Wakuu wa Republican wataka chama kikate udhamini kwa Trump

Donald Trump Haki miliki ya picha AFP
Image caption Donald Trump anasema hajali kwamba chama cha Republican kitakata udhamini wa kampeni zake.

Zaidi ya wakuu 70 wa chama cha Republican wamesaini barua na kuituma kwa mkuu wa kamati ya kitaifa ya chama hicho wakimtaka aache kusaidia kampeni za Donald Trump.Wamesema "ubaguzi " na " uwezo mdogo" unakiweka chama katika hatari kushindwa katika uchaguzi wa Novemba.

Barua ilisema kwamba badala yake chama kinapaswa kuelekeza juhudi zake katika kuwalinda wagombea katika uchaguzi wa seneti na baraza la wawakilishi.

Wajumbe wa zamani wa baraza la Congress ni miongoni mwa wale waliosaini barua hiyo.

''Tunaamini kwamba kauli za kugawanya watu, uropokaji, ukosefu wa uwezo na kuvunja rekodi ya mgombea asiye maarufu vinaweza kuitia demokrasia hatarini ," ilieleza barua hiyo.

Akijibu kuhusu hatua ya barua hiyo , Bw Trump amesema kuwa hajali kwamba chama kinaweza kukata msaada kwake .

"kile ninachoweza kufanya ni kusitisha udhamini wangu kwa chama cha Republican " alisema bilionea huyo.

Lakini je ni yapi matumaini kwa wasiompenda Trump katika Republican?

  • Tumaini la kujiuzulu: Iwapo Trump ataamua kujiondoa mwenyewe itakua njia rahisi ya kupata mtu atakaechukua nafasi yake kama mgombea, lakini si rahisi achukue uamuzi huo .
  • Uwezekano mwingine ni kumtafuta mgombea mwingine: Bila Bw Trump kuondoka kwenye kinyang'anyiro hicho, kumuweka mtu mwingine haiwezekani chini ya sheria za chama.Baadhi wanafikiria kumuidhinisha mgomea mwenye msimamo huru Gary Johnson, lakini hili linaweza kuleta mgawanyiko wa kura za chama.
  • Suala jingine ni kumlazimisha aondoke kwa kutumia sheria ya siri: baadhi wanafikiria kumtangaza Bwa Trump "kama mtu mwenye matatizo ya kiakili ", chini ya kanuni ya kamati ya kitaifa ya Republican ambayo haijawahi kutumiwa.Lakini hii itakua hatua ngumu kwasababu huwezi kumuita mtu aliechaguliwa na watu zaidi ya milioni 10 asiye na uwezo wa kiakili.
  • Kukaa na kusubiri: Baadhi ya wanachama wa Republican ambao hawajaathiriwa wanadhani njia bora tu ni kumpinga Bw Trump na kusubiri watakapopata mgombea bora.