Muhtasari: Habari kuu leo Jumanne

Miongoni wa habari kuu leo, wapiganaji wanaotoka Uturuki wanajiandaa kuingia Syria kukabili IS, John Kerry anaanza ziara Nigeria na wanafunzi Texas wana uhuru kukaa na bunduki.

1. Wapiganaji kutoka Uturuki kukabili IS Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia wakitoroka mapigano mji wa Manbij

Operesheni moja kubwa ya kuwafurusha wapiganaji wa Islamic State kutoka mji wa Jarablus mpakani mwa Syria, inaonekana kushika kasi.

Mwaandishi wa BBC aliyepo kusini mwa Uturuki, anasema kuwa waasi wa Syria wapatao 1,500 wanaoungwa mkono na Uturuki, wamekusanyika huko tayari kuvuka mpaka na kuanzisha mashambulizi. Jumatatu usiku, kikosi cha ulipuaji cha Uturuki, kilirusha makombora kulenga maskani ya Islamic State mjini humo. Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uturuki, amesema kuwa kundi la IS linafaa kusambaratishwa kabisa, kutoka kaskazini mwa Syria.

2. ANC yashindwa uchaguzi wa meya Johannesburg

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Ni mara ya kwanza kwa ANC kushindwa Johannesburg tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi

Chama tawala nchini Afrika kusini ANC kimepoteza udhibiti katika mojawepo ya mijiji mikuu zaidi nchini humo, Johannesburg, kwa mara ya kwanza tangu kuangushwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi miaka 20 iliyopita.

Herman Mashamba anayetoka katika chama cha upinzani cha Democratic Alliance, amechaguliwa kuwa meya mpya. Bwana Mashamba ameahidi kubadilisha utawala wa jiji.

3. Kerry kuanza ziara rasmi Nigeria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption John Kerry amemaliza ziara yake nchini Kenya

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry leo Jumanne anaanza rasmi ziara yake ya siku mbili nchini Nigeria.

Masuala ya usalama na ufisadi yanatazamiwa kutawala mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari mjini Abuja.

Ziara ya Bwana Kerry, inatazamiwa kufufua tena uhusiano kati ya Marekani na Nigeria, ambao uliyumbayumba wakati wa utawala wa Rais Goodluck Jonathan. Jonathan alikasirishwa na Washington, baada ya kukataa kumuuzia silaha, ili kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram.

4. Watu 40 walazwa baada ya mkasa kiwandani Bangladesh

Haki miliki ya picha AFP

Zaidi ya watu 40 wamelazwa Hospitalini nchini Bangladesh, baada ya kuvuja kwa gesi katika kiwanda kimoja cha utengezaji mbolea, katika mji wa Chittagong. Waliojeruhiwa wana matatizo ya kupumua baada ya kuvuta hewa ya kemikali kali iitwayo diammonium phosphate.

Watu wanaoishi viungani mwa kiwanda hicho, wameondolewa na kuhamishiwa maeneo salama.

Maafisa wa idara ya kuzima moto wanaendelea na kazi ya kuzuia kuvuja zaidi kwa gesi hiyo.

5. Wanafunzi kuingia na bunduki darasani Texas

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sheria hiyo ilianza kutekelezwa tarehe 1 Agosti

Wahadhiri watatu wa chuo kikuu cha Texas nchini Marekani, wameshindwa kuzuia sheria mpya inayowakubalia wanafunzi kuingia darasani wakiwa na bunduki.

Jaji mmoja katika mji wa Austin alipuuzilia mbali madai ya waathiri hao, akisema kuwa madai yao hayana msingi wowote kwani hamna hatari katika ubebaji wa silaha ikiwa hakutakuwa na malumbano makali darasani.

Kwa miaka 20 iliyopita, Jimbo la Texas limekuwa likiwakubalia watu kubeba bastola zao, lakini sheria mpya iliyoanza kutumika majuma matatu yaliyopita, kumekuwepo na vikwazo kwa wanafunzi.

6. Mwogeleaji wa Marekani Ryan Lochte apoteza udhamini

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ryan Lochte ni miongoni mwa waogeleaji wanne waliohadaa kuhusu kisa cha wizi Rio

Na Muogeleaji wa Marekani, Ryan Lochte, amepoteza nne kati ya mikataba ya wadhamini wake wakuu, baada ya yeye na wenzake watatu kutoa madai ya uongo kuhusiana na kuvamiwa na kuibiwa na wezi waliokuwa na silaha wakati wa mashindano ya Olimpiki mjini Rio De Jeneiro.

Kampuni ya uundaji mavazi ya kuogelea, Speedo, ilikuwa ya kwanza kufuta mkataba, ikafuatiwa na Kampuni ya Ralph Lauren; kampuni inayotengeneza mafuta ya kujipaka, kisha ile ya Syneron-Candela kisha waundaji wa mto wa kulalia, Airweave.