Askari Polisi wanne wauwawa nchini Tanzania

Nsato Marijani-Kamishina Operesheni na Mafunzo nchini Tanzania
Image caption Nsato Marijani-Kamishina Operesheni na Mafunzo nchini Tanzania

Polisi wanne wameuwawa na raia wawili kujeruhiwa baada ya kushambulilwa na watu wenye silaha ambapo pia walipokonya bunduki mbili na risasi kadhaa huko mjini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Hadi sasa bado haijajulikana chanzo cha mauaji japo polisi wanasema wanahisi tukio ni la ulipizaji kisasi dhidi ya polisi.

Jeshi la polisi , chini ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijani limedhibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilikuwa ni la uvamizi wa moja ya benki jijini Dar es salaam ,huku wakiwa na ulakini wa mazingira ya uhalifu huo.

Amesema inaonekana kuwa tukio hilo halikulenga kuivamia benki bali lililenga kuua askari ili kulipiza kisasi kwa kuwa hakuna kitu chochote kilichopotea au kuharibika katika benki hiyo.

Aidha Jeshi hilo limesema kuwa kuna baadhi ya watu waliandika mitandaoni kushabikia mauaji ya askari hao na kukejeli mazoezi waliokuwa wakifanya,huku baadhi ya viongozi wa kisiasa, kusikika katika majukwaa yao wakiwahamasisha wafuasi wao kuwashambulia polisi.Hatua hiyo imepelekea jeshi la polisi kutoa onyo kwa kukemea tabia hiyo;na kuhaidi kuwafuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliofanya uchochezi wa tukio hilo kwa namna moja au nyingine.

Pamoja na hayo Jeshi la polisi limesitisha pia mikutano ya ndani yenye wasiwasi wa kuchochea uhalifu kwa kuwa wamebaini mikutano hiyo imekuwa ikitumika kuhamasisha uhalifu.