Virusi vya Corona:Je chanjo milioni 241 ziko hatarini kupotea wakati hata nusu ya watu duniani hawajapata ?

Queue in Delhi for vaccine

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais Biden amewataka viongozi wote duniani kuahidi kuchanja 70% ya idadi ya watu ulimwenguni ifikapo Septemba mwaka ujao. Lakini utafiti unaonesha nchi tajiri bado zinashikilia chanjo nyingi, ambazo nyingi zinaweza kuisha muda wake hivi karibuni.

Wakati akipanda ndege kwenda Iran msimu huu wa joto, Bahar alifurahi kumwona baba yake kwa mara ya kwanza katika miaka minne.

Hakuwa na wazo la jinsi virusi vya corona vilivyoathiri nchi - na familia yake - katika wimbi la pili la mlipuko wa virusi hivyo.

Kwanza alikuwa rafiki wa familia, ambaye alikuwa akiandaa harusi ya mtoto wake akaugua na kufariki muda mfupi baadaye.

Halafu akafuata mjomba wa baba yake, halafu shangazi yake naye akafariki. Bahar alikuwa na wasiwasi sana juu ya bibi yake ambaye alikuwa amepata dozi moja tu ya chanjo na alikuwa bado akingojea ya pili.

Bahar ana miaka 20 na anaishi Marekani ambako alipata chanjo mwezi Aprili.

Ingawa alijua kuwa ana kinga kwa kiasi fulani, alitumia siku za mwisho za likizo yake akiwa nyumbani kwa baba yake akiwa na wasiwasi juu ya nani atafuata kushambuliwa na virusi. Watu wachache katika familia yake wamepewa chanjo katika nchi ambazo usambazaji wa chanjo ni mdogo.

Mara tu baada ya kurudi Marekani, aliambiwa kuwa baba yake alikuwa mgonjwa. Akiwa mbali na kudhoofika kwa hofu.

"Nilijihisi kama nina hatia ," anasema. "Nilidhani Iran ilikuwa salama kabisa, nilijihisi kuwa mzima kabisa kwa sababu nilikuwa nimepata dozi mbili za chanjo ya Pfizer." Baba yake alipona lakini ndugu zake wengi wazee hawakupona. "Nilijihisi kuwa na hatia sana kujua hivyo."

Chanzo cha picha, Submitted

Ukosefu huu wa usawa wa usambazaji wa chanjo hufanya takwimu kamili kukosekana. Zaidi ya nusu ya dunia bado haijapokea hata dozi moja ya chanjo ya corona.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, 75% ya chanjo ya corona zimekwenda kwa nchi 10.

Kitengo cha Upelelezi cha uchumi kimehesabu kuwa nusu ya chanjo zote zilizotengenezwa hadi sasa zimekwenda kwa 15% ya idadi ya watu duniani, nchi tajiri zikiwa zimepata chanjo nyingi mara 100 zaidi ya zile nchi maskini.

Mnamo Juni, wanachama wa G7 - Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani - waliahidi kutoa dozi bilioni moja kwa nchi maskini kwa mwaka ujao.

"Nilitabasamu nilipoona hivyo," anasema Agathe Demarais, mwandishi wa ripoti ya hivi karibuni juu ya usambazaji wa chanjo ulimwenguni katika Kitengo cha Ujasusi wa Uchumi na mwanadiplomasia wa zamani. "Nilikuwa sina matumaini au jambo hili haliwezi kutokea."

Uingereza iliahidi dozi milioni 100, hadi sasa imetoa chini ya milioni tisa.

Rais Biden aliahidi dozi milioni 580 lakini mpaka sasa Marekani imetoa dozi milioni 140.

Umoja wa Ulaya uliahidi dozi milioni 250 mwishoni mwa mwaka - imetuma karibu 8% ya hizo.

Maelezo ya video,

Covax

Kama nchi nyingi za kipato cha kati na maskini , Iran ilinunua chanjo kutoka mpango wa Covax, unaoungwa mkono na WHO ili kutoa dozi eneo ambalo lina uhitaji zaidi.

Mpango wa Covax unanunua na kuuza chanjo kwa bei nafuu na kutoa msaada kwa mataifa maskini.

Lakini mpango wa Covax umekabiliwa na changamoto kubwa ya usambazaji.

Ilipanga kusambaza dozi bilioni mbili kwa mwaka huu 2021 na nyingi zikitokea kituo cha India lakini wakati wimbi la pili la maambukizi lilipotokea, zoezi la usambazaji ulizorota kwasababu India ilisitisha usambazaji wa chanjo nje ya nchi mwezi Mei kwa kuwa taifa hilo lilipata athari kubwa ya maambukizi.

Tangu wakati huo Covax amekuwa ikitegemea kupata msaada kutoka nchi tajiri.

Na usambazaji umekuwa wa kusuasua , baadhi ya nchi zinazopokea bado hazijachanja 2% ya idadi ya watu.

"Hivi sasa dozi huwa zinatolewa kwa kiwango kidogo, taarifa ikiwa imechelewa na hata tarehe ya mwisho kutumia ikiwa imekaribia - na kufanya zoezi kuwa gumu katika kuweza kusambaza katika nchi ambazo zinazoweza kuzichukua," anasema Aurélia Nguyen, mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Covax.

Usambazaji sio shida ya dunia yote.

Nchi zenye uwezo wa kiuchumi zimekuwa zikihodhi chanjo za ziada, kwa mujibu wa Airfinity, kampuni ya uchambuzi wa sayansi inayotafiti usambazaji wa chanjo duniani.

Watengenezaji wa chanjo sasa wanatengeneza dozi 1.5bn kila mwezi, 11bn zitakuwa zimetengenezwa mwishoni mwa mwaka.

"Wanazalisha kwa idadi kubwa na kiwango kimeongezeka sana kwa miezi mitatu au minne iliyopita," anasema Dk Matt Linley, mkuu wa utafiti wa Airfinity.

Nchi tajiri zinaweza kuwa na dozi 1.2bn ambazo hazihitaji - hata ikiwa wataanza kutoa nyongeza.

Sehemu ya tano ya dozi hizo - chanjo milioni 241 - zinaweza kuwa katika hatari ya kupotea kama hazitatolewa hivi karibuni, anasema Dk Linley.

Kuna uwezekano kwamba nchi maskini hazitaweza kupokea chanjo isipokuwa zikiwa zimebaki angalau na miezi miwili kabla ya muda wake kumalizika.

"Sidhani kuwa ni lazima kwa nchi tajiri kuwa wabinafsi, zaidi ni kwamba hawakujua ni chanjo gani itafanya kazi," anasema Dk Linley. "Hivyo walipaswa kununua baadhi ya chanjo hizo."

Pamoja na utafiti wa hivi karibuni, Airfinity inatarajia kuonesha serikali kuwa kuna chanjo nzuri na kwamba hawaitaji kuweka za ziada.

Badala yake wanaweza kuchangia kile wasichokihitaji sasa na kuwa na kuwa na uhakika kwamba dozi zaidi zitatolewa katika miezi ijayo.

Hawataki kuwekwa mbali, "anasema Agathe Demarais." Pia ni kuhusu msukumo wa siasa za ndani kwa sababu sehemu ya wapiga kura labda hawatafurahi kuona chanjo zikitolewa, ikiwa bado wanahisi kwamba bado zinahitajika nyumbani."

Serikali ya Uingereza inasema haina akiba ya chanjo na imefanya makubaliano na Australia kutoa dozi milioni nne ambazo zitarudishwa kutoka kwa mgawo wa Australia mwishoni mwa mwaka.

"Usambazaji na utoaji wa chanjo umesimamiwa kwa umakini nchini Uingereza kutoa kwa wale wote wanaostahiki fursa ya kupewa chanjo kwa haraka iwezekanavyo," anasema msemaji wa Idara ya Afya na ustawi wa Jamii.

Aurélia Nguyen wa Covax anasema sio serikali tu ambazo zinahitaji kuchukua hatua.

"Pia tunahitaji watengenezaji watimize ahadi zao na Covax kutoa kipaumbele kwa mikataba ya mataifa ambayo tayari hayana dozi za kutosha."

Ikiwa sasa wazalishaji wa chanjo duniani wanazalisha dozi bilioni 1.5 kila mwezi, anasema, swali ni kwanini dozi chache zinawafikia nchi masikini.

"Eneo ambalo lina uhitaji wa Covax , serikali zinapaswa kuweka foleni ili tuweze kupata dozi ambazo tumezitaka mapema."

Kwa Bahar na familia yake, dozi hizo sio idadi ya namba tu bali ni maisha halisi, ya marafiki na familia.

Kila siku chache, anasikia simulizi nyingine ya mtu kufa kutokana na corona. Wakati marafiki katika chuo kikuu walisema hawataki kupata chanjo alikuwa akijaribu kubishana nao lakini hawezi kufanya hivyo tena, inasikitisha sana.

"Ninajaribu tu kupuuzia lakini ni ngumu kuona watu hawatumii fursa waliyonayo."