Washukiwa watatu wa ugaidi wauawa Rwanda

Msemaji wa polisi wa Rwanda Celestin Twahirwa
Image caption Msemaji wa polisi wa Rwanda Celestin Twahirwa

Washukiwa wengine watatu wa ugaidi wamepigwa risasi na kuuawa na polisi leo asubuhi katika eneo la Bugarama kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Hiyo inafikiwa wanne, idadi ya washukiwa waliouawa katika kipindi cha siku mbili baada ya kuhusishwa na ugaidi nchini humo.

Mkuu wa polisi katika eneo hilo Sano Nkeramugaba amethibitisha tukio hilo kwa vyombo vya habari.

"Washukiwa walikuwa 6, wavulana na msichana mmoja. Walikuja hapa Bugarama kufundisha maadili ya Kiislamu. Tulipotaka kuwakamata, baadhi wametaka kukimbia tukawapiga risasi," amesema.

"Watatu walifariki dunia papo hapo, mmoja amejeruhiwa na wengine wawili tuliwakamata."

Ameongeza kusema kwamba wamekiri kuhusika na kundi la Al Shabaab.

Polisi wamesema washukiwa sio watu wa eneo hilo na badala yake ni kutoka maeneo mbali mbali ya nchini Rwanda.

Usiku wa kuamkia jana polisi walimpiga risasi na kumuuwa mtu mwingine mjini Kigali aliyefahamika kwa jina la Shanny Mbonigaba baada ya kufyatuliana risasi na kumjeruhi polisi mmoja.

Hayo yanajiri wakati watu wengine 23, wote Waislamu, wanakabiliwa na kesi mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na kundi la kigaidi la Islamic State linalopigana vita nchini Syria.

Baadhi wanakana tuhuma hizo wakisema walipandikiziwa kesi kutokana na mgogoro wa ndani baina yao na wakuu wa dini ya kiislamu nchini Rwanda.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii