Gabriel Jesus: asajiliwa na Man City akitokea Palmeiras

Gabriel Jesus

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha,

Gabriel Jesus mchezaji mpya wa Manchester City

Matajiri wa Manchester City inaarifiwa wamemsajili winga kinda wa miaka 19 raia wa Brazili Gabriel Jesus anayetoka katika timu ya Palmeiras kwa gharama ya pauni milioni 27 .

Jesus amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano ingawa atasalia na timu yake ya Palmeiras mpaka hapo msimu wa ligi ya Brazili utakapokamilika mwezi December.

City wamemuelezea kinda huyo kama mchezaji kinda mwenye kipaji anayetokea Marekani ya Kusini na kwamba ameghairi nia yake ya kwenda Barcelona. Jesus alipigiwa kura ya kuwa mchezaji mchanga anayeinukia kwa kiwango cha hali ya juu miongoni mwa wachezaji nguli kutoka kwenye kikosi chake cha Brazili kuingia katika michuano ya Olimpik ya Rio .

Gabriel amefunga magoli 26 katika michezo 67 katika kikosi cha kwanza cha Palmeiras katika ligi kuu ya Brazil ingawa bado hajacheza katika kikosi cha kwanza cha wakubwa cha taifa lake .Kwa kuongezea tu kuhusiana na mkataba wake endapo atafanikiwa kufanya vizuri akiwa na Man City ambao wanautumia uwanja wa Etihad basi Gabriel ataongezewa kiasi cha pauni milioni nne .

Jesus amesema kwamba Man City imesheheni vipaji lukuki akiwemo meneja mahiri Pep Guardiola na kwamba atajifunza mengi kutoka kwao . Gabriel akaendelea kujinasibu kwa kusema kuwa atawaonesha mashabiki wa timu ya Man City kile atakachofanya na kwamba anatamategemeo ya kufikia malengo yake akiwa pamoja na Man City.

Jesus anao uwezo mkubwa wa kucheza namba zote za mbele iwe winga ya kushoto,kati,kulia ama hata mbele lakini pia atakuwa na mshambuliaji mpya wa kimataifa aliyesajiliwa na kocha Guardiola , Leroy Sane anayetokea Ujerumani kwa gharama ya pauni milioni 37 akitokea timu ya Schalke.Guardiola mpaka sasa ameshatumia kiasi cha pauni milioni mia moja kwa usajili wa wachezaji katika msimu ujao wa ligi ambao ni Ilkay Gundogan, Nolito, Oleksandr Zinchenko na Aaron Mooy.