Putin hakutarajia haya yatafanyika alipoivamia Ukraine

th

Chanzo cha picha, Reuters

Tarehe 24 Februari 2022, Urusi iliivamia Ukraine katika  hatua iliyozidisha  mzozo wake nan chi hiyo Jirani tangu kuanza kwa usahama mwaka wa 2014

 Uvamizi huo ulisababisha mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi barani Ulaya tangu Vita vya pili vya dunia  huku zaidi ya Waukraine milioni nane wakikimbia nchi na theluthi moja ya idadi ya watu kuhamishwa.

Hata hivyo vita hivyo vimeleta matokeo ambayo kamwe rais wa Urusi Vladmir Putin hakuyategemea katika mpango wake na wakuu wake wa kijeshi .

Wadadisi wanasem Putin alikuwa na mpango wa kuingia Ukraine na kuidhibiti serikali yan chi hiyo baada ya wiki chache lakini mgogoro huo umedhihirisha kwamba hali sio rahisi kama alivyofikiri .Kando na  athari za vita hivyo kwa dunia nzima ,kuna mambo haya manne ambayo  Putin hakufikiria yangefanyika

Unaweza pia kusoma

      Nato itazidisha wanachama wake

Nchi ambazo awali zilikuwa haziegemei upande wowote ambazo zinapakana na Urusi sasa zinataka kujiunga na muungano wa kujihami wa Nato . Finland na Sweden ni nchi za hivi punde kuiga hatua katika jitihada zao za kujiunga na muungano huo ambao umejitokeza kama mlinzi mkubwa kwa nchi zinazoonekana kuchokozwa na ubabe wa Urusi. 

Urusi inapinga vikali mataifa hayo mawili kujiunga na imetumia upanuzi wa muungano wa kijeshi wa kujihami wa nchi za Magharibi kama kisingizio cha vita vyake nchini Ukraine.

Nchi zote mbili zimeshikilia msimamo wa kutoegemea upande wowote kwa miaka, lakini tangu Urusi ilipovamia Ukraine uungwaji mkono wa wanachama wa Nato umeongezeka sana.

Finland na Uswidi zilitangaza nia yao ya kujiunga na muungano wa kujihami wa nchi za Magharibi wenye wanachama 30 mwezi Mei, ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Awali Uturuki ilitishia kupinga ombi lao lakini baada ya saa nne za mazungumzo katika mkutano wa Nato mjini Madrid nchi hizo tatu zilifikia mwafaka. Viongozi wa Nato wanatarajiwa kuzialika rasmi Finland na Sweden kuwa wanachama kabla ya kumalizika kwa mkutano huo.

Kwanini zinajiunga sasa?

Vitendo vya Vladimir Putin vimesambaratisha hali ya utulivu iliyodumu kwa muda mrefu kaskazini mwa Ulaya, na kuziacha Sweden na Finland zikihisi hatari.

Waziri Mkuu wa zamani wa Ufini Alexander Stubb alisema kujiunga na muungano huo ni "makubaliano yaliyofanywa" kwa nchi yake mara tu wanajeshi wa Urusi walipoivamia Ukraine mnamo tarehe 24 Februari.

Kwa Wafini wengi, matukio ya Ukraine huleta hali wanayoifahamu vizuri. Wanasovieti walivamia Finland mwishoni mwa 1939. Kwa zaidi ya miezi mitatu jeshi la Finland liliweka upinzani mkali, licha ya kuwa idadi yao ilikuwa ndogo sana.

Waliepuka kutawaliwa  lakini waliishia kupoteza 10% ya eneo lao.

Kutazama vita nchini Ukraine vikitokea ilikuwa kama kufufua historia hii, alisema Iro Sarkka, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Helsinki. Wafini walikuwa wakitazama mpaka wao wa kilomita 1,340 (maili 830) na Urusi, alisema, na kufikiria: "Je, hii inaweza kutokea kwetu?"

Chanzo cha picha, Reuters

Marekani kuongeza idadi ya wanajeshi wake Ulaya

Jambo la mwisho ambali Putin alitegemea vita vyake vitasababisha ni hasimu wake mkubwa Marekani kuapa kuongeza idadi ya wanajeshi na silaha karibu na mipaka yake .Kutokana na umoja  wan chi  za Ulaya na  Marekani katika kulaani  uvamizi wa Ukraine ,Marekani sasa imejipata na fursa ya kuongeza nguvu zake za kijeshi barani Ulaya na karibu na mipaka ya  Urusi .

Marekani itaongeza uwepo wake wa kijeshi kote Ulaya kwani Nato ilikubali "mabadiliko ya kimsingi" katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Makao makuu ya jeshi ya kudumu yataundwa nchini Poland, wakati meli mpya za kivita za Marekani zitaenda Uhispania, ndege za kivita nchini Uingereza na wanajeshi wa ardhini kuelekea Romania.

Bw Biden alisema Nato "inahitajika zaidi kuliko ilivyowahi kuwa".

Muungano huo una maboresho  makubwa zaidi tangu Vita Baridi, mkuu wa Nato Jens Stoltenberg alisema. 

Mpango huo mpya katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi utamaanisha zaidi ya wanajeshi 300,000 walio tayari zaidi mwaka ujao, kutoka kiwango cha sasa cha 40,000.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza (MoD) pia imesema inaongeza kwa kiasi kikubwa vikosi kwa ulinzi wa pamoja wa Nato, na meli zaidi za kivita, ndege za kivita na vikosi vya ardhini vikiwa tayari - ingawa MoD ilisema haitatoa maelezo juu ya idadi kama zilivyo.

Tangazo la Marekani linaona kwamba inaboresha uwepo wake katika bara zima lakini hasa katika Ulaya ya Mashariki ambako makao makuu mapya ya Kikosi cha 5 cha Jeshi yatawekwa.

Bwana Biden alirudia ahadi ya muungano wa "kulinda kila inchi" ya eneo lake, akisema: "Tunamaanisha hivyo tunaposema shambulio dhidi ya mtu mmoja ni shambulio dhidi ya wote.

  Kutengwa zaidi na nchi za magharibi

Chanzo cha picha, Getty Images

 Vikwazo Zaidi vimezidi kuifuata Urusi na watu mashuhuri katika serikali ya Urusi .

Kampuni kadhaa za kigeni zimeendelea pia kuondoka Urusi  na kuitenga Zaidi nchi hiyo kutoka jamii ya kimataifa .

Hatua hiyo imeifanya Urusi kujipata ikiwatafuta washirika wapya hasa barani Afrika na Asia ili kuendelea na ushirikiano wa kibiashara na mauzo ya bidhaa zake .

  Vita vya Ukraine kudumu kwa muda mrefu

Chanzo cha picha, AFP

Wadadisi wanakubali kwamba Putin na makamanda wake walijua kwamba uvamizi wa Ukraine ungedumu tu kwa wiki chache .

Hata hivyo hatua ya Ukraine  kuanzisha vita vya kujilinda iliwashangaza wengi Mambo yalizidi kuwa mabaya wakati nchi za Ulaya zilipoanza kuipa Ukraine misaada ya kijeshi ili kupambana na  Urusi .

Kadri vita hivyo vinavyoendelea kwa kipindi kirefu ndivyo mzozo huo unavyozidi kuwa mbaya kwa pande zote mbili .