Uchaguzi Kenya 2022:Raila na Ruto watofautiana kuhusu sajili ya wapiga kura itakayotumiwa

Na Yusuf Jumah

BBC Swahili

TH

Chanzo cha picha, IEBC/TWITTER

Maelezo ya picha,

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya Wafula Chebulati

 Tume  huru ya Uchaguzi na mipaka nchini Kenya sasa ipo katika njia panda kuhusu itakavyowaridhisha wagombeaji wawili wakuu wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti tarehe  tisa mwaka huu .

  Mgombeaji wa urais  wa muungano wa Azimio One Kenya Raila Odinga na mpinzani wake wa Kenya Kwanza William Ruto ambaye pia ndiye naibu wa Rais  wametofautiana kuhusu matumizi ya sajili ya elktroniki na ile ya kawaida(Karatasi) katika uchaguzi ujao .

Tume ya Uchaguzi ,IEBC ilisema haitatoa sajili za wapiga kura kwenye vituo vya kupigia kura na kusisitiza kutumia mfumo wa kielektroniki.

Huku  Raila  akisema kuna haja ya matumizi ya rejista za kielektroniki na za karatasi za  wapiga kura katika uchaguzi ujao, Ruto  alionekana kuunga mkono  uamuzi wa  IEBC wa kutegemea sajili ya wapigakura wa kielektroniki pekee.

Raila katika hoja zake  alitaka kujua ni kwa nini IEBC ilisita kutumia sajili ya wapiga kura iliyo kwenye karatasi .

Wakili wake Paul Mwangi aliteta kuwa hii ni kinyume na Sheria ya Uchaguzi.

Alisema kuwa sheria inaitaka tume kuwa na daftari la mwongozo la wapiga kura kama mfumo wa pili wa utambuzi wa wapiga kura endapo mfumo wa kielektroniki utafeli.

"Msisitizo sio kwamba usitumie teknolojia. Tumia mifumo yote ambayo imeelezwa lakini sheria inakutaka uwe na mfumo huo iwe utatumika au la," Mwangi alisema.

Ruto  kwa upande wake  amesema muungano wa Kenya Kwanza hauna wasiwasi na matumizi ya rejista ya kielektroniki mradi tu usalama wake umehakikishwa.

"Kumekuwa na ripoti kwamba Kenya Kwanza inataka sajili ya kawaida. Hatutaki rejista ya kawaida. Ukitupa ulinzi wa kutosha kwamba ya kielektroniki itafanya kazi bila uwezekano wowote wa kufeli basi sisi hatuna pingamizi," Ruto alisema.

Mgombea  huyo wa Kenya Kwanza alisema matumizi ya vifaa vya kidijitali katika kuendesha kura ni njia katika demokrasia ya kisasa.

 

Uchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu wagombeaji wa Urais

Chanzo cha picha, IEBC/YWITTER

Maelezo ya picha,

Mgombeaji wa urais wa Muungano wa Azimio Raila Odinga na Mgombea mwenza wake Martha Karua

Katibu mkuu wa chama cha  UDA-anachokiongoza Ruto , Veronicah Maina alikuwa na maoni kwamba daftari la wapiga kura linaweza kuweka njia ya udanganyifu kwa kuwafanya watu kupiga kura mara mbili.

Alieleza kuwa rejista hiyo halisi inatoa nafasi kwa watu kuingia vituoni  na kujifanya wanathibitishwa kutoka kwa sajili halisi ilhali hawajatambuliwa kupitia mashine maalum ya kilektroniki ya  KIEMS.

“Kutokana na hayo, tuna wapigakura wengi ambao hawajajiandikisha wanaoingia kwenye vituo (vya kupigia kura), kupata karatasi za kupigia kura na kupiga kura kwa kukwepa kifaa cha KIEMS,” Maina aliongeza.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilifichua kuwa itatumia mfumo kamili wa upigaji kura wa kibayometriki katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Katika hali ambapo kitambulisho cha kibayometriki kitashindikana, maafisa hao watapitia Mfumo wa Kusimamia Uchaguzi wa Kenya (KIEMS) kwa kutumia nambari ya kitambulisho, ambayo itachukua taarifa za mpigakura ili kutambuliwa.

" Vifaa vya KIEMS hufanya kazi nje ya mtandao katika suala la utambulisho, inafanya kazi kupitia nakala mbadala. Maelezo haya yatakuwa katika kadi ya SD na ikiwa kuna hitilafu kadi ya SD inaweza kuwekwa kwenye kifaa kingine ,"

Taarifa hizo zitajumuisha alama za vidole za mpiga kura, ambazo zitampa nafasi karani wa uchaguzi kufanya upya kitambulisho cha alama za vidole ili kuthibitisha utambulisho wa mpiga kura.

IEBC iliteta kuwa mbinu ya kusajili kwa mikono ina uwezekano wa kutumiwa vibaya ikisema wapiga kura wanapotambuliwa kupitia teknolojia, mfumo huo huweka kiotomati maelezo ya waliopiga kura kumaanisha kwamba ikiwa mtu huyo atajiwasilisha tena, basi mtu huyo hawezi kupiga kura (tena. )

Chanzo cha picha, IEBC/TWITTER

Maelezo ya picha,

Ruto  kwa upande wake  amesema muungano wa Kenya Kwanza hauna wasiwasi na matumizi ya rejista ya kielektroniki mradi tu usalama wake umehakikishwa.

Masuala mengine yaliyojadiliwa

Kando na suala hilo la sajili ya wapiga kura mengine yaliyotolewa na timu ya Azimio ni utoaji wa orodha ya vituo vyote vya kupigia kura, muundo wa karatasi  za kupigia kura na eneo la uchapishaji na idadi ya vifaa vya Kiems vitakavyotumika na nambari zao za mfululizo.

Timu hiyo pia ilihoji ni kwa nini wasimamizi kumi kati ya 47 wa kaunti wa tue ya uchaguzi wanatoka jamii moja.

Pia wanataka wapewe nakala iliyoidhinishwa ya sajili ya wapigakura, maelezo ya jinsi kadi za SD zitakavyopakiwa kwenye vifaa vya Kims na wafahamishwe eneo ambako tume ya uchaguzi itaweka makao yake ya kusimamia shughuli nzima ya kuhesabu kura .

Azimio pia ilitaka kujua ni kampuni gani itachapisha karatasi za kupigia kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

IEBC ilisema itajibu masuala yote ya kiufundi yaliyotolewa na timu ya Azimio na wagombeaji wengine wa urais wiki ijayo.

Naibu Rais William Ruto, mgombea urais wa (UDA) pia alitoa wasiwasi wake kuhusu masuala mbali mbali ya uchaguzi .

Mwenyekiti Wafula Chebukati alisema timu yake imejitolea kuandaa majibu kuhusu masuala yote katika kongamano litakalofanyika  mapema mwezi ujao.

Alisema kuwa tarehe itapangwa kwa wagombeaji wote wa urais kuzuru kiwanda kitakachochapisha karatasi za kupigia kura siku zijazo.

Mengi zaidi kuhusu Uchaguzi wa Kenya