Putin ashinikiza vikosi vyake kusonga mbele  licha ya kutekwa kwa Lysychansk

TH

Chanzo cha picha, EPA

Rais wa Urusi Vladimir Putin amemuamuru waziri wake wa ulinzi kuendeleza mashambulizi nchini Ukraine baada ya Urusi kuuteka mji wa Lysychansk.

Bw Putin alionyeshwa kwenye runinga ya Urusi akitoa wito kwa vikosi vya pande zingine kutekeleza malengo yao kulingana na "mipango iliyoidhinishwa hapo awali".

Utekaji  huo unamaanisha kuwa eneo lote la Luhansk sasa liko mikononi mwa Urusi.

Hapo awali gavana wa eneo hilo la Ukraine alisema mji huo ulisalimishwa  ili Warusi wasiuharibu kwa mbali.

Wanajeshi sasa wamehamia maeneo mapya yenye ngome, Serhiy Haidai aliambia BBC.

Kupoteza mji huo na kukabidhi udhibiti wa Luhansk kwa Urusi ilikuwa chungu, alisema, lakini akaongeza: "Hii ni vita moja tu tumepoteza, lakini sio vita mapambano."

Aliomba silaha zaidi kutoka Magharibi ili kukabiliana nguvu za Urusi .

Unaweza pia kusoma

Rais Volodymyr Zelensky ameahidi kwamba vikosi vya Ukraine vitarejea kuchukua tena Lysychansk "kwa hisani ya ongezeko la  usambazaji wa silaha za kisasa".

Urusi sasa imeongeza mashambulizi yake katika miji katika eneo jirani la Donetsk, huku maeneo yanayozunguka Sloviansk na barabara kati ya Lysychansk na Bakhmut yakilengwa, kulingana na vikosi vya Ukraine.

Kwa pamoja mikoa ya Donetsk na Luhansk huunda eneo la viwanda la Donbas.

Bw Putin alionekana akimwambia Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu kwamba wanajeshi walioshiriki katika kampeni ya kukamata Luhansk wanapaswa "kupumzika na kukuza uwezo wao wa kivita".

"Vitengo vingine vya kijeshi, ikiwa ni pamoja na kundi la Mashariki na kundi la Magharibi, lazima vitekeleze majukumu yao kulingana na mipango iliyoidhinishwa hapo awali," alisema, akielezea matumaini kwamba katika nyanja hizo watapata mafanikio sawa na katika eneo la Luhansk.

Muda mfupi kabla ya kuzindua uvamizi wa Ukraine mnamo tarehe 24 Februari, Bw. Putin alitambua Luhansk na Donetsk zote kuwa nchi huru. Vikosi vinavyoungwa mkono na  Urusi vilianza uasi huko mnamo 2014 - mwaka ambao Urusi pia ilishikilia peninsula ya Crimea.

Zaidi ya wiki moja iliyopita, wanajeshi wa Urusi waliiteka Severodonetsk - ambayo mashambulizi ya mabomu ya Urusi yamesababisha  kuwa magofu.

 

Chanzo cha picha, Reuters

Akiandika saa chache baada ya kuanguka kwa Lysychansk, mshauri wa rais Oleksiy Arestovych hata alienda hadi kuita utetezi wa Lysychansk-Severodonetsk "operesheni ya kijeshi iliyofanikiwa".

Kwa kuzingatia kwamba bendera ya Urusi sasa inaruka juu ya miji yote miwili, mantiki hiyo inaweza kuonekana kuwa potovu kidogo, lakini maoni yake ni kwamba walikuwa wakicheza mchezo wa muda  mrefu, wakijipa muda muhimu

Ili kuelewa mantiki hii, unahitaji kuelewa umuhimu wa silaha za Magharibi kwa ulinzi wa Ukraine. Kwa kifupi, bila vifaa vya Nato wangekuwa katika shida kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.

Kadiri wanavyoweza kuchelewesha hatua  ya Urusi, ndivyo roketi za hali ya juu zaidi na mifumo ya ufundi wanaweza kuleta kwenye mapigano. Mifumo ya HIMARS inayotolewa na Marekani, ambayo tayari inafanya kazi, inasemekana kubadilisha kwa kiasi kikubwa safu ya mapigano. Muda zaidi unamaanisha ugavi zaidi, ambao kwa upande wake unaelekeza mizani kwa upande wao, haswa ikizingatiwa kwamba vikwazo vinamaanisha kuwa Urusi inajitahidi kuchukua nafasi ya vifaa na risasi iliyotumiwa. 

Sasa kwa mtazamo wa Urusi. Lengo lao lililotajwa ni kutwaa, wanasema "ukombozi", wa Donbas. Kuchukua Luhansk kunaleta hatua hiyo karibu.

Hakika, umuhimu wake ulisisitizwa na Rais Putin jana , alipowapa  makamanda "Mashujaa wa Urusi" tuzo ya juu zaidi ya Shirikisho.

Wanajeshi watatu wa Ukraine ambao wamehudumu huko Donbas wameelezea mapigano huko kuwa ya kikatili.

"Warusi wanapenda kuharibu jiji, kijiji, kabisa. Hawajali ni nani  yuko humo- raia wa Kiukreni au wanajeshi," Mark, mpiganaji wa kujitolea aliyerudi kutoka mstari wa mbele katika eneo la Luhansk, aliniambia.

Askari mwingine, Nikolai, aliniambia atakuwa anadanganya kama hangekubali kwamba  mapigano yalikuwa "ya kutisha". 

Wanajeshi wote watatu wanakubaliana na Ukraine kujiondoa wakati wanajeshi wake wamezidiwa nguvu: "Ni vigumu sana kushikilia ardhi. Ni kujitakia  vifo vingi. Hakuna kilichosalia hapo sasa. Hakuna raia. Hakuna jiji. Walilishambulia kwa mabomu."

Hawawezi kutoa maelezo ya majeruhi, lakini walizungumza  kwamba waliojeruhiwa au kuuawa ni "wengi". "Watu tuliosoma nao, tuliokula pamoja nao, watu waliojitolea kama sisi. Wengi wametoweka."

Na bado, walisisitiza kwamba watarejea Donbas ndani ya siku chache ili kupigana.