Muhtasari: Habari kuu leo Jumatano

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, kumetokea tetemeko la ardhi Italia na FBI wanachunguza madai kwamba Urusi imehusika kudukua mitandao ya wanahabari Marekani.

1. Tetemeko la ardhi latokea katikati mwa Italia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Majumba mengi yameporoka katika miji iliyo eneo la Umbria

Kumetokea tetemeko la ardhi katikati mwa Italia karibu na mji wa Perushia.

Meya wa mji wa Amatrice, ulioko karibu na hapo, ameiambia Runinga ya Italia kuwa majumba kadhaa yameporomoka, huku watu wakikwama chini ya vifusi. Anasema kuwa nusu ya majengo katika mji huo yamebomolewa kabisa.

Uzito wa tetemeko hilo ulifikia 6 nukta 2 katika vipimo vya Richter na likasikika hadi katika miji ya Rome na Venice.

2. FBI yachunguza madai ya udukuzi wa vyombo vya habari

Haki miliki ya picha Getty Images

Idara ya upelelezi nchini Marekani, FBI, inachunguza ripoti ya makosa ya kimitandao baada ya wadukuzi kuvamia mitandao ya habari nchini Marekani, likiwemo gazeti maarufu la New York Times.

Maafisa wakuu nchini Marekani, wanasema kuwa wapelelezi wanachunguza uhusiano uliopo kati ya wadukuzi hao na idara ya ujasusi ya Urusi.

3. Korea Kaskazini yarusha kombora kutoka kwa nyambizi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kombora hilo limeanguka maeneo ya bahari ya Japan

Kwa mara nyingine tena Korea Kaskazini imerusha kombora hatari kutoka kwa nyambizi, na kukiuka marufuku ya kimataifa.

Duru kutoka kwa jeshi la Marekani, zinasema kuwa walifuatilia kombora hilo na kusema lilisafiri kwa kilomita 500, kabla ya kuanguka katika maeneo ya bahari ya Japan.

Uzinduzi huo umefanyika huku mawaziri wa maswala ya nchi za nje kutoka Japan, China na Korea Kusini wakikutana mjini Tokyo.

4. Kofi Annan kuongoza tume ya mapatano Myanmar

Haki miliki ya picha SIMON MAINA

Aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan, ataongoza tume iliyobuniwa kuchunguza namna ya kumaliza ghasia katika jimbo la Rakhine, nchini Myanmar.

Uamuzi huo wa serikali wa kumteua Bw Annan, unaonesha bayana kuwa kiongozi mkuu wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, yuko radhi kusikiliza mawazo mapya ya kutatua mzozo huo.

5. Milipuko miwili yatokea hotelini Thailand

Idara ya Polisi nchini Tailand, inasema kwamba milipuko miwili ya mabomu imetokea katika hoteli moja iliyoko katika mji wa Pattani, kusini mwa nchi hiyo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wapatao 30 wakajeruhiwa.

Wote walikuwa raia wa Thailand. Mapema mwezi huu, misururu kadha ya milipuko ilitokea kote nchini Thailand, ikilenga miji ya kitalii.

6. Mwanahabari aliyeigiza 'Yes Minister' afariki

Haki miliki ya picha COURTESY

Na mwanahabari wa zamani wa Uingereza, ambaye pia alikuwa mwaandishi vitabu, Antony Jay, na ambaye pia alihusika katika kuigiza katika filamu moja ya kipindi cha runinga 'Yes Minister' na 'Yes, Prime Minister' -- amefariki akiwa na umri wa miaka 86.