Tanzania kufungia Vyuo vya Ufundi kwa kukosa ubora

Vyuo vitano vimefungiwa nchini Tanzania
Maelezo ya picha,

Vyuo vitano vimefungiwa nchini Tanzania

Baadhi ya wamiliki na wadau wa elimu wamelalamikia Baraza la Elimu ya ufundi nchini Tanzania kuvifutia usajili vyuo vitano huku vingine arobaini na moja vikifungiwa kuendesha mafunzo.

Hata hivyo, Baraza hilo, limesema limelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya vyuo hivyo kushindwa kuwa na sifa stahiki za kuendelea kutoa mafunzo katika ubora unaohitajika.

Miongoni mwa vyuo vilivyoathiriwa na hatua hiyo ni Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi iliyopo jijini Mwanza ambapo Dr. CUthbert Nahonyo ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya ushauri katika Chuo hicho anakosoa hatua hiyo na kusema kuwa ni baraza lenyewe ndio lenye makosa kwa kuwa usajili wao uliisha tangu mwaka 2012 na wamekuwa wakifuatilia kupata usajili mpya kwa muda mrefu bila kupata majibu.

Ama kwa upande wa vyuo vilivyofutiwa usajili ni Chuo cha Zoom Polytechnic College kilichopo jijini Dar es Salaam ambapo mmiliki wa chuo hicho bwana Syeta Malimi anaona zoezi hilo limeharakishwa bila ya wao kushirikishwa.Japo kuwa NACTE waliwahi kuwatembelea na kuwataka waboreshe mazingira ya kusomea kama vile kuwa na maktaba na kukarabati jengo,lakini gharama ikawa kubwa hivyo wakaona ni bora kukiamisha chuo hicho katika eneo lingine ambalo wataweza kumudu gharama,na barua ya kutoa taarifa juu ya kuhama kwao rasmi tayari walishaituma baraza.

Pamoja na kwamba chuo hicho kimefutwa lakini BBC ilipokitembelea ilikuta wanafunzi wanaendelea na masomo yao kama kawaida, ingawa hawakuficha hisia zao juu ya kushtuliwa na taarifa za kufutwa kwa chuo chao hasa ikizingatiwa kwamba hatua hii imechukuliwa wakati ambapo baadhi ya wanafunzi walikuwa tayari washalipa ada na wengine wanakaribia kumaliza muda wao wa masomo, hivyo taarifa hiyo imewafanya kutojua mustakbali wao na hata wazazi wao watakuwa katika nafasi gani ya kuwasaidia kuendelea na masomo yao.

Maelezo ya picha,

Baadhi ya Wanafunzi wakiendelea na masomo

Utaratibu wa kawaida

Hata hivyo Baraza hili limesema,huu ni utaratibu ambao upo mara kwa mara ili kuboresha elimu ya ufundi nchini Tanzania. Twilumba Mpozi ni kaimu mkurugenzi wa usajili na ithibati ya vyuo anasema zoezi hili huwa linafanyika mara kwa mara haswa wakati huu wa usaili ili wanafunzi na wazazi waweze kujua vyuo ambavyo vimesajiliwa na vina ubora.

Na hatua hiyo imekuja baada ya kipindi cha miaka ya hivi karibuni nchini Tanzania, kumekuwa na utitiri wa vyuo ambavyo baadhi havikidhi kiwango, hivyo kushusha kiwango cha elimu.