Mzozo wa DRC: Wanafunzi wanaosoma katika shule za mpakani na Rwanda wakwama

Wanafunzi wa Rwanda wanaosoma mjini Goma-DRC wanakabiliwa na vitisho vya usalama kutokana na mzozo uliopo kati ya nchi hizo mbili jirani.
Hali bado si shwari mpakani na hii inazua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wazazi katika mji wa Rubavu ambao watoto wao wanaosomea nchini DRC , wakisema kuna hatari ya wao kulengwa kutokana na jinsi walivyo.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana akiwa mjini Rubavu amezungumza na baadhi ya wanafunzi na wazazi ili kujua jinsi mivutano na machafuko hayo yanavyoathiri elimu yao.
Alianza kwa kutembelea mtaa wa kifahari uliopewa jina la RCD mjini Rubavu wanamoishi raia wengi
Anasema kwamba baadhi ya wanafunzi raia wa Rwanda wanaoishi katika eneo hilo walishindwa kurejea katika shule zao mjini Goma.
Wanafunzi hao ambao hawakutaka majina yao kutajwa kwa sababu za usalama wao walielezea masaibu yao:
Mmoja wao ananukuliwa akisema kwamba wale walio na familia zao mjini Goma walikubaliwa kusalia huku wengine walio na familia nchini Rwanda wakitakiwa kurudi nchini Rwanda mara moja.
Mama mmoja ambaye pia hakutaka jina lake litajwe kwa sababu ya usalama wa watoto wake 4 wanaosomea mjini Goma anasema kwamba awali watoto wake wamekuwa wakisomea mjini Goma na kurudi nchini Rwanda bila tatizo lolote lakini sasa ni mmoja ya wazazi ambao wamekuwa na shaka.
“Watoto wangu wanasomea Goma huku wakirudia nchini Rwanda, mwanzo hakukuwa na tatizo lakini kwa sasa kutona na hali ilivyo tuna mashaka sana. siku ya kwanza ya maandamano nilipata wasi wasi mkubwa-mtoto wangu alichukua boda boda toka shuleni ili kumfikisha mpakani walipofika katikati ya njia alipomwambia mwendesha boda boda kuwa anaelekea kwenye mpaka wa Rwanda akamuacha hapo kwa kumwambia :’kumbe wewe ni Mnyarwanda’ si unaona ni shida?’
Lakini afisa tawala wana maoni gani kuhusa hali hiyo?
Mwandishi wetu alifanikiwa kumhoji, Meya wa mji wa Rubavu Ildephonse Kambogo aliyesisitiza kwamba Rwanda inawataka raia wake kuzingatia swala la usalama wao na kupunguza safari zao kwenda nchini Congo.
Meya huyo anasema kwamba wamekuwa wakifanya mikutano ili kuuhamasisha umma kuepuka safari zisizo na za lazima nchini DR Congo.
Kulingana na mzazi mmoja ,wanafunzi kutoka Rwanda wanaosomea mjini Goma ni wengi japokuwa idadi yao kamili haijulikani.
Hapo awali manispaa ya mji wa Rubavu ilikuwa na mpango wa kuwataka wanafunzi wa Rwanda wanaosomea mjini Goma kuja kusomea hapa mjini Rubavu na kuanza kutayarisha baadhi kwa lugha ya kiingereza,lakini inavyoelekea mpango huo ulishindwa kufanya kazi. Na baadhi ya wazazi hawakuridhika na mpango huo:
‘’Mpango bado upo lakini hatujaridhika na mipango iliyochukuliwa wala viwango vyenyewe vya elimu - ina maana wale watoto wamezoea kusomea Congo na ili kuwaweka sawa na wenzao wanaosomea hapa Rwanda ni shida kubwa sana, ndiyo sababu tuliamua kuwabakisha Congo ingawaje sasa usalama wa huko unatutia woga na hatujui la kufanya.’’
Raia wa mjini Rubavu wanasema wanapendelea amani ipatikane katika upande wa pili wa mpakani ili Watoto wao wanaosomea nchini Congo warudi haraka shuleni.
Mfumo wa elimu wa nchi mbili ni tofauti - huku Congo wakitumia Kifaransa ,Rwanda wanatumia lugha ya Kiingereza.