Madaktari wa Afrika Mashariki kupata ujuzi wa saratani Uingereza

Saratani ya matiti Haki miliki ya picha SCIENCE PHOTO LIBRARY
Image caption Madaktari watapata ujuzi wa kung'amua mapema maradhi ya saratani na kuyashughulikia ipasavyo

Madaktari 600 wanaofanyia kazi katika nchi za Afrika mashariki watapata mafunzo maalum juu ya saratani na magonjwa mishipa mjini London kwa kipindi cha miaka minne .

Hii ni sehemu ya mpango ulioandaliwa na taasisi Uingereza ya British Council kwa ushirikiano na chuo cha kitabibu cha Uingereza cha Royal School of Physicians, serikali za Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda, na kudhaminiwa na benki ya maendelea ya Afrika mashariki.

Mradi huo unalenga kuongeza idadi ya madaktari wanaoweza kushughulikia visa vya saratani vinavyoendelea kuongezeka.

Nchini kenya pekee, takriban watu 28,000 hupatikana na maradhi ya saratani kila mwaka.

Wengi wao hutambua kuwa wana ugonjwa huo wakati ukiwa umefikia kiwango cha juu.

Lakini mpango huu mpya ulioanzishwa kwa madaktari unatarajiwa kuongeza idadi ya madaktari wenye ujuzi wa kung'amua mapema maradhi ya saratani na kuwahudumia ipasavyo.

Madaktari hao 600 watachaguliwa kutoka hospitali za serikali zanye ukosefu wa madaktari bingwa na ambazo ziko mbali na miji.

Baada ya mafunzo madaktari hao watatakiwa kuhakikisha wanarejea kwenye hospitali walikoajiriwa na kufanya kazi kwa walau miaka mitano.

Mara kwa mara wagonjwa wengi wa saratani katika kanda ya Afrika mashariki hulazimika husafiri nje ya nchi kwa matibabu kutokana na ukosefu wa ujuzi muhimu wa kitabibu, ukosefu wa teknolojia na dawa.