Ndoto iliyozimika – Ingekuwaje kama Tanganyika na Burundi zingeungana miaka 60 iliyopita?

Na Ezekiel Kamwaga

Mchambuzi

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika safari yake ya mwisho kutembelea Tanzania – wakati huo ikijulikana kama Tanganyika, mwanzoni mwa miaka ya 1960, Waziri Mkuu wa kwanza wa Burundi, Louis Rwagasore, alimwambia Baba wa Taifa la Tanzania, Julius Nyerere, ndoto yake moja kubwa; kwamba baada ya nchi zao kupata Uhuru, waunde Shirikisho la Tanganyika na Burundi. Hiyo ndiyo kumbukumbu iliyobaki kichwani kwa Mwalimu wakati rafikiye huyo akipanda ndege kurejea Bujumbura.

Nyerere aliwasimulia kumbukumbu yake hiyo viongozi wa kisiasa wa taifa hilo mara kwa mara wakati akiwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi mwishoni mwa miaka ya 1990. Kwa bahati mbaya, Rwagasore aliuawa kwa kupigwa risasi baada ya kuwa Waziri Mkuu kwa wiki mbili tu– Septemba 28 hadi Oktoba 13 mwaka 1962. Kifo chake kinahusishwa sana na njama za wakoloni Wabelgiji pamoja na mivutano ya kikabila ya ndani ya Burundi.

Wakati Burundi ikiadhimisha miaka 60 ya Uhuru wake Julai Mosi mwaka huu, mjadala mkubwa katika jamii ya Warundi unahusu ni kwa namna gani maisha katika taarifa hiyo yangebadilika endapo ndoto ya Rwagasore na Nyerere ingetimia. Pengine, swali kubwa zaidi ni, kwa vipi siasa na maisha katika eneo la Maziwa Makuu zingekuwa kama ndoto hiyo ingetimia?

Tanganyika ilikuja kuungana na Zanzibar mwaka 1964 kuunda taifa la Tanzania lenye amani na utulivu lakini baada ya kifo cha Rwagasore, Burundi limekuwa taifa lililoshuhuhudia mauaji ya viongozi, vita vya wenyewe kwa wenyewe na taabu kwa raia wake kwa muda mrefu.

Mateso ya Warundi

Kupata picha ya mwananchi wa kawaida wa Burundi aliyezaliwa miaka 50 iliyopita, hakuna mfano mzuri kama niliowahi kuelezwa na mwandishi wa zamani wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Eric David Nampesya, miaka michache iliyopita.  

Nampesya aliyeripoti sana habari za wakimbizi wa vita za wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya kimbari katika miaka ya 1990, ana kisa cha mtu aliyekuwa tumboni mwa mamaye wakati mauaji dhidi ya Wahutu wa Burundi ya mwaka 1972 yalipoanza.

Wazazi wa mtoto huyo walikimbilia nchi jirani ya Rwanda na kuishi kama wakimbizi. Yeye alizaliwa huko lakini mwaka 1994, wakati mauaji ya kimbari yalipoanza nchini Rwanda, familia ilikimbia machafuko hayo kwenda kuishi – kwa mara nyingine kama wakimbizi, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

Wakati Laurent Kabila na waasi wa Banyamulenge walipoanza mapigano dhidi ya utawala wa Mobutu Sseseseko, ilibidi familia hiyo ya Warundi ikimbie tena kwa sababu ilikuwa hatari kwao kuwa mara nyingine. Hapo ndipo walipokimbilia katika mojawapo ya kambi za wakimbizi Tanzania – walipokutana na mwandishi huyo wa BBC. Hiyo ni stori ya familia moja lakini wapo Warundi wengi wanaoweza kusema wamepitia maisha ya namna hiyo katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

Mauaji na vita Burundi

Unaweza pia kusoma

Mwaka 1965, baba wa Rwagasore aliyekuwa pia Mfalme wa Burundi, Mwambutsa IV, alimteua Pierre Ngendandumwe, kuwa Waziri Mkuu kuchukua nafasi ya mwanawe aliyekuwa kipenzi cha Warundi. Siku nane tu baada ya kushika wadhifa huo kwa mara ya pili, Ngendandumwe aliuawa kwa kupigwa risasi na mkimbizi kutoka Rwanda.

Novemba mwaka 1965, mwanajeshi Michel Micombero alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoung’oa ufalme na kutangaza Katiba ya chama kimoja. Yeye naye alipinduliwa na Jean Baptiste Bagaza mwaka 1976. Ni utawala wa Micombero ndiyo uliokuwa madarakani wakati mauaji makubwa ya wananchi wa Burundi yaliyosababisha mamilioni ya watu kukimbia nchi yalitokea mwaka 1972.

Bagaza naye alipinduliwa na Pierre Buyoya mwaka 1987. Ni Buyoya ndiye aliyetawala hadi mwaka 1993, wakati Burundi ilipoitisha uchaguzi wake wa kwanza wa vyama vingi baada ya kurejeshwa kwa mfumo huo mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Maafa mengine yakatokea baada ya mshindi wa uchaguzi huo, Melchior Ndadaye, kuuawa takribani miezi mitatu tu baada ya kuingia madarakani.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo wa Burundi, Cyprien Ntaryamira, alipewa kiti cha urais kuchukua nafasi ya Ndadaye Februari mwaka 1994, lakini akauawa miezi miwili baadaye, Aprili 6, 1994, kwenye ajali ya ndege akiwa na Rais wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, wakati wakitoka Arusha kwenye mazungumzo ya kutafuta amani ya nchi yake. Nafasi yake ilikuja kujazwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la nchi hiyo, Sylvestre Ntibantunganya.

Kwenye mkutano mmoja na waandishi wa habari niliohudhuria wa aliyekuja kuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, mwaka 2004, kiongozi huyo alisema waliamua kuingia msituni na kufanya vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa vile ilionekana njia za kawaida za kidemokrasia zisingefaa.

Hatimaye Nkurunziza aliingia madarakani kidemokrasia na kuwa Rais wa taifa hilo kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2020 na ni utawala wake ndiyo uliorejesha amani Burundi kwa kipindi kirefu kuliko wakati mwingine wowote baada ya Uhuru. Baada ya kifo chake mwaka 2020, nafasi yake imechukuliwa na Evariste Ndayishimiye anayeongoza hadi sasa.

Kwanini Burundi na Tanganyika zilitaka kuungana?

Nyerere na Rwagasore walikuwa marafiki. Wote walikuwa watoto wa kichifu waliopata bahati ya kusoma ughaibuni. Wote pia waliamini katika Umajumui wa Afrika na walikuwa na rafiki mwingine wa pamoja – aliyekuwa Waziri Mkuu wa DRC, Patrice Lumumba. Nyerere – akiwatumia kisiri wanachama wa TANU kama Ali Mwinyi Tambwe, ndiyo waliokuwa wakisaidia kifedha chama cha rafikiye cha UPRONA kwenye harakati za kudai Uhuru wa Burundi.

Lakini urafiki wa Tanganyika na Burundi haukuanzia kwa Nyerere na Rwagasore. Kati ya Februari 27, 1885 hadi Novemba 25, 1918 yaani kwa takribani miaka 33– Tanganyika, Rwanda, Burundi na sehemu ndogo ya Msumbiji ziliwahi kuwa nchi moja chini ya ukoloni wa Ujerumani zikijulikana zote kwa jina la Deutsch-Ostafrika. Kwa hiyo walichotaka kufanya ni kurudi katika historia tu.

Nyerere pia, inajulikana, alikuwa amefanya mazungumzo na Rais Jomo Kenyatta wa Kenya, kuhusu uwezekano wa kuunda Serikali ya Muunganiko wa Kenya na Tanzania – yeye akikubali kumwachia Kenyatta nafasi ya urais. Ni wazi kuwa Nyerere na Rwagasore walikuwa na wazo la kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki miaka 60 iliyopita.

Pamoja na kutoungana kama ilivyokuwa ndoto zao, Tanzania na Burundi pengine ndiyo nchi zenye uhusiano wa kirafiki zaidi miongoni mwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki.

Ingawa bado taarifa hazijawekwa wazi, Nkurunziza alirudi madarakani kwa msaada wa Tanzania baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi dhidi yake mnamo Mei mwaka 2015.

Kwenye vikao vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Burundi na Tanzania hujulikana kwa kupiga kura ya Pamoja – vikao vya upatanishi vya Burundi viliongozwa kwanza na Watanzania chini ya Mwalimu Nyerere na Jaji Mark Bomani kabla ya kupokewa na Nelson Mandela mara baada ya kifo cha Mwalimu mwaka 1999.

Na ingawa hali inaonekana kutulia Burundi, ikiwa sasa bado inapambana na vikundi vya waasi wanaodaiwa kukimbilia ndani ya misitu ya DRC, inaonekana hali bado haijawa shwari kwa asilimia kubwa.

Na Burundi ina changamoto nyingine ambazo nchi nyingi za Afrika zinazo pia. Umasikini bado ni tatizo kubwa – ikitajwa kama nchi masikini zaidi duniani lakini ikiwa pia na tatizo la kuwa na idadi kubwa ya watu kulinganisha na eneo dogo la ardhi ililonalo. Wakati kwa wastani watu 67 hukaa katika kilomita moja ya mraba kwenye nchi za EAC, kwa Burundi wastani ni watu 135 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019.

Maandishi ya wanahistoria wa siasa za Afrika katika miaka ya 1960, yanaonyesha kwamba misukosuko iliyolikumba taifa hilo la pili kwa udogo miongoni mwa wanachama wa EAC – ikiwamo mauaji ya Rwagasore, lilisababishwa na woga wa nchi za kibeberu kwamba huenda Burundi ingetumiwa na Wakomunisti wa China au Urusi kama ngome ya kupinga uporaji na ubeberu ndani ya DRC.

Labda kwa Nyerere na Rwagasore, utulivu, maendeleo na amani ya Burundi ulikuwa ni muhimu kwa utulivu wa eneo zima la Maziwa Makuu. Pengine hili ni jambo la kuangaliwa kwa jicho makini na viongozi wa sasa wa nchi za EAC katika wakati ambapo masuala ya ulinzi na usalama yanalegalega kwenye eneo hili na duniani kwa ujumla. Hivi karibuni uhusiano wa Tanzania na Burundi umeimarika zaidi katika nyanja za siasa na uchumi.

Juhudi za kuziunganisha kwa kutumia reli ya kisasa kutoka Uvinza mkoani Kigoma mpaka Gitega -Bujumbura na mpaka wa Burundi na DRC kwenye mji wa Uvira zimeshika kasi. Kumekuwa na safari za kirafiki kati ya vyama tawala nchini Tanzania (CCM) na CNDD-FDD nchini Burundi ambapo makatibu wakuu wao wametembeleana mara mbili ndani ya mwezi mmoja uliopita.

Zipo taarifa kwamba wazo la kurudi katika ndoto ya waasisi wa mataifa hayo zimeanza kujadiliwa tena katika korido za Dodoma na Gitega. Je, marais Samia Suluhu Hassan na Evariste Ndayishimiye ndiyo hatimaye watatimiza ndoto za Mwalimu Nyerere na Mwana wa Mfalme Rwagasore? Wakati utasema. Heri ya Siku ya Kuzaliwa Burundi.