Msomali akamatwa kwa mauaji London

Msomali akamatwa kwa mauaji London Haki miliki ya picha PA
Image caption Msomali akamatwa kwa mauaji London

Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 19 raia wa Norway mwenye asili ya Kisomali, amekamatwa kwa kushukiwa kutekeleza tendo la kumdunga kisu mwanamke mmoja Mmarekani katikati mwa London.

Watu wengine watano walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Alhamis.

Waliojeruhiwa ni raia wa Uingereza, Marekani ,Israeli na Australia.

Polisi wamemtambua mwanamke aliyeuawa kuwa raia wa marekani na mwenye umri wa miaka 60.

Polisi wanasema kuwa, shambulio hilo la kisu huenda lilisababishwa na mtu aliyekuwa na msongo wa mawazo au matatizo ya akili.

Polisi wanasema kwamba, hakuna ushahidi wowote kwamba mshukiwa alikuwa amepata mafunzo ya itikadi kali au kuwa na uhusiano na mitandao wa wapiganaji wa Kiislamu kama vile kundi la Islamic State.

Image caption Polisi wanasema kwamba, hakuna ushahidi wowote kwamba mshukiwa alikuwa amepata mafunzo ya itikadi kali

Aidha wanasema pia taifa anakotoka mtu sio sababu hasa inayoweza kuwafanya au kuwachochea kushuku kuwa lilikuwa ni shambulizi la kigaidi.

Naibu Mkuu wa kitengo cha polisi wa mji wa London Metro Mark Rowley, amewaambia waandishi wa habari kuwa huenda kijana huyo alikuwa na matatizo ya kiakili.

Bwana Rowley alikuwa amewaambia waandishi wa habari kuwa wanachunguza tishio la ugaidi kama moja ya vyanzo vya mashambulizi hayo.