Vita huenda vikazuka Sudan Kusini, msemaji wa Machar aonya

Mabior Garang de Mabior

Chanzo cha picha, Mabior Garang de Mabior / Facebook

Maelezo ya picha,

Bw Mabior Garang de Mabior na Dkt Riek Machar

Msemaji wa Dkt Riek Machar ameonya kuwa huenda Sudan Kusini ikatumbukia tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe iwapo Umoja wa Afrika hautaingilia kati.

Bw Mabior Garang de Mabior amesema wanajeshi waaminifu kwa Dkt Machar wako tayari kuingia mji mkuu wa Juba iwapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitaidhinisha pendekezo la Umoja wa Afrika la kutuma wanajeshi nchini humo.

Haijabainika iwapo Dkt Machar, mpinzani wa muda mrefu wa Rais Salva Kiir, ana wanajeshi wa kutosha wa kumuwezesha kujaribu kuingia Juba.

Tahadhari ya Bw Mabior imetolewa kufuatia hatua ya Rais Kiir ya kuwafuta kazi mawaziri sita wanaoegemea upande wa Dkt Machar.

Rais Kiir na Dkt Machar walikuwa wameunda serikali ya umoja wa kitaifa lakini ikavurugika baada ya vita kuzuka mjini Juba mwezi uliopita.

Dkt Machar, aliyekuwa makamu wa rais, aliondoka Juba na kufikia sasa hajulikani alipo.

Baadhi ya wanasiasa wa mrengo wake walikutana na kumuidhinisha Taban Deng Gai kuwa makamu mpya wa rais.

Hatua hiyo ilipingwa na wanasiasa watiifu kwa Dkt Machar.