Gari lampeleka mmiliki hospitalini

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Gari aina ya Tesla

Wakili mmoja nchini Marekani Joshua Neally alipelekwa hospitalini na gari lake la umeme Tesla linalojiendesha baada ya mishipa ya damu kuganda na kumsababishia uchungu mwingi kifuani.

Neally anayemiliki gari aina ya Tesla X alikuwa akielekea nyumbani kwake katika mji wa Springfield, Missouri, akitokea Branson.

Hata hivyo wakili huyo alibanwa na uchungu mwingi sana kifuani na tumboni.

Kiunyume na matarajio ya wengi alihofia kuwa angalipiga simu ya gari la huduma ya kwanza ingelimchukua muda mrefu kupata matibabu na hata labda kufa kwa hivyo akaamua kubofya kifaa cha gari lake kinachoiwezesha kujiendesha kumpeleka hospitali iliyokaribu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Gari la Tesla linalojiendesha kama analomilika wakili Neally.

Na kwa takriban kilomita 32 hivi gari hilo aina ya Tesla Model X lilimpeleka wakili huyo mwenye umri wa miaka 37 hospitalini.

'Pulmonary embolism'' ama kuziba kwa mishipa ya damu mara nyingi husababisha maafa kwani moyo unashindwa kupitisha damu na hivyo mwili unakosa hewa.

Madakta walipigwa na butwaa alipoingia katika chumba cha wagonjwa mahututi mwenyewe.

Wanasema ilikuwa ni bahati kwake kujifikisha hospitalini katika hali hiyo.

Haki miliki ya picha Facebook/Neally Law
Image caption Wakili Joshua Neally

Gari hilo la kisasa linalotumia umeme na lenye uwezo wa kujiendesha limekumbwa na utata katika siku za hivi punde nchini Marekani baada yake kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Ajali ya hivi punde zaidi ilihusisha dereva wa gari hilo na lori.

Yamkini chombo cha gari hilo kinachoiwezesha kujiendesha kilifeli kutambua kuwepo kwa lori katika barabara yake na hivyo likahusika katika ajali ya ana kwa ana.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Tesla imemulikwa na vyombo vya usalama wa umma baada ya kuhusika katika ajali kadhaa katika siku za hivi punde

Watengenezaji wa gari hilo wanasema kuwa baadhi ya wamiliki wa magari hayo hawafahamu kulitumia vyema huku wengine wakitatizika kufuata maagizo rahisi ya jinsi ya kulimudu gari hilo wakati wamelikabidhi usukani wa kujiendesha lenyewe.

Teknolojia hiyo ya kujiendesha sasa inafanyiwa uchunguzi wa ubora na halmashauri ya usafiri wa magari barabarani.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kwa wakili huyo iliyomnusuru hata hivyo ni kifaa kilekile kinacholaumiwa na wengi.

Joshua Neally anasema gari hilo litaokoa maisha ya watu wengi.