Urusi na Ukraine: Je kutekwa kwa mji wa Severodonetsk kuna maana gani katika mzozo huu?

Ukraine ililazimika kujiondoa katika mji huo baada ya wiki kadhaa za mashambulizi ya Urusi

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Ukraine ililazimika kujiondoa katika mji huo baada ya wiki kadhaa za mashambulizi ya Urusi

Inaweza kuwa waliona kama hatua isiyoweza kuepukika, lakini hiyo haina maana kwamba kutekwa kwa mji wa Severodonetsk ni uchungu kidogo kwa Ukraine.

Kwa muda wa wiki kadhaa lilikuwa jambo kuu la uvamizi wa Urusi, mashambulio makubwa ya risasi na mashambulio ya anga yalifanyika na kusababisha mji huo mkongwe wenye watu chungu nzima  viwanda kuwa vifusi.

Mwishowe, makamanda wa Ukraine walisema kutetea mabaki kungegharimu maisha ya watu wengi sana.

Katika hotuba yake ya Jumamosi usiku baada ya Urusi kuthibitisha udhibiti kamili wa Severodonetsk, Rais Volodymyr Zelensky alisema ilikuwa siku ngumu, ‘’kimaadili na kihisia’’ kwa nchi yake.

Hakuna ubishi, kupoteza mji mkubwa zaidi ambao bado wanashikilia katika mkoa wa Luhansk kunaleta moja ya malengo muhimu ya kimkakati ya Urusi hatua moja karibu.

Tangu kushindwa kwa majaribio yao ya awali ya kuteka nchi nzima, Moscow imelenga kuchukua eneo pana la mashariki linalojulikana kama Donbas.

Hiyo inatokana na maeneo mawili, Donetsk na Luhansk.Lakini, kuchukua Luhansk nzima bado haijahakikishiwa, hata kama kuna uwezekano mkubwa.

 Katika njia ya Urusi ni mji wa Lysychansk, maili chache tu kutoka Severodonetsk - lakini bado ipo mikononi mwa Kiukreni.

 Ni hapa ambapo vikosi vya Ukraine vinafikiriwa kujiondoa baada ya kuachana na Severodonetsk.

Ili kuelewa ni kwa nini Lysychansk ni muhimu, tunahitaji kuelewa jiografia ya eneo hilo na jukumu ambalo limecheza katika vita hadi sasa.

Miji hiyo miwili iko kwenye mto wa Siversky Donets: unapitia Donbas na imekuwa eneo la vita vyenye gharama kubwa sana kwa Urusi.

Maelezo ya picha,

Chanzo: Taasisi ya utafiti wa vita

Hasa, jaribio moja lililofanyika mwezi mmoja uliopita liligharimu kikundi kizima cha batali.

Mamia ya wanaume na makumi ya magari ya kivita yaliangamizwa na mizinga ya Ukraine walipokuwa wakijaribu kufika upande mwingine.

Hakika, pamoja na madaraja yote kati ya Severodonetsk na Lysychansk kuharibiwa, kona ya mto inatoa kizuizi kikubwa cha asili kwa Urusi kusonga mbele zaidi.

Kuongezea hilo, Lysychansk ipo juu ya kilima, na kuchukua nafasi za mwisho za Ukraine huko Luhansk itakuwa pambano la kupanda mlima, kihalisia.

Wachambuzi katika Taasisi ya Utafiti wa Vita wanatoa muhtasari wa kila siku kuhusu mzozo huo.

Katika tathmini yao mnamo tarehe 24 Juni walibaini kuwa ''vikosi vya Ukraine vitachukua maeneo ya ardhini ya juu huko Lysychansk, ambayo inaweza kuwaruhusu kurudisha nyuma mashambulio ya Urusi kwa muda ikiwa Warusi hawataweza kuzingira au kuwatenga''.

Maelezo ya picha,

Wanajeshi waUrusi walikabiliwa vikali walipokuwa wakijaribu kuvuka mto mwezi Mei

Lakini inaonekana hivyo ndivyo Urusi inalenga kufanya.

Wanasonga mbele kutoka kusini, wakidai kuwa ndani ya eneo linaloonekana la jiji.

Msemaji wa wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi alidai kuwa jaribio la vikosi vya Ukraine kutetea Lysychansk na Severodonetsk ''halikuwa na maana wala manufaa yoyote''.

''Kwa kiwango ambacho wanajeshi wetu wanaenda, hivi karibuni eneo lote la [liliyojitangazia uhuru wake] Jamhuri ya Watu wa Luhansk litakombolewa,'' alisema Andrei Marochko, mwakilishi wa jeshi linaloungwa mkono na Kremlin huko Luhansk.

''Vikosi vyetu tayari viko katika maeneo ya mji wa Lysychansk. Kwa hiyo tunaweza kusema tunadhibiti kikamilifu mienendo yote ya wanajeshi wa Ukraine.''

Swali kuu ni: mwisho wa Urusi ni nini?

Je, watajaribu kuchukua Donbas, wakijaribu kuilazimisha Ukraine kukubali usitishaji vita, kunyakua mikoa ya Luhansk na Donetsk na kuchora upya mipaka ya kitaifa?

Hili linawezekana, haswa ikiwa vikosi vya Urusi vimechoka kama wachambuzi wengi wanavyosema.

Inaweza kuwasilishwa nyumbani kama mafanikio.

''Operesheni maalum ya kijeshi ilikomboa'' Donbas, au kile kilichosalia.

Huenda Urusi ikatumai kuwa siasa yenye kutegemea vitendo zaidi ingeingia, huku Ukraine ikishinikizwa kukubali kupotezwa kwa eneo kwa jina la amani na utulivu wa kimataifa.

Ukraine ingekuwa karibu kukataa hii, na mgogoro kufika mwisho ingekuwa matokeo yake.

Vinginevyo, je, Rais Putin atataka kumalizia alichoanza, labda kuchukua pande zote za kusini, au hata kufanya msukumo mwingine kwa Kyiv?

Maelezo ya picha,

BBC inazungumza na baadhi ya maelfu ya wanajeshi wa kigeni ambao wamejiunga na vita dhidi ya Urusi

Ni mtu mmoja tu anayejua jibu la hilo, na hashirikishi mipango yake.

Lakini ikiwa tunataka kutafuta dalili za jinsi hii ''operesheni maalum ya kijeshi'' inaweza kumalizika, tunahitaji kuangalia maneno ya Bw Putin mwenyewe.

Katika hotuba yake mwanzoni mwa Juni, alijilinganisha waziwazi na Peter the Great, akilinganisha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na vita vya upanuzi vya mfalme wa Urusi karne tatu zilizopita.

Ilikuwa, bila shaka, kukiri kwamba vita yake mwenyewe ilikuwa kunyakua ardhi.

''Inaonekana imetuangukia sisi pia, kurejesha na kuimarisha [ardhi zetu],'' Bw Putin alisema.

Akiongea na kundi la vijana wajasiriamali, tabasamu lilitanda usoni mwake.

Ilikuwa wazi kabisa alikuwa akimaanisha uvamizi wake wa Ukraine.

Urusi ilifanya makosa makubwa mwanzoni mwa vita hivi.

Walipuuza nia ya watu wa Ukraine kupinga pamoja na uwezo wa vikosi vyao vya kijeshi.

Kukimbilia kwao Ikulu kulikutana na kushindwa vibaya.

Ilikuwa ni tajriba yenye uchungu, lakini pia somo muhimu.

Maandamano yao ya polepole lakini yasiyokoma ndani ya Donbas yanaonyesha wamejifunza kutokana na makosa yao na wanaonekana kuazimia kutoyarudia.