Waziri: Mapenzi ya jinsia moja ni haramu Uganda

Simon Lokodo
Image caption Waziri wa maadili nchini Uganda Simon Lokodo

Waziri wa maadili nchini Uganda amesema kuwa shughuli zote za wapenzi wa jinsia moja ni haramu na kinyume na tamaduni za watu wa Uganda.

Simon Lokodo aliuambia mkutano wa waandishi habari kuwa shughuli za wapenzi wa jinsia moja haziruhusiwi kamwe Uganda.

Waziri huyo alikuwa akitoa sababu iliyosababisa polisi kupiga marufuku mkutano wa wapenzi wa jinsi moja katika klabu moja ya usiku mjini Kampala majuzi.

Mwanaharakati wa kupigania haki za wapenzi ya jinsia moja nchini Uganda anasema kuwa watu wenye wapenzi wa jinsia moja wanastahili kuendelea na shughuli zao ikiwa watahitaji kufanya hivyo.

Kupitia mtandao wake wa kijamii Frank Mugisha anasema kuwa ''jamii ya LGBT itaendelea kufanya mikutano yao kama inavyoruhusiwa kikatiba bila pingamizi lolote''

Lakini Waziri wa maadili nchini Uganda amesema kuwa serikali yake haitawafumbia macho wale wanaoshabikia wapenzi wa jinsia moja na kujaribu kusambaza harakati zao alizoita haramu nchini humo.

''Katika jamii yetu maswala ya ngono huwa ni ya siri mno, itakuwaje kuwa sasa maswala ya ngono yanawekewa gwaride ?''

''Tutapambana na mtu yeyote atakayejaribu kuchochea ama hata kufadhili na kupigia debe swala la wapenzi wa jinsia moja''

Padri Simon Lokodo aliiambia BBC kuwa serikali yake tayari imeunda mpango mahsusi wa kuwasaidia watu wa jamii hiyo ya LGBTI kujiunga upya na jamii.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Alahmisi usiku polisi walivunja tamasha la wanamitindo wa wapenzi ya watu wa jinsia moja na kushika baadhi yao.

Aidha aliongezea kuwa wale waliokuwa wanapanga Gay Pride parade mwishoni mwa juma kukomesha haraka harakati zao.

Alahmisi usiku polisi walivunja tamasha la wanamitindo wa wapenzi ya watu wa jinsia moja na kushika baadhi yao.

Waziri anasemakuwa shughuli hizo haziendani na sheria za Uganda kwani mikusanyiko yao haikukubaliwa na polisi.

Lakini mmoja wa waandalizi wa tamasha hizo Pepe Julian mapema aliiambia BBC kuwa kila kitu kitakuwa sawa kwani waliifahamisha vyombo vya usalama.

Mapenzi ya watu wa jinsia moja iliharamishwa nchini Uganda chini ya sheria za ukoloni katika kifungu kinachokataza mtu kufanya ngono kinyume na kawaida.