‘Tutachukua hatua kali kujilinda’-Urusi sasa yaionya Lithuania

th

Chanzo cha picha, EPA

Urusi imeionya Lithuania kuhusu madhara makubwa baada ya kupiga marufuku usafirishaji wa baadhi ya bidhaa kwenye eneo la Urusi la Kaliningrad.

Urusi "hakika itajibu vitendo hivyo vya uhasama," afisa mkuu wa usalama Nikolai Patrushev alisema.

Lithuania inasema ni kufuatia tu vikwazo vya Umoja wa Ulaya vilivyowekwa kutokana na uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.

Kaliningrad - eneo la kimkakati ambapo Meli ya Baltic ya Urusi ina makao yake makuu - haina mpaka na Urusi bara.

Eneo la magharibi lilitwaliwa kutoka Ujerumani baada ya Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945 na limepakana na wanachama wa EU na Nato Lithuania na Poland.

Eneo hilo - ambalo inakadiriwa kuwa watu milioni moja wanaishi - linategemea sana uagizaji wa malighafi na vipuri kutoka Urusi na EU.

Gavana wa mkoa Anton Alikhanov alisema marufuku hiyo itaathiri  karibu 50% ya bidhaa ambazo Kaliningrad inaagiza kutoka nje.

Wakati wa ziara ya Jumanne huko Kaliningrad, Bw Patrushev alisema kizuizi cha Lithuania kilichochewa na Magharibi "katika ukiukaji wa... sheria za kimataifa".

Katibu wa Baraza la Usalama la Urusi alionya kwamba "hatua zinazofaa" zitachukuliwa "katika siku za usoni" 

"Madhara yao yatakuwa na athari mbaya kwa watu wa Lithuania," aliongeza, bila kutoa maelezo zaidi.

Mapema Jumanne, balozi wa EU aliitwa kwa wizara ya mambo ya nje ya Urusi juu ya kizuizi hicho.

Chanzo cha picha, Reuters

Wiki iliyopita, mamlaka ya Kilithuania ilitangaza kupiga marufuku bidhaa zilizowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kupita katika eneo lao hadi Kaliningrad.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Lithuania Gabrielius Landsbergis alisema: "Si Lithuania inayofanya lolote: ni vikwazo vya Ulaya vilivyoanza kufanya kazi kuanzia tarehe 17 Juni... Ilifanyika kwa mashauriano ya Tume ya Ulaya na chini ya miongozo ya Tume ya Ulaya."

EU imekariri kauli ya Lithuania, ikisema kwamba nchi hiyo inatekeleza tu vikwazo vilivyowekwa na EU kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Orodha ya vikwazo ni pamoja na makaa ya mawe, Chuma ,vifaa vya ujenzi na teknolojia ya hali ya juu.

Kama mwanachama wa muungano wa kijeshi wa Nato, Lithuania inalindwa na mikataba ya pamoja ya ulinzi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price alisema Marekani inasimama upande wa Lithuania, akiongeza kuwa kujitolea kwa nchi hiyo kwa kifungu cha 5 cha Nato - ambacho kinaona shambulio dhidi ya nchi moja mwanachama kama shambulio la wote - ni "vazi la chuma".

Maafisa wa Urusi wamekasirishwa na Lithuania - na EU - juu ya kupiga marufuku usafirishaji wa baadhi ya bidhaa kwenda Kaliningrad. Wanaifananisha na kizuizi.

Lakini wizara ya mambo ya nje ya Moscow inaposema "Urusi inahifadhi haki ya kuchukua hatua kulinda maslahi yake ya kitaifa", inamaanisha nini hasa? Vitendo gani na lini?

Kremlin inasema inajaribu kusuluhisha hilo hivi sasa.

Siku ya Jumatatu, msemaji wa Rais Vladimir Putin, Dmitry Peskov, alibainisha kuwa "hali kwa kweli ni mbaya sana na inahitaji uchambuzi wa kina kabla ya kuandaa hatua zozote au maamuzi yoyote. Uchambuzi huu wa kina utafanywa katika siku chache zijazo."

Jana , mmoja wa washirika wa karibu wa Bw Putin, Nikolai Patrushev, alisafiri kwa ndege hadi eneo la Kaliningrad kujadili "usalama wa kitaifa kaskazini-magharibi mwa Urusi". Bw Patrushev ni katibu wa Baraza la Usalama lenye nguvu la Urusi. Maafisa wanadai ziara hiyo ilipangwa muda mrefu kabla. Ni bahati mbaya.

Linapokuja suala la "usalama wa taifa", Kaliningrad ni eneo muhimu. Meli za Baltic za Urusi zina makao yake makuu huko. Na hapo awali Moscow ilituma makombora yenye uwezo wa nyuklia wa Iskander katika eneo la Kaliningrad.