Jumuiya ya Afrika Mashariki, majeshi na mustakabali wa amani DRC

Rashid Abdallah

Mchambuzi

th

Chanzo cha picha, State House Kenya

Tangazo la mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Uhuru Kenyatta la kutaka kupelekwe kikosi cha kijeshi cha jumuiya hiyo katika nchi mwanachama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limeungwa mkono na nchi jumuiya pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Endapo tangazo hilo litafanyiwa kazi kivitendo, litabadili sura ya mgororo wenyewe, kutoka kuwa mgogoro wa DRC na baadhi ya nchi jirani kwa upande mmoja, dhidi ya makundi ya waasi na kuwa mgogoro rasmi wa jumuiya nzima ya Afrika Mashariki dhidi ya makundi hayo.

  Ufanisi wa nguvu za kijeshi  

DR Congo haijawahi kupumzika kupambana na makundi ya waasi. Tangu kuingia madarakani Rais Félix Tshisekedi, Januari 2019, ameahidi mara kadhaa kutokomeza uasi mashariki mwa nchi hiyo. Mapambano yanaendelea lakini nafuu kwa raia haijapatikana. Waasi bado wana nguvu za kushambulia raia na wanajeshi. 

Uganda pia imeingia kijeshi Kongo mwishoni mwa 2021 chini ya operesheni  Shujaa, baada ya mashambulizi katika ardhi yake kutoka kwa Allied Democratic Forces (ADF). Ingawa operesheni hiyo imezuia tu mashambulizi mapya ndani ya Uganda, haijafanikiwa kulisambaratisha kundi hilo.

Kwa miaka mingi pia kipo kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO) kutoka nchi mbalimbali, lengo ni kuleta amani. Nchi za Afrika Mashariki,Tanzania na Kenya zinachangia wanajeshi katika kikosi hicho huku Tanzania ikiwa na walinda amani wapatao 800 ndani MONUSCO.

MONUSCO imeundwa takribani miongo miwili iliopita. Nguvu na wingi wa makundi ya waasi huzifanya operesheni za walinda amani hao, kuonekana hazikidhi haja mbele ya macho ya raia wanaoshambuliwa mara kwa mara.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Mwili wa askari wa DRC ulirudishwa nchini DR Congo kutoka mpaka wake na Rwanda

Ukubwa wa mgogoro wa Kongo kwa nchi za Jumuiya

Mashariki mwa DRC ni eneo linalotumiwa na makundi mengi, hata yale ambayo hayapigani moja kwa moja na serikali ya nchi hiyo. Ukubwa wa msitu uliopo katika taifa hilo, huvutia makundi ya waasi ya ndani na yale ya nchi jirani.

Kundi la RED-Tabara na National Forces of Liberation (FNL), haya yametoka Burundi na yana uadui na serikali ya nchi hiyo.

Yanajificha Mashariki mwa DRC na kufanya mashambulizi katika ardhi ya Burundi.

Katika mazungumzo yake ya kwanza na vyombo vya habari tangu aingie Ikulu hapo Juni 2020, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, alieleza Mei 10, 2022, kwamba  ikiwa makundi hayo yatakuwa tayari kwa mazungumzo ya usuluhishi, serikali yake iko tayari.

Kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FLDR) licha ya kufanya mashambulizi ndani ya Kongo, linaundwa na wapiganaji wanotajwa kutokea Rwanda na idadi kubwa ni maafisa na wanamgambo wa zamani waliokimbilia Kongo baada ya kuhusika na mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda.

Uganda pia inakumbwa na kitisho cha makundi kadhaa likiwemo lile hatari zaidi la Allied Democratic Forces (ADF). Kundi hili limetangaza utiifu kwa kundi la Islamic State, hufanya mashambulizi ndani ya Kongo na Uganda.

Changamoto za kikosi cha pamoja

Wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki inawaza kuwa na kikosi cha pamoja kupambana na uasi, Kongo inaituhumu Rwanda kulisaidia kundi la M23.

Tuhuma hizi zimeutia shaka kubwa uhusiano wa nchi hizo na pia kuhatarisha maisha ya Wakongo wenye asili ya Rwanda.

Hii si mara ya kwanza kwa Rwanda kutuhumiwa kufadhili M23. Ripoti ya Umoja wa Mataifa, iliyochapishwa na vyombo vya habari 2012 iliituhumu Rwanda kuunga mkono kundi hilo.

Pia, ripoti hiyo ikaituhumu Uganda vilevle kuunga mkono M23. Hata hivyo, Rwanda  na Uganda zimekana mara kadhaa kuhusika na ungaji mkono huo wa makundi ya waasi .

DRC imeridhia kupelekwa kikosi cha kikanda katika ardhi yake, ila kwa sharti kwamba Rwanda isishiriki katika kikosi hicho. Hili linaleta mtihani mkubwa kwa mpango huu ambao bado uko katika hatua za awali.

 

  Kwanini mgogoro wa DRC ni mgumu?

Chanzo cha picha, Reuters

Ugumu wa mgogoro wa DRC unachangiwa  na wingi wa makundi ya waasi. Hadi Februari mwaka huu, kuna jumla ya makundi 120 yaliyojificha huko kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la The Guardian la Uingereza. 

Hali ni tofauti na Somalia, ambako kundi linalosumbua ni la Al Shabaab tu, au Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado kunakopatikana kundi la Kiislamu. Hata Nigeria kwa miaka mingi kundi lilikuwa ni moja tu la Boko Haram kabla ya Islamic State nalo kuingia katika eneo la Afrika Magharibi.

Makundi yaliyopo DRC yamezaliwa katika nchi nne tofauti, Kongo yenyewe, Rwanda, Burudi na Uganda. Kila kundi lina sababu zake za kushika silaha. Wakati fulani huko nyuma hata waasi kutoka Sudan Kusini walikuwepo Kongo kabla ya kuondoka.

Huu si mzozo ambao mzizi wake ni mmoja; ukiridhia matakwa ya kundi moja, utakuwa umepatia ufumbuzi matakwa ya makundi yote. Hapana. Hoja ama sababu za  ADF kushika silaha hazifanani na za LRA, wala matakwa ya Red-Tabara si matakwa ya FLDR.

Mkusanyiko wa hayo yote huufanya mgogoro DRC kuwa mgumu zaidi kuupatia suluhisho kuliko migogoro mingi barani Afrika. Ili amani ya kudumu ipatikane, ni lazima makundi yote, yaweke silaha chini. Makundi ambayo yanayotoka nchi tofauti na yapo kwa dhamira tofauti.

Makovu ya ukoloni, tawala za kidikteta, ukabila, misimamo mikali ya kiimani, rasilimali zilizopo; ni kati ya mambo yaliyochangia uwepo wa haya makundi. Yapo kwa muda mrefu na waathirika wakubwa wa matendo ya kikatili ni raia.

Jumuiya ya Afrika Mashariki itamaliza uasi DRC?

Kwa hakika operesheni za kijeshi wakati mwingine huifanya migogoro kutoka kuwa mibaya hadi kuwa mibaya zaidi. Operesheni hizo hazitoi uhakika wa kuisha kwa mgogoro, ingawa hiyo haipaswi kuwa hoja ya kutotumia nguvu ya kijeshi ikihitajika.

Swali la ikiwa hatua ya kupeleka vikosi itamaliza uasi, haliwezi kuwa na jawabu ya haraka haraka ya ‘ndio au hapa’.

Kwa sababu hata ikiwa operesheni hiyo itafanikiwa, itakuwa ni operesheni ya muda mrefu, kabla ya kuifikia hatua ya mwisho ya kuhesabu hasara na faida.

Bila shaka, Jumuiya ya Afrika Mashariki ina kibarua kikubwa ikiwa mpango uliopendekezwa utatekelezwa kivitendo.

Kwa upande mwingine, njia za kisiasa kutafuta suluhu zinapaswa kupewa kipaumbele kwanza kabla kutumia njia ya kupeleka majeshi, ambayo inaweza kuwa njia ya mwisho kabisa baada ya njia nyingine za kidiplomasia kushindikana.