Pagan Amum: Sudan Kusini yafaa ‘itawaliwe na UN’

Pagan Amum

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Pagan Amum wakati mmoja alikuwa rafiki mkubwa wa Rais Salva Kiir

Mwanasiasa mmoja mashuhuri nchini Sudan Kusini ameambia BBC kwamba taifa hilo linafaa kuwekwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa muda.

Pagan Amum, ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa chama tawala cha SPLM, amesema hatua kama hiyo inaweza kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kurejesha uthabiti nchini humo.

Amum, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni, amesema Umoja wa Mataifa unafaa kuunda serikali ya wataalamu wa Sudan Kusini.

Amesema bila hatua kuchukuliwa, taifa hilo limo hatarini ya kutumbukia kwenye vita vikali na vya kikatili vya kikabila.

Mwanasiasa huyo amesema vita hivyo huenda vikala vibaya zaidi kushinda vilivyoshuhudiwa Somalia.

Ijumaa, serikali ya Sudan Kusini ilikubali pendekezo la mataifa ya kanda la kutuma wanajeshi wa kulinda amani nchini humo.

Hata hivyo, serikali hiyo imepinga pendekezo lolote la usimamizi kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vilizuka tena Desemba 2013 kufuatia jaribio la kupindua serikali.

Mapigano yaliendelea hadi kutiwa saini kwa mkataba wa Amani Agosti mwaka jana.

Lakini katika miezi ya hivi karibuni, vita vimezuka upya na aliyekuwa makamu wa rais kuambatana na mkataba huo wa amani, Dkt Riek Machar, akaondoka mji mkuu Juba.