Raia wa Zimbabwe waandamana Kenya

Waandamanaji wanataka mabadiliko ya uongozi nchini Zimbabwe.
Image caption Waandamanaji wanataka mabadiliko ya uongozi nchini Zimbabwe.

Raia wa Zimbabwe wanaoishi nchini Kenya wameandamana jijini Nairobi, wakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi nchini Zimbabwe, na viwango vya juu vya ufisadi.

Waandamanaji hao wanataka mabadiliko ya uongozi nchini Zimbabwe.

Waandamanaji hao pia wameanza kampeni mitandaoni wakitumia #thisflag, wakimtaka rais Robert Mugabe ajiuzulu.

Mugabe mwenye umri wa miaka 92 amekana uwezekano wowote wa kuondoka madarakani.

Image caption Raia wa Zimbabwe waandamana nchini Kenya

"Nia yetu ni kuhamasisha ulimwengu kuhusu ufisadi unaoendelea nchini Zimbabwe, chini ya uongozi wa Rais Robert Mugabe". Anasema Reginald kadzutu, raia wa zimbabwe anayeishi mjini Nairobi.

Waandamanaji hao pia wanalenga kuhamasisha mashirika ya kimataifa ya kifedha kukatiza uhusiano wao na taifa hilo, wakisema pesa wanazotoa hazitumiki kwa manufaa ya raia wanaokumbwa na hali ngumu ya maisha.

"Tunataka pia kuwasilisha maombi yetu kwa mabalozi wa mataifa tajiri yanayofadhili Zimbabwe kukata uhusiano wao, hadi mabadiliko yaafikiwe". Kadzutu anasema.

Haya yanajiri huku taifa hilo likikabiliwa na matatizo chungu nzima ambapo Inakadiriwa kuwa watu milioni tatu nchini humo wanakabiliwa na baa la njaa kufuatia ukame uliosababisha mifugo elfu 20,000 kufa.

Maandamano makubwa yalifanyika nchini Zimbabwe yakiongozwa na Mchungaji Evan Mawarire aliyewahimiza Wazimbabwe kupitia mitandao ya kijamii kupambana na vitendo vya rushwa pamoja na ukosefu wa ajira.

Image caption Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe

Robert Mugabe ndiye rais mwenye umri mkubwa zaidi barani Afrika na amekuwa akiiongoza Zimbabwe tangu ijinyakulie uhuru wake mwaka wa 1980.

Uchaguzi mkuu ujao nchini Zimbabwe umeratibiwa kufanyika mwaka wa 2018.