Hospitali ya Taifa Muhimbili yawatenganisha pacha walioungana

Na Lizzy Masinga

BBC Swahili

Watoto walioungana

Chanzo cha picha, MNH

 

Madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamefanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto pacha walioungana kifuani Rehema na Neema.

Upasuaji huo uliodumu kwa saa 7, ulioanza saa 3 asubuhi na kumalizika saa 9 alasiri, umefanikiwa licha ya ugumu na changamoto kubwa kwa watoto hao kuungana ini, moyo na baadhi ya tishu za ndani.

Upasuaji huo uliofanyika kwa mafanikio umefanyika leo Ijumaa Julai Mosi 2022 kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya 31 kutoka Tanzania na Ireland ambao wanatokea Shirika la Operation Child Life.

Akizungumza na vyombo vya habari, Daktari bingwa wa upasuaji watoto hospitalini hapo, Zaitun Bokhari amesema upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji watoto wadogo 12.

“Madaktari wa usingizi sita, madaktari wa kutengeneza ngozi ‘plastic surgery’ wanne,  madaktari ambao kazi yao kuangalia mfumo mzima wa watoto unakwenda vizuri wawili na wauguzi 6,” amesema.

Kufanyika kwa upasuaji huu leo unaandika historia nyingine kwa kuwa Tanzania inakua nchi ya tatu baada ya Misri na Afrika Kusini katika bara la Afrika kufanya upasuaji mgumu zaidi kwa pacha walioungana.

Maelezo ya video,

Pacha walioshikana Tanzania walio na ndoto kuu

Kadhalika, madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili nchini Tanzania walifanikiwa kuwatenganisha mapacha wawili walioungana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu upasuaji huo uanze katika kituo cha afya cha Dar es Salaam mwaka 1994.

Mapacha hao wa kiume wenye umri wa miezi miwili walitenganishwa na madaktari bingwa 10, miongoni mwao wakiwa Watanzania tisa na mmoja kutoka Ireland.

Pacha hao walikuwa wameunganishwa kwenye sehemu ya tumbo kuelekea kifuani, hali inayojulikana kitabibu kwa jina la omphalopagus.

Uamuzi wa kuwatenganisha nchini Tanzania ulifikiwa mwishoni mwa Julai mwaka 2018, wiki mbili baada ya kulazwa na kufanyiwa matibabu ya magonjwa mbalimbali.

Madaktari pia walishawishika juu ya upatikanaji wa vifaa na wataalamu wa kufanya kazi hiyo.

Hata hivyo, ilichukua zaidi ya siku 50 kukamilisha upasuaji, kwani pacha hao walikuwa chini ya uzani wa kilo 4.5 unaohitajika kila mmoja.

Upasuaji wa kwanza wa mapacha walioungana ulifanyika nchini Tanzania mwaka 1994, lakini haukufaulu kwa sababu mtoto mmoja alifariki baada ya siku 63.

Mapacha walioungana wakoje?

Mapacha walioungana huwa ni wachache sana kutokea au kuwepo, katika watoto laki mbili wanaozaliwa kila mwaka anazaliwa mtoto mmoja tu wa aina hiyo.

Watoto wengi huwa hawawezi kuishi ,hufa mara baada ya kuzaliwa au mimba huharibika.

Watoto hawa uzaliwa katika uzao wa yai moja,hufanana na wana jinsia moja. Kuzaliwa kwa watoto hawa huwa kuna hali ya kustaajabisha,kwa ujumla watoto hao wanaweza kuishi wakizaliwa katika hali hiyo huwa ni kati ya asilimia 5 mpaka asilimia 25.

Katika rekodi za historia zinasema kwamba mapacha wa kuungana wengi wanaoweza kuishi kwa muda mrefu ni wa kike,kwa asilimia 70.