Muhtasari: Habari kuu leo Ijumaa

Miongoni mwa habari kuu leo, kocha wa Kenya ametimuliwa kutoka Olimpiki Rio, kukaripotiwa visa vya Polio Nigeria na Fiji wakatwaa dhahabu raga Rio.

1. Kocha wa Kenya atimuliwa kutoka Rio

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanariadha Ferguson Rotich

Kocha wa Kenya anayesimamia wanariadha wa mbio fupi katika kikosi cha Kenya kilichopo mjini Rio de Janeiro amerudishwa nyumbani kwa udanganyifu.

John Anzrah ameshtumiwa kwa kujifanya kuwa mwanariadha Furguson Rotich kwa kutoa sampuli ya mikojo badala yake.

Afisa mkuu wa michezo ya Olimpiki nchini Kenya Kipchoge Keino amesema kuwa shirika lake haliwezi kuvumilia tabia kama hiyo.

2. Visa viwili vya Polio vyaripotiwa Nigeria

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha,

Polio huzuiwa kupitia chanjo

Taifa la Nigeria limeripoti visa viwili vya ugonjwa wa Polio,ikiwa ni visa vya kwanza katika kipindi cha miaka miwili iliopita.

Mlipuko wa ugonjwa huo, umeripotiwa katika jimbo la kaskazini la Borno ambapo kundi la boko haram linafanya operesheni zake.

3. Venezuela na Colombia kufungua mpaka

Chanzo cha picha, AFP

Mataifa ya Venezuela na Colombia yamekubali kufungua baadhi ya sehemu za mpaka wao.

Kuanzia Jumamosi watu wanaotembea kwa miguu wataweza kutumia sehemu walizotengewa kuvuka.

Venezuela ilifunga mpaka wake mwaka mmoja uliopita kutokana na sababu za kiusalama.

4. FBI yasema ilisaidia Canada kuzuia shambulio

Chanzo cha picha, Reuters

Shirika la kijasusi la FBI linasema kuwa liliwapatia maafisa wa polisi wa Canada, habari zilizozuia shambulio la kujitolea mhanga katika eneo moja la mjini lililo na watu wengi.

Aaron Driver alipigwa risasi na polisi akiwa katika hatua ya mwisho ya kujiandaa kutekeleza shambulio na bomu lililotengezwa nyumbani.

5. Papa wanaoishi muda mrefu zaidi

Chanzo cha picha, JULIUS NELSEN

Utafiti mpya unaonyesha kuwa papa wanaoishi katika sehemu za Greenland wanaishi muda mrefu zaidi ya mnyama yeyote yule aliye na uti wa mgongo, wakifikisha hadi umri wa miaka 400.

Sayansi ya kubaini umri imegundua kuwa wanyama hao huishi zaidi ya wanyama wanaoishi kwa miaka 100 kama vile baadhi ya kobe, nyangumi na binadamu.

6. Fiji yajishindia nafasi ya kwanza Olimpiki

Taifa la Fiji limeshinda medali yake ya kwanza katika michezo ya Olimpiki ikiwa ile ya dhahabu kwa kuishinda Uingereza katika fainali za michuano ya mchezo wa raga wa watu saba kila upande.

Waziri mkuu wa taifa hilo Frank Baini-Marama amesema kuwa ni wakati mzuri katika historia ya taifa hilo.