Je,kuwa karibu na mgodi ni neema au la?

Moja ya Nyumba iliyojengwa na Mgodi wa Buzwagi
Image caption Moja ya Nyumba zilizojengwa na Mgodi wa Buzwagi kama fidia kwa mkazi wa eneo hilo

Baadhi ya raia nchini Tanzania ambao wanaishi katika maeneo ya migodi,wanalalamikia fidia wanayopewa kutoka kwa wawekezaji, na kudai kuwa hailingani na ardhi iliyochukuliwa.

Miongoni mwa migodi hiyo ni Accacia-Buzwagi ulioko kaskazini magharibi mwa Tanzania ambapo viongozi wake wanaeleza kuwa wamekuwa wakijihusisha na shughuli za miradi ya kimaendelo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, hospitali, shule na kulipa kodi inayotumiwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Image caption Baadhi ya Wananchi wa Mwendakulima wakiwa kwenye kituo cha afya

Lakini pamoja na shughuli zote hizo kufanyika katika eneo hilo bado baadhi ya wananchi wanaozunguka mgodi huo wanalalamikia uwepo wa mgodi huo katika kijiji chao.

''..Nina majuto kwanini nimezaliwa Tanzania na kwanini nizaliwe karibu na mgodi hapa Mwendakulima? Kwa sababu mpaka sasa tunapata shida kupata maeneo ya kulima, kwa mfano baba yangu alilipwa milioni saba kwa ekali 23, na ilikuwa mwaka 2008 hivyo, mimi kama mimi siwezi kusema kwamba tumenufaika na mgodi huu kwasababu bado nina maumivu..'' Anasema Simon Mabumba.

Pius Mpundi, Mwanasheria kutoka Shirika la kutetea haki za Binadamu "SHIHUDA" anaona kwamba malipo waliyopewa wananchi hawa si ya haki. Kwa kuwa Buzwagi imewafidia kwa kuwajengea nyumba za chumba kimoja, alichofananisha sawa na Msalani. Akisema kuwa maendeleo ya mji huo, hayalingani na faida ambayo mgodi huu wanaupata.

Image caption Miongoni mwa nyumba zinazojengwa kama fidia na mgodi wa Buzwagi

Kwa upande wake, Vicent Ndesekio, Afisa kata wa eneo hilo anasema licha ya Mgodi huo kuwajengea wananchi nyumba nzuri tofauti na walizokuwa nazo awali, bado hawaridhiki.

Amesema kwa sasa wanachofanya ni kubadili mtazamo kwamba mgodi unawajibika kuwafanyia kila kitu, kwani nao pia wanapaswa kujiajiri ili waweze kujitegemea.

Image caption Shule ya msingi ya Mwendakulima iliyojengwa na mgodi wa Buzwagi

Asa mwaipopo,Meneja mkuu katika mgodi wa Buzwagi, anasema upande wao wamefata utaratibu wote wa kisheria.

''...Ni kweli kwamba mgodi huu ulipoanza kujengwa ulichukuwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na wenyeji. Utaratibu wa fidia ni utaratibu wa kiserikali na ni utaratibu wa kisheria. Ukiwa unafanya kazi na watu wengi kiasi uelewa na tafsiri hutofautiana, lakini utaratibu ulizingatia sheria na taratibu na ulizingatia soko ndio maana wengi waliridhika na wakalipwa. Na kama wangekuwa na madai ya msingi sidhani kama suala hili lingechukua miaka mingi kama hivi...''.