Maafisa 150 serikalini wahusishwa na mihadarati

Rodrigo Duterte akitaja majina ya maafisa wakuu wanaohusika na mihadarati

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Rais Duterte amesema kuwa atachukuwa lawama zote endapo yeyote aliyetajwa atapatikana bila makosa

Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, amewataja hadharani na kuwahusisha maafisa wakuu wa serikali yake na ile ya awali na mtandao mpana wa ulanguzi wa dawa za kulevya nchini humo.

Rais Rodrigo Duterte, amewataka wajisalimishe kwa idara ya usalama inayopamban na ulanguzi wa mihadarati la sivyo watachunguzwa.

Wakuu hao ni pamoja na mameya, wabunge na majaji wa taifa hilo.

Anasema wote hao wanahusika na biashara hiyo haramu.

Katika hotuba kwa taifa iliyopeperushwa moja kwa moja kwa runinga, Rais Duterte amewaomba wenyewe wajitokeze na kuingia korokoroni kabla hajawakamata.

Rais huyo alisoma majina yao moja baada ya mwengine na mara moja akaamrisha maafisa wanaowapa usalama wajiondoe mara moja.

''Wale watakaoonesha japo dalili ya kupinga kukamatwa ninawaamrisha polisi kuwafyatulia risasi papo kwa hapo'' aliongezea kiongozi huyo.

Rais huyo alitwaa mamlaka mwezi Juni mwaka huu huku akiapa kukabiliana vilivyo na tatizo la ulanguzi wa mihadarati.

Inaaminika kuwa mamia ya watu wanaoshukiwa kuhusika na biashara hiyo haramu wameuwawa na maafisa wa polisi katika siku za hivi karibuni.