Ugaidi: Sheria kali Ujerumani ikilenga wageni

Mwanamke aliyevalia burka Haki miliki ya picha Associated Press
Image caption Ujerumani inapania kuipiga marufuku vazi la kiislamu la wanawake la burka

Serikali ya Ujerumani inapania kuidhinisha sheria kali itakayopiga marufuku wanawake waislamu kuvalia nguo inayofunika nyuso zao ili kukabiliana na tishio la ugaidi.

Waziri wa usalama wa ndani ataidhinisha sheria hizo miongoni mwa zingine zinazolenga kukabiliana na tishio la ugaidi baada ya matukio kadha ya ugaidi nchini humo.

Waziri Thomas de Maiziere pia amependekeza kurahisisha sheria zitakazowezesha utawala kuwafurusha wageni pindi wanapowashuku kushiriki njama za ugaidi mbali na kuwezesha polisi na madaktari kubadilishana habari kuhusu washukiwa.

Waziri huyo vilevile amepanga kuwasilisha masharti mengine makali Alhamisi yanayolenga kukabili tishio la kigaidi.

Kumetokea visa kadhaa vya ugaidi nchini Ujerumani zingine zikihusishwa na kundi la wanamgambo wa Islamic Sate.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri wa usalama wa ndani Thomas de Maiziere

Vazi la Burka ni moja kati ya nguzo za dini za kiislamu inayowataka wanawake wajifunike mwili mzima ila viganja vya mkononi.

Hata hivyo sio wanawake wengi wanayoivalia nchini Ujerumani.

Ujerumani haina vikwazo dhidi ya mavazi na inatazamwa kuwa moja ya mataifa yenye uhuru wa mavazi.

Miaka mitatu iliyopita kamati maalum ya bunge iliyokuwa ikichunguza uhalali wa mapendekezo ya kupiga marufuku vazi la Niqab au Burka miongoni mwa wanawake waislamu iliamua kuwa kufanya hivyo ingehujumu khaki zao na kuwa ingekuwa kinyume cha katiba.

Hata hivyo ni kamati hiyo iliruhusu marufuku ya vazi hilo katika viwanja vya michezo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Polisi watapewa mamlaka ya kushika doria katika vituo vya usafiri

Hii haitakuwa marufuku ya kwanza barani ulaya kwa vazi hilo, Ni marufuku kuvalia burka Ufaransa Ubeljiji na miji kadha nchini Italia.

Waziri Maiziere anatarajiwa kuwaunga mkono mawaziri wanaoegemea upande wa chama cha Christian Democrat na Bavarian wanaopendekeza sheria kali dhidi ya wahamiaji.

Baadhi ya mapendekezo yao ni

  • Marufuku ya burka
  • Marufuku ya uraia wa mataifa mawili kwa Wajerumani wanaoshukiwa kuwa magaidi
  • Uajiri wa maafisa zaidi 15,000 kufikia 2020
  • Kuwatumia polisi kushika doria katika vituo vya usafiri
  • Kuzuia fedha za ugaidi kufadhili misikiti
  • Kufurusha wahubiri wanaounga mkono ugaidi

Mapendekezo hayo yanatarajiwa kujumuisha kufukuzwa kwa waalifu kutoka nchini humo na matumizi ya juu ya kamera za cctv.

Wito umekuwa ukitolewa kwa utala kupiga marufuku uraia mara mbili.

Naibu mkuu wa ujasusi katika mji wa Bavaria ameiambia BBC kuwa hatari ya kutokea shambulizi nchini Ujerumani ni ya juu.