.

Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Hoima -Tanga wenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania utagharimu dola za Marekani bilioni 3.55, unatarajiwa kusafirisha mapipa laki 2 ya mafuta kwa siku na wakati wa ujenzi unatarajiwa kuzalisha ajira kati ya 6,000 na 10,000.

Mradi huo utakao gharimu dola za kimarekani bilioni 3 unajengwa kwa ushirikaino wa serikali za nchi hizo mbili na washirika na unatariji kutoa ajira zaidi ya 30,000.

Rais Magufuli alisema hatua ambayo Tanzania na Uganda zimefikia katika mradi wa bomba la mafuta ni matokeo ya urafiki na udugu wa kihistoria ulioko kati ya nchi hizi mbili.

Rais Magufuli alisema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Uganda, Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika nzima, na kwamba pamoja na faida zilizoainishwa kwa bomba hilo kupitia Tanzania ni uwepo wa amani, uzoefu wa Tanzania katika uendeshaji wa miradi ya mabomba ya mafuta na gesi, jiografia nzuri ya usafirishaji mafuta, ardhi na ubora wa bandari ya Tanga, Tanzania inaupokea mradi huo kwa heshima kubwa na ni kumbukumbuku kubwa ya Rais Museveni na Serikali yake.

"Huu ni mradi mkubwa sana, najua Uganda mmepata mapipa Bilioni 6.5 ya mafuta huko Hoima na pengine mtapata mengine na sisi pia tunatarajia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, haya yote tutayapitisha kwenye bomba hili hili.

Kwa upande wake rais Museveni amempongeza rais Magufuli na Serikali yake kwa kutia msukumo mkubwa kufanikisha mradi huu na amesema mradi huu utazinufaisha nchi za Afrika Mashariki yakiwemo mashirika ya ndege ambayo yatapata mafuta kwa gharama nafuu na hivyo kukua zaidi kibiashara.

Rais Museveni aliuelezea mradi huo kama moja ya matokeo ya ushirikiano na ametoa wito kwa viongozi hasa vijana kuendeleza misingi ya umoja na ushirikiano kati ya nchi zao ili kujipatia manufaa ya kiuchumi.

Chanzo cha picha, Museveni-Twitter

Maelezo ya picha,

Wiki iliyopita baadhi ya viongozi wa Tanzania walikutana na Rais Museveni kujadili mradi huo wa bomba la mafuta