Muhtasari: Habari kuu leo Alhamisi

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, waasi wa FARC nchini Colombia wametia saini mkataba wa amani, na idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko Italia imefika 160.

1. Waasi wa FARC watia saini mkataba wa amani Colombia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waasi wa FARC wameendeleza vita dhidi ya serikali kwa karibu miaka 50

Serikali ya Colombia na kundi la waasi la FARC, zimetia saini muafaka wa amani, na kumaliza mzozo na uhasama uliodumu miaka hamsini.

Pande zote mbili zimekubaliana kufanya kazi pamoja ili kuangazia umoja na utangamano na kudumisha amani. Muafaka huo sasa ni sharti uidhinishwe na kura ya maoni itakayopigwa na wa Colombia wote hapo mwezo Oktoba tarehe 2.

2. Waliofariki kutokana na tetemeko Italia wafika 247

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Juhudi za uokoaji zimeendelea usiku kucha

Shirika la msalaba mwekundu nchini Italia, linasema kuwa idadi ya watu waliofariki katika janga mbaya la tetemeko la ardhi lililosambaratisha miji na vijiji kadha katika maeneo yenye milima katikati mwa nchi hiyo hapo jana Jumatano imepanda na kufikia zaidi ya 247.

Makundi ya uokoaji yanaendelea kusaka manusura ndani ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka katika majimbo ya katikati ya nchi hiyo ya Umbria, Lazio na Marche.

3. UN yasema serikali ya Syria imetumia mabomu ya kemikali

Haki miliki ya picha AFP

Umoja wa Mataifa umesema kuwa serikali ya Syria imetumia mara mbili mabomu ya kemikali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Pia imebainika kuwa kundi la wapiganaji la Islamic State limetumia gesi ya sumu katika shambulio moja.

4. Kiongozi wa Brexit ahutubu mkutano wa Trump

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bw Nigel Farage

Mwanasiasa mmoja wa Uingereza aliyeongoza kampeini ya kujiondoa kutoka ndani ya Umoja wa Ulaya (EU), Nigel Farage, amehutubia mkutano mmoja wa kampeni za urais wa chama cha Republican nchini Marekani.

Huku Bw Trump akisimama sako kwa bako naye, kinara huyo mkuu wa chama cha UK Independence Party (UKIP) anayeondoka, aliwaambia wafuasi wa Republican kuwa, mengi yanawezekana watu watasimama kidete kupinga uongozi wowote ule.

5. Wahandisi waunda roboti inayojitosheleza

Haki miliki ya picha R TRUBY/M WEHNER/L SANDERS/HARVARD UNIVERSITY

Wahandisi wa chuo kikuu cha Harvard nchini Marekani, wamesema kuwa wameunda roboti yenye uwezo wa kufanya kazi kivyake bila ya usaidizi wa kuongozwa na mwanadamu. Imeundwa kutokana na silicone gel na kina fanana na pweza.

6. Watu 13 wauawa chuo cha Marekani Kabul

Haki miliki ya picha Reuters

Na kumetokea shambulio la bomu katika Chuo Kikuu cha Marekani mjini Kabul.

Walinda usalama wamefaulu kuwauwa kwa risasi washambuliaji wawili.

Washambuliaji hao waliwauwa watu 13. Mashambuilizi katika Chuo hicho kikuu yalianza hapo jana Jumatano kwa mlipuko mkubwa wa bomu kisha kufuatiwa na mashambulio ya risasi iliyowalazimu baadhi ya wanafunzi kuruka kutoka Orofa ya pili ya majengo ya chuo hicho kikuu.

Zaidi ya watu 30 walijeruhiwa.