Olimpiki Tokyo 2021: Ndoto ya miaka 40 ya Tanzania kupata ushindi itatimia?

Tanzania

Chanzo cha picha, Olympics

Ni miaka 41 imepita tangu Tanzania ilipotwaa kwa mara ya kwanza na ya mwisho medali katika michezo ya Olimpiki ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne ikishirikisha wanamichezo kutoka nchi zaidi ya 200.

Tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo mwaka 1964, Tanzania imetwaa medali mbili tu ambazo zote ilizipata katika michezo ya mashindano hayo iliyofanyika mwaka 1980 huko Moscow, Urusi.

Medali hizo zote zilikuwa za shaba ambapo moja ilitwaliwa na mwanariadha Suleiman Nyambui aliyeshika nafasi ya pili katika mbio za Mita 5000 na nyingine ikichukuliwa na Filbert Bayi katika mbio za Mita 3000.

Mara baada ya hapo, Tanzania imekuwa ikipeleka wanamichezo wake katika mashindano hayo lakini wamekuwa wakishindwa kurudi na medali.

Mwaka huu mashindano ya Olimpiki yanaanza rasmi hii leo huko Japani na Tanzania itawakilishwa na wanamichezo watatu tu ambao wote ni wanariadha wa mbio ndefu, Gabriel Geay na Alphonce Simbu upande wa wanaume huku kwa upande wa wanawake itawakilishwa na Failuna Matanga.

Serikali, uongozi zanyooshewa kidole

Chanzo cha picha, Filbert Bay/Getty image

Maelezo ya picha,

Filbert Bayi

Wadau mbalimbali wa michezo haswa riadha ambao umekuwa ukipeleka washiriki katika michezo hiyo wanafichua kuwa sapoti ndogo ya baadhi ya mamlaka za serikali na udhaifu wa uongozi wa vyama vya michezo hasa Shirikisho la Riadha Tanzania ni miongoni mwa sababu ambazo zimepelekea Tanzania kutovuna medali katika mashindano hayo kwa muda mrefu.

Nyambui ambaye alishinda medali ya shaba katika michezo hiyo mwaka 1980 alisema kuwa kama nchi ingekuwa inatoa ushirikiano kwa vyama vya michezo na kuvipa msaada wa kifedha, Tanzania ingekuwa inavuna medali nyingi katika mashindano hayo

"Kama nchi haina mfumo mzuri wa kuandaa wanamichezo kwa ajili ya kushiriki michezo hiyo na badala yake jukumu hilo limeachwa kwa vyama vya michezo ambavyo vingi havina uwezo wa kifedha kumudu gharama za kuwaandaa wanamichezo.

Hii ni tofauti na mataifa mengine ambayo vyama vya michezo vinapewa sapoti kubwa ya kifedha na wataalam katika kuwaandaa wanamichezo wao na ndio maana zinafanikiwa," alisema Nyambui.

Katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Wilhelm Gidabuday alisema idadi ndogo ya washiriki na udhaifu wa uongozi wa shirikisho hilo ndio umekuwa ukiiangusha Tanzania.

"Kwenye chama cha riadha ushindi unaanzia kwenye kamati ya ufundi na baadaye katika kamati ya utendaji. Medali inapatikanaje kama vigezo vya kiufundi havijazingatiwa? Hili tumekuwa tukilifikisha katika mamlaka za kiserikali na zimekuwa zikipuuzia.

Watu wamekuwa wakijali maslahi yao. Mimi nilijiuliza lakini hakuna kibaya nilichokifanya. Mfumo uliopo unafanya baadhi ya watu waonekane kuwa wabaya. Viongozi ndio haohao miaka yote," alisema Gidabuday.

Ikumbukwe kwamba malengo ya awali yalikuwa ni Tanzania kuwakilishwa na washiriki wa michezo angalau minne tofauti lakini kutokana na ukata imelazimika kuwakilishwa na wanamichezo watatu tu.

Matumaini finyu Japan

Kitendo cha kuwakilishwa na wanamichezo watatu tu katika mashindano ya Olimpiki mwaka huu hapana shaka kinaiweka Tanzania katika wakati mgumu wa kuvuna medali yoyote katika mashindano hayo.

Idadi kubwa ya wawakilishi katika mashindano hayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuzifanya nchi mbalimbali kupata idadi kubwa ya medali kulinganisha na Tanzania ambayo imekuwa ikitoka patupu.

Kwa mfano, taifa la Marekani ambalo mara kwa mara hufanya vizuri katika michezo hiyo, mwaka huu litawakilishwa na wanamichezo 613 wakifuatiwa na wenyeji Japan ambao watakuwa na wanamichezo 552 na Uingereza inashika nafasi ya tatu kwa kuwakilishwa na idadi kubwa ya wanamichezo ambapo itakuwa na watu 376

Mdau wa mchezo wa riadha, Kulwa Bundala alisema idadi ndogo ya wanamichezo inaiweka nchi katika uwezekano finyu wa kuvuna medali katika mashindano hayo

"Tunawakilishwa na namba ndogo sana ya wanamichezo jambo ambalo linanipa mashaka kama tunaweza kupata medali katika hayo mashindano kwa sababu ikiwa hao watatu watafanya vibaya maana yake hakutokuwa na michezo mingine ya kuweza kunusuru.

Lakini katika michezo hatupaswi kukata tamaa kupitiliza na kama wanariadha wetu watajituma inawezekana wakatuletea heshima," alisema Bundala.

Kwa upande wa Nyambui alisema haoni uwezekano wa Tanzania kupata medali katika michezo hiyo.

"Mimi nadhani kwa sasa na hata mashindano ya Olimpiki mwaka 2024 tumeshachelewa na tunatakiwa tujipange kwa ajili ya yale ya mwaka 2028.

Ni vigumu kushindana na mataifa ambayo wachezaji wao wameandaliwa vizuri na wanaenda kwa idadi kubwa mashindanoni. Siku ambayo kama taifa tutakaa chini na kuamua kwamba imetosha tunataka medali, naamini ndio tutapafanya vyema," alisema Nyambui.

Hata hivyo, kocha wa riadha, Alfredo Shahanga alisema ana matumaini ya kufanya vizuri licha ya uchache wa wanamichezo.

"Kama tukipata walau medali mbili au moja tutakuwa tumepata ushindi mkubwa sana. Timu yetu ya wanaume ya Marathon ambayo ina Alphonce Simbu ambaye ni mshindi wa tatu wa Mashindano ya Dunia ya London 2019 na Gabriel Geay ambaye atakuwa anakimbia Marathon yake ya pili baada ya kuvunja rekodi ya taifa kwa kukimbia kwa saa mbili na dakika nne, wachezaji hao wote wawili ni wazuri na wako katika ngazi ya juu ya kimashindano ambayo katika ngazi hiyo lolote linaweza kutokea.

Niseme kwamba timu ni ndogo lakini timu kuwa hivyo isiondoe matumaini ya kurudi na medali kwa sababu wachezaji waliopo wanakimbia katika muda mzuri," alisema Shahanga.

Mwanariadha Fabian Joseph alisema ana matumaini wenzake watafanya vyema katika hayo mashindano.

"Matumaini ninayo ingawa wenzetu wachache watatuwakilisha katika hayo mashindano kwa sababu wamekuwa na maandalizi mazuri kabla ya kuelekea Japan," alisema Joseph

Tiba yasakwa

Uwekezaji mzuri katika sekta ya michezo kwa watu binafsi na serikali, uongozi bora katika vyama vya michezo na maandalizi mazuri kwa wanamichezo vimeonekana kama suluhisho la kudumu la changamoto hiyo ya Tanzania kufanya vyema katika michezo hiyo.

Ni kupitia uwekezaji huo wa kifedha na kisera, nchi itaweza kuwaandaa wanamichezo mahiri kuanzia katika umri mdogo ambao wataandaliwa vyema kuweza kufanya vyema katika mashindano hayo na mengine ya kimataifa.

Lakini pia sapoti ya serikali kwa kutoa sapoti ya kifedha kwa vyama vya michezo ili viweze kupeleka idadi kubwa ya wanamichezo katika mashindano hayo na mengineyo.

Mkurugenzi wa maendeleo ya Michezo Tanzania, Yusuph Singo alisema serikali ya michezo imeweka mikakati ya kuhakikisha nchi inafanya vyema katika mashindano ya Olimpiki na mengine ambayo itapeleka wanamichezo wake.

"Kama mnavyoona tumeamua kuwekeza katika mashindano ya michezo kwa shule za msingi, sekondari na vyuo lakini pia tumeweka mkazo katika kuwaandaa wataalam wa kutosha kupitia chuo chetu cha michezo cha Malya.

Lakini pia tumekuwa na ushirikiano na baadhi ya mataifa ambayo yako tayari katika kutusaidia kujenga vituo vya michezo hivyo naamini tutapiga hatua kubwa," alisema Singo.

Kwa upande wa Shahanga alisema iko haja kwa wanamichezo kupata maandalizi mazuri kwa sapoti ya serikali.

"Wanamichezo kwa mfano riadha wanatakiwa waandaliwe mapema na wapate fursa ya kushiriki mashindano mengi ya kufuzu. Ukiwa na wanariadha 25 kwa mfano na wakawekwa katika kambi ya maandalizi kwa miaka angalau miwili, ni rahisi kupata medali katika mashindano kama haya ya Olimpiki," alisema Shahanga.