Guinea: Wanawake wajawazito hukwepa hospitali wakihofia Ebola

TAMASIN FORD

Chanzo cha picha, TAMASIN FORD

Maelezo ya picha,

TAMASIN FORD

Guinea imekuwa huru na ugonjwa wa Ebola tangu mwezi Juni. Lakini wanawake wajawazito badio wanaogopa virusi vya ugonjwa huo , wakiepuka hospitali na kujifungua peke yao, ameandika mwandishi wa BBC Tamasin Ford.

Mamanata Soumah aliniambia kuwa hajawahi kumuona mkunga, muuguzi wala wakati wote wa ujauzito wake. Na ingawa anaingia siku ya tatu ya uchungu wa mimba bila kupata dawa za kupunguza maumivu, amekataa kuhudumiwa na mtu yeyote.

Nilimuuliza ni kwa nini.

"Niliogopa ebola," alisema.

Hii ilikua mwezi wa Machi. Miezi mitano baada ya eneo hili kutangazwa kuwa halina Ebola.

"Sikua na moyo wa kwenda kufanyiwa uchunguzi kwenye klinikikwasababu watu wengi hufa," alisema.

Bi Soumah aliniambia anamuhisi mtoto tumboni.

"Mtoto amechoka sana," Alisema huku akionekana kuwa mwenye wasi wasi .

"Alizaliwa akiwa amekufa."

Si mwanamke pekee mjamzito ambae anaogopa sana kwenda hospitalini.

Zaidi ya wanawake sita , wameshikilia watoto wao wachanga kwenye mapaja yao, wakisubiri nje ya ofisi ya mkuu wa kijiji cha Kalemodiagbe kusungumza name.

Mmoja wao alikua wifi yake Bi Soumah. M'mah Camara bado anakataa kumpeleka mwanae hospitalini kupata chanjo.

Sawa na Bi Soumah, pia alikaa siku tatu nyumbani alipokuwa na uchungu wa mimba, akikataa kumuona daktari wala mkunga.

Lakini tofauti na Bi Soumah, mwanae alinusurika.

Chanzo cha picha, TAMASIN FORD

Maelezo ya picha,

M'mah Camara alikataa kuhudumiwa na mkunga katika siku tatu za uchungu wa mimba

Alimfunga taratibu taulo yake ya kijani mwanae mchanga wa miezi miwili.

Akiwa na umri wa miaka 27 aliwapoteza jamaa 13 wa familia yake kutokana na Ebola, akiwemo mumewe.

Baada ya kufa, kulingana na mila za eneo hilo, aliolewa na kaka yake ambaye ni baba ya mtoto wake .

"Wakati wa mlipuko wa Ebola watu walikwenda kliniki lakini hawakuwahi kamwe kurudi. Ninahofu kwenda huko huenda," Alisema.

Huu ndio mtazamo wa akina mama wengine na wanawake wajawazito katika kijiji hiki, wanasema alieondoka wakati wa Ebola kwenda hospitalini , kliniki ama kutuo cha afya hakurudi.

Katika kijiji hiki pekee watu 43 walifariki dunia kwa maradhi ya Ebola.