Muhtasari: Habari kuu leo Jumatatu

Miongoni mwa habari nyingine kuu, Rais Erdogan amesema yuko tayari kurejesa adhabu ya kifo Uturuki, Waziri wa michezo Kenya Hassan Wario naye amelalamikia kutolewa kwa madai mapya kuhusu matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini.

1. Erdogan kurejesha adhabu ya kifo Uturuki

Maelezo ya picha,

Rais Erdogan amewaambia watu mjini Istanbul kuwa atapitisha sheria ya kifo kama italetwa tena na bunge la nchi hiyo.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amehutubia mkutano wa hadhara uliokuwa na zaidi ya watu milioni moja ulioitwa kukemea jaribio la mapinduzi la mwezi uliopita.

Aliuambia umati wa watu kwamba atarudisha tena hukumu ya kifo iwapo itaungwa mkono na bunge

Ujerumani imeonya kwamba kurudishwa kwa hukumu hiyo kutamaliza matumaini ya Uturuki kujiunga na muungano wa Ulaya.

2. Waziri wa Kenya atetea wanariadha Rio

Maelezo ya picha,

Bw Hassan Wario

Waziri wa michezo nchini Kenya Hassan Wario amesema kuwa kutolewa kwa kanda ya video inayomuhusisha meneja wa timu ya Kenya katika michezo ya Olimpiki na matumizi ya dawa za kusisimua misuli ni uovu.

Amesema kuwa kanda hiyo iliotolewa na kituo cha habari cha Ujerumani ARD inalenga kuwavunja motisha wanariadha wa Kenya.

Meja Michael Rotich ambaye alirekodiwa akiahidi kuwaonya wanariadha wa Kenya kuhusu ziara ya maafisa wa kukabiliana na dawa hizo na kutaka wapewe hongo, anarudi nyumbani.

3. Watu 38 wafariki maporomoko ya ardhi Mexico

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wanajeshi wamekuwa wakisaidia katika juhudi za uokoaji

Mamlaka nchini Mexico inasema kuwa watu 38 wameuawa na maporomoko pamoja na mafuriko yaliosababishwa na kimbunga kilichopiga taifa hilo siku ya Jumamosi.

Waathiriwa wengi walifariki baadaa matope kufunika makazi yao katika jimbo la Puebla.

4. Urusi yakerwa na marufuku Olimpiki ya walemavu

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Goncharova ni mmoja wa wanariadha wa kutegemewa wa Urusi

Urusi imeishtumu hatua ya Kamati ya kimataifa ya michezo ya watu Walemavu kupiga marufuku wanariadha wake katika michezo ya mwezi ujao ya Rio kutokana na madai kwamba serikali inawafadhili wachezaji wake kutumia dawa za kusisimua misuli.

5. Wanajeshi wa UN auawa Mali

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Umoja wa Mataifa ulituma wanajeshi Mali mwaka 2013

Wanajeshi walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali wanasema mmoja wao ameuawa na wengine wanne kujeruhiwa wakati gari lao liliposhambuliwa na kilipuzi.Mali limekuwa eneo hatari zaidi miongoni mwa vikosi vya umoja wa mataifa.

6. Deby kuapishwa kuhudumu muhula wa tano Chad

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais Deby alitangazwa mshindi akiwa na asilimia 62 ya kura

Vikosi vya usalama nchini Chad vimevunja maandamano ya upinzani katika mji mkuu wa Ndjamena kwa siku ya pili mfululizo.

Rais Idriss Deby ataapishwa kwa muhula wake wa tano baadaye hii leo.