Mwanaume ashikiliwa kwa kupanda uzio Buckingham Palace

Kasri ya Buckingham Palace

Chanzo cha picha, PA

Mwanamume mwenye umri wa miaka 22 ametiwa nguvuni baada ya kupanda uzio wa usalama kwenye kasri ya Buckingham Palace, kwa mujibu wa polisi.

Mwanamume huyo kutoka eneo la Croydon, kusini mwa mji wa London, alikamatwa saa za asubuhi alipoonwa na maafisa wa polisi waliokua wakifanya uchunguzi kwenye wa kamera za CCTV.

Alikamatwa saa kumi na robo alfajiri kabla ya kuingia ndani ya kasri.

Maafisa wa ulinzi wa kasri wamesema kuwa mtu huyo alikua amelewa na kwamba kitendo chake hakikufikiriwa kuwa na uhusiano na ugaidi .

Waliongeza kuwa mtu huyo hakua na silaha.

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha,

Michael Fagan alivamia na kuingia ndani ya kasri mnamo mwaka 1982 na kuzungumza na Malkia kwa muda wa dakika

Kwa sasa anashikiliwa katika kituo cha polisi mjini London.

Hakuna mtu yeyote wa familia ya kifalme aliekuwemo kwenye kasri wakati wa tukio hilo.

Msemaji wa kasri ya Buckingham Palace alikataa kutoa kauli yoyote kuhusu tukio hilo.

Kumekua na matukio kadhaa ya kuingia kwa nguvu ndani ya kasri, likiwemo tukio la mwaka mwaka jana ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 41 alikamatwa baada ya kuzima kwa king'ora kwenye kasri hilo .

Mwaka jana wanaume wawili walipanda hadi kwenye paa kama sehemu ya maandamano ya haki za akina baba huku mwaka 2013, mwanamume mmoja alifanikiwa kupanda uzio huo na kukamatwa ndani ya chumba ambacho kilikua wazi kwa ajili ya umma wakati wa mchana.

Tukio linalokumbukwa zaidi la uvamizi wa kasri ni la mwaka 1982 ambapo Michael Fagan aliingia chumbani kwa Malkia na kukaa kwa muda wa dakika 10 akizungumza nae hadi pale Malkia alipoweza kupiga king'ora Falgan alipoomba sigara.