WHO: Uhaba wa vipimo unakwamisha juhudi za kudhibiti HIV

Chupa za vipimo vya HIV Haki miliki ya picha SPL
Image caption Watafiti wanaonya kwamba huenda malengo ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza maambukizi ya HIV yasifikiwe

Ukosefu wa vipimo vya virusi vya HIV vinavyosababisha maradhi ya ukimwi unaweza kuzorotesha juhudi za dunia za kubaini na kuwatibu watu wenye maambukizi ya HIV, wameonya wataalam kutoka Shirika la Afya Duniani.

Walitathmini tafiti za mwaka mzima za WHO zilizofanywa katika nchini 127 kati ya mwaka 2012 na 2014 huku utafiiti huo ukiuliza uwezo na matumizi ya vipimo vya damu vinavyochunguza hali ya HIV na afya.

Watafiti walibaini uhaba wa kutisha katika uchunguzi huo.

Wanaonya kwamba huenda malengo ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza maambukizi ya HIV yasifikiwe.

Malengo hayo yanasema kufikia mwaka 2020, asilimia 90% ya watu wote wanaoishi na virusi vya ukimwi -HIV-watakua wanapata dawa za -antiretroviral -zinazopunguza makali ya Ukimwi na kwamba asilimia 90% ya watu hao wanapaswa kuwa wanapata "dawa ya kudumaza virusi hivyo".

Vipimo vya maabara ni muhimu kuweza kufikia malengo haya.

Lakini Vincent Habiyambere na wenzake wanasema katika jarida la kitabibu la PLoS kwamba baadhi ya nchi zenye kipato cha chini na cha wastani, zikiwemo zile za mataifa ya Afrika ambako maambukizi ya HIV ni kero kubwa, haziko tayari kwa changamoto hiyo.

Hata hivyo upimaji wa HIV umekuwa ukiongezeka kwa miaka, lakini bado kuna mapungufu katika baadhi ya maeneo ya dunia.