Wanafunzi kuingia na bunduki darasani Texas, Marekani

Wanafunzi wa chuo Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanafunzi waliotimiza miaka 21 wanaweza kuingia na bunduki darasani iwapo wana leseni ya kumiliki bunduki

Wanafunzi wa vyuo katika jimbo la Texas, Marekani wameruhusiwa kuingia na bunduki darasani.

Hii ni baada ya maprofesa wawili kushindwa kwenye ombi lao la kutaka mahakama izuiwe kutekelezwa kwa sheria mpya inayowaruhusu wanafunzi kubeba bunduki bila kuzionyesha hadharani.

Jaji katika mji wa Austin alipuuzilia mbali madai ya wahadhiri hao kwamba kuwepo kwa bunduki huenda kukawa hatari kubwa iwapo mjadala mkali utazuka darasani.

Mwanasheria mkuu wa Texas, Ken Paxton, ambaye ni wa chama cha Republican, aliunga mkono uamuzi wa jaji.

Alisema raia wanaotii sheria wana haki ya kujilinda hata wakiwa kwenye vyuo vikuu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Baadhi ya watu wanaamini sheria hiyo huenda ikasababisha mauaji zaidi

Chama cha Republican kinaamini kutekelezwa kwa sheria hiyo kunaweza kuzuia visa vya watu kuuawa kwa wingi na watu wenye bunduki kwa sababu wanaweza wakajilinda.

Jimbo la Texas lilipitisha sheria ya kuwaruhusu raia kubeba bunduki bila kuzionyesha hadharani miaka 20 iliyopita ingawa watu hawakuruhusiwa kuingia nazo vyuoni.

Hilo lilibadilishwa wiki tatu zilizopita kupitia marekebisho ya sheria.