Muhtasari: Habari kuu leo Ijumaa

Miongoni mwa habari kuu leo, waziri ameuawa na wachimba migodi Bolivia, waasi wakaruhusiwa kuondoka Daraya, Syria na Marekani imefyatua kombora kuonya mashua ya Iran.

1. Wapiganaji na raia waruhusiwa kuondoka Syria

Haki miliki ya picha AFP

Makubaliano yameafikiwa ya kuwaruhusu raia na waasi kuondoka mji wa Syria, Daraya, ambao umekuwa ukizingirwa na vikosi vya serikali kwa muda mrefu.

Pande zote mbili zinasema zoezi hilo litaanza hivi leo.

2. Marekani yafyatua kombora kuonya mashua ya Marekani

Haki miliki ya picha US NAVY

Pentagon inasema mashua ya kivita ya marekani imefyatua makombora kadhaa ya kuionya Iran, baada ya mashua yake ya kivita iliyo na uwezo wa kufyatua kwa kasi, kukaribia mashua za marekani katika eneo la ghuba.

Msemaji wa pentagon anasema kisa hicho sio cha kwanza wiki hii, ambapo mashua za Iran zimekuwa zikitekeleza shughuli zake kwa njia aliyoelezea kuwa, isiyo salama na inayokiuka sheria.

3. Italia yatangaza hali ya hatari katikati mwa Italia

Haki miliki ya picha EPA

Waziri mkuu wa Italia ametangaza hali ya tahadhari katika maeneo ya katikati mwa taifa hilo, ambayo yalikumbwa na tetemeko baya la ardhi, ambapo watu 250 waliaga dunia. Matteo Renzi ameahidi kwamba pesa zaidi na rasilimali zitaongezwa, baada ya serikali kutoa euro milioni 50 kutoka kwenye hazina ya dharura, kusaidia waathiriwa.

4. Mwogeleaji Mmarekani Ryan Lochte ashtakiwa Brazil

Haki miliki ya picha Getty Images

Polisi nchinio Brazil wamemshtaki mwogeleaji wa marekani Ryan Lochte, kwa makosa ya kutoa taarifa za udanganyifu, baada ya madai yake kwamba, yeye pamoja na wenzake watatu waliporwa na watu waliojihami kwa bunduki, wakati wa michezo ya olimpiki mjini Rio. Madai hayo yamebainika kuwa ya uwongo. mwogeleaji huyo anakabiliwa na kifungo cha miezi 18 gerezani.

5. Waziri auawa na wachimba migodi Bolivia

Tuelekee nchini Bolivia ambapo, vyombo vya habari vinaripoti kwamba naibu waziri wa usalama wa ndani ametekwa nyara na wachimba migodi wanaofanya mgomo, na kwamba huenda ikawa ameaga dunia. Rodolfo Illanes, alitekwa nyara kwenye kizuizi cha barabarani eneo la Panduro, takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu wa La Paz.

6. Mradi wa kuzuia mimba wafeli Australia

Haki miliki ya picha AP

Nchini Australia, Mradi unaolenga kupunguza idadi ya wasichana wanaopata mimba ya mapema kwa kutumia watoto bandia, huenda limesababisha matokeo ambayo hayakuwa yanatarajiwa ama ambayo hayakutakikana. Zaidi ya wasichana 1000, walitakiwa kutunza watoto bandia ambao walikuwa wakipiga mayowe na kutoa sauti za kunyongwa na chakula. lengo lilikuwa, kuwazuia kupata mimba ya mapema. Baadaye ilibainika kwamba, wasichana walioshiriki katika mradi huo, walikuwa na uwezekano mara mbili wa kupata mimba ya mapema kuliko wale ambao hawakushiriki katika uchunguzi huo.