Iran yawanyonga 'magaidi' 20

Afisa mmoja wa serikali ya Iran anaandaa kitanzi kabla ya kunyongwa kwa watu katika mji wa Noor (15 April 2014) Haki miliki ya picha AFP
Image caption Iran iliwanyonga takriban watu 1,000 mwaka uliopita kwa mujibu wa Amnesty international

Watu 20 wanaoushukiwa kuwa wanachama kwa kile utawala nchini Iran unakitaja kuwa kundi la kigaidi la Sunni wamenyongwa .

Mkuu wa mashtaka aliyenukuliwa akiongea na kituo komoja cha televisheni amesema kuwa watu hao walihusishwa na mauaji ya watu 20 kwa milipuko na mashambulizi mengine Magharibi mwa Iran.

Utawala unasema kuwa watu hao walikuwa sehemu ya kundi moja lenye siasa kali ambalo liliwaua viongozi wa Sunni mwaka 2009.

Vyombo vya habari vya dola vinawalaumu kwa mauaji ya wanawake na watoto kati ya mwaka wa 2009 na 2011.

Iran, ambayo inaidadi kubwa ya wa-Shia, inadaiwa kuwa imewanyonga takriban watu 977 mwaka uliopita kwa mujibu wa shirika la kupigania haki za kibinadamu la Amnesty International.

Mashirika ya kutete haki za kibinadamu yamefutilia mbali madai ya wahanga hao kusikizwa katika mahakama yakidai ilikuwa ni porojo tu.

Mashirika hayo yanamtaja Shahram Ahmadi, ambaye wanadai hukumu dhidi yake ilitolewa baada ya kupigwa na kulazimishwa kukiri makosa aliyodaiwa kufanya.

Mkuu wa mashtaka Mohammad Javad Montazeri amesema kuwa wakurdi hao walikuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Tawhid na Jihad.

China mwaka jana iliwanyonga takriban watu 1000.

Mataifa mengine yaliyowanyonga watu wengi ni Pakistan - 326 na Saudi Arabia iliyowatia kitanzi watu 158.